loader
Dstv Habarileo  Mobile
Polisi wanaokiuka maadili, sheria waonywa

Polisi wanaokiuka maadili, sheria waonywa

KAMISHNA wa Polisi wa Ushirikishwaji wa Jamii, Dk Mussa Ali Mussa, amewaonya askari ambao wamekuwa wakikiuka misingi ya sheria ndani ya jeshi hilo katika kutenda haki kwa wananchi, akiwataka kuacha mara moja tabia hiyo.

Halikadhalika amesema yapo mambo yanafanywa na askari polisi kwa sasa, ambayo yakiachwa yaendelee, yataharibu na kubadilisha sura ya Jeshi la Polisi nchini jambo ambalo halikubaliki.

Dk Musa aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo ngazi ya koplo namba mbili ya mwaka 2021/2022, katika Shule ya Polisi Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambako alisema baadhi ya askari wamekuwa wakikiuka maadili na misingi ya sheria.

Alisema ni wajibu wa askari polisi kuhudumia jamii kwa uadilifu, uaminifu, utii, haki na uzalendo. Alisisitiza kuwa wanapaswa kutoa huduma nzuri kwa wananchi kwa kufuata sheria na kuacha ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo kubambikia kesi.

“Mkafanye kwa uadilifu, utii na uaminifu mkitanguliza uzalendo mbele, wapo baadhi ya askari ambao wanakwenda kinyume na maadili, niwaombe msiwe na tabia hizo maana hatutasita kuwachukulia hatua,” alisema Dk Musa.

Aidha, alisema yapo baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na askari ambayo yamekuwa yakikiuka misingi ya taaluma za jeshi hilo ambayo ni pamoja na utovu wa nidhamu, uvaaji mbovu pamoja na askari kutofanyiwa ukaguzi wakati wakiingia kazini.

“Tunaingia kazini kila mtu anaingia kwa wakati wake, hakuna ukaguzi, matokeo yake sasa mtu anatoka na ‘hang over’ anaingia kazini na wakati mwingine tunampa silaha, turejeshe utaratibu wa kufolenisha, kuwakagua askari kujua nani mzima, nani anaumwa na nani amekuja katika mazingira mengine,” alisema.

Alisema mambo mengine ni uvaaji mbovu wa baadhi ya askari hususani kutovaa sare za jeshi hilo inavyotakiwa na kwamba ni wajibu wa viongozi hao kwenda kusimamia masuala yote ya kinidhamu. Pia aliwataka askari hao kwenda kushughulikia makosa mbalimbali ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ulawiti ambayo yameendelea kushika kasi katika jamii.

Mkuu wa Shule ya Polisi -Moshi, Ramadhani Mungi alisema jumla ya wanafunzi 4,260 walifanya mtihani na 4,237 ndio waliofaulu huku 23 walifeli.

Mungi alisema miongoni mwa mafunzo waliyopewa askari hao ni jinsi ya kubaini na kutambua uchochezi na viashiria vya ugaidi pamoja na masuala ya jinsia, unyanyasaji wa wanawake na watoto pamoja na mbinu za medali za kivita

foto
Mwandishi: Na Upendo Mosha, Moshi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi