loader
Rais Samia alivyotumia fedha za IMF/Covid-19 ni somo kwa Afrika

Rais Samia alivyotumia fedha za IMF/Covid-19 ni somo kwa Afrika

KWA miongo kadhaa kumekuwa na mjadala kwamba Afrika haiwezi kuendelea kwa kutegemea misaada na zaidi utegemezi wa misaada umehusishwa na kuongezeka kwa umasikini wa Bara la Afrika.

Nikumbushe alichoandika mchumi nguli, Dambisa Moyo kwenye kitabu chake DEAD-AID, amesisitiza hoja hiyo katika ukurasa wa 11. Ameonesha kuwa, wakati kiwango cha misaada kwa Bara la Afrika kilikuwa juu zaidi katika miaka ya 1970 mpaka 1998. Hicho ni kipindi ambacho Afrika ilitoka kuwa na asilimia 11 ya masikini wote duniani mpaka asilimia 66.

Wapinzani wa hoja kuwa misaada inaongeza umasikini wamejenga hoja yao katika misingi kuwa tatizo ni udhaifu wa serikali za Afrika katika kupanga na kutekeleza matumizi ya fedha za misaada kutokana na rushwa, ufisadi, matumizi mabovu na zaidi kupangiwa matumizi na watoaji mikopo na misaada.

Zaidi, wanasema misaada ni sababu ya umasikini wakisisitiza hoja yao kwa kurejea mfano wa namna msaada wa Marekani chini ya mpango wake wa ‘Marshal plan’ wa dola za Marekani bilioni 15 ulivyofufua uchumi wa Ulaya baada ya Vita ya Pili ya Dunia.

Kwamba Afrika kutoka kuwa bara lenye asilimia 11 ya masikini wote duniani miaka ya 1970 mpaka zaidi asilimia 70 ya masikini mwaka 2019 na inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2030, bara litakuwa asilimia 87 ya masikini wote duniani.

Ni hoja yangu kwamba kilichotokea kwenye msaada/mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Covidi-19 kwa nchi za Afrika, kinathibitisha hoja ya kwanini tatizo si misaada bali wanaopewa misaada! Wakati mataifa mengi Afrika yametumia sehemu kubwa ya fedha za IMF za kupambana na ugonjwa huo kwa semina, warsha, kampeni, ununuzi wa vifaa tiba nakadhalika, Rais wetu Samia Suluhu Hassan amefanya tofauti kwa lengo lile lile!

Ndio msingi wa hoja kwamba Rais Samia amejenga hoja IMF na kukubalika kwamba kukabili Covid-19 Tanzania inahitaji kuongeza madawati na madarasa ili wanafunzi wasibanane darasani na hivyo kupunguza uwezekano wa kuambukizana.

Kwa sababu hii, Rais Samia amefuta tatizo la madawati na madarasa kwa mwaka 2022 kwa kutenga sehemu ya fedha za IMF kukamilisha maboma ya madarasa 15,000 na madawati 462,795. Kwamba yanunuliwe magari 25 ya kuchimba visima kila mkoa na mitambo mitano ya kuchimba mabwawa ili kupunguza tatizo la upatikanaji maji kama njia ya kukabili ugonjwa huo.

Nakumbuka Ripoti ya Taasisi ya Tafiti za maoni ya Synovate ambayo ni ya tano kwa ukubwa duniani, mwaka 2008 ilionesha kuwa maji ndio ilikuwa kero namba moja Tanzania. Hivyo Rais Samia anatumia fedha za IMF/Covid-19 kukabili tatizo la maji ambalo ni ajenda ya nchi hata kabla ya ugonjwa huo.

Ametumia tatizo la ugonjwa kukabili upungufu wa magari ya kubeba wagonjwa kwa kununua magari hayo 395 yatakayosambazwa vituo vya afya na hospitali nchi nzima! Na kwamba tuongeze vyuo vya ufundi (Veta) 32 ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kuepuka kuambukizana. Yote hii ni kwamba Rais anatekeleza ajenda ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi kiasi kwa kutumia fedha hizo.

Ni wazi kama Bara la Afrika lingekuwa na viongozi wenye fikra kama za Rais wetu kuhusu matumizi ya mikopo nafuu na misaada, wana wa Afrika wangeona tofauti kubwa sana kwenye mataifa yao. Ukisoma taarifa ya IMF ya Oktoba 8, mwaka huu, dola bilioni 26.46 (zaidi ya Sh trilioni 60.86) zilikwishatolewa kwa ajili ya kukabili ugonjwa huo kwenye nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Lakini ndio hivyo, wengi zimeishia kuagiza barakoa na vifaa vya hospitali, semina, warsha na makongamano ya kujengeana uwezo wa namna ya kujikinga na Covid-19. Wakati Tanzania imepata dola za Marekani bilioni 567, Rais Samia anakuja na mpango ambao si tu wenye uwazi na tija kubwa kwenye uchumi wa nchi, bali uwazi wa kiwango cha juu hata kufanya Watanzania kuona fahari ya mkopo husika.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/5a789683eaeaee0c621335677f1a2ad4.jpeg

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Na David Kafulila

1 Comments

  • avatar
    Laurent Ndichaye
    20/10/2021

    Hoka zako zina mshiko.lakini hujatufafanulia jinsi fedha hizo zitakavyolipwa.Je,shule binafsi na taasisi binafsi zitapewa fedha hizo kwa ajili ya madarasa au madawati ?Kwa mfano shule za jumuiya ya wazazi .

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi