loader
Dstv Habarileo  Mobile
Nyumba 116 za watumishi wa afya 3448 kujengwa

Nyumba 116 za watumishi wa afya 3448 kujengwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema sehemu ya Sh bilioni 226.68 zilizotengwa kwa ajili ya huduma za afya msingi, zitatumika kujenga nyumba za watumishi 116 zitakazochukua watumishi 348.

Ummy ameyasema hayo wakati wa kuelezea mgawo wa fedha Sh bilioni 535.6 kati ya Sh trilioni 1.3 ambazo serikali imepokea kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupambana na athari za ugonjwa wa Covid-19 kupitia Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano ya Covid-19.

Ummy aliwaambia waandishi wa habari jijini Dodoma jana kuwa maeneo yatakayojengwa nyumba hizo ni yaliyopo pembezoni hasa vituo vilivyo mbali na makao makuu ya halmashauri, mbugani, visiwani, milimani na maeneo yenye changamoto za kufikika kirahisi. 

“Kwa mantiki hii, halmashauri za majiji, manispaa na miji hazikupewa kipaumbele kwenye mgawo huu,” alisema.

Ummy alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya afya pia zinaenda kuanzisha Huduma za Dharura (EMD) katika halmashauri 75 na kujenga majengo ya huduma za wagonjwa mahututi 25 katika halmashauri 25 za kimkakati.

Alisema ujenzi wa miundombinu ya huduma za dharura ni pamoja na maeneo yenye idadi kubwa ya watu, maeneo yenye umbali mrefu wa upatikanaji wa huduma za dharura, maeneo yenye milipuko ya magonjwa ya mara kwa mara na muingiliano mkubwa wa watu na maeneo yenye changamoto za ajali za mara kwa mara (barabara kuu).

Aidha, Ummy alisema pia serikali itajenga mitambo mitano ya kuzalisha oksijeni (Oxygen Plant) ambayo itapelekwa katika halmashauri za wilaya tano za Karatu, Mlele, Bunda, Masasi na Nyasa. Kila moja imetengewa Sh milioni 600. 

“Pia halmashauri hizi pia zitapata mitambo mitano ya kusambaza oksijeni wodini sambamba na halmashauri nyingine 68 zilizopo kwenye maeneo yenye ajali hasa kwenye barabara kuu, maeneo yenye milipuko ya magonjwa ya mara kwa mara,” alifafanua Ummy.

Kuhusu ununuzi wa mitambo 60 huduma ya mionzi, Ummy alisema itapelekwa kwenye maeneo ya mbali, idadi kubwa ya watu na maeneo yenye matukio ya ajali za mara kwa mara.

Alisema pia serikali itanunua magari ya kubebea wagonjwa 195 na kugawiwa katika halmashauri zote 184 na pia magari 212 kwa ajili ya usimamizi na uratibu wa shughuli za afya, ustawi wa jamii na lishe na usambazaji wa bidhaa za afya katika mikoa yote 26 na halmashauri zote 184. 

“Halmashauri zinahimizwa kupelekwa ambulance hizi katika vituo vya afya vilivyo mbali sana kutoka katika hospitali za halmashauri ili kuwezesha huduma za rufaa kwa wagonjwa,” alisema Ummy.

Alisema pia serikali itanunua na kusambaza vifaa na vifaa tiba ikijumuisha vitanda na mashuka yake 2,208, mashine za usingizi 60, taa za upasuaji 60, majokofu ya kutunzia damu na mavazi kinga (PPE) kwa ajili ya wataalamu wetu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b64f4eede50c0720e1319f460f863950.jpeg

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi