loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mil 400/- zajenga mabwawa manne vijijini

Mil 400/- zajenga mabwawa manne vijijini

ZAIDI ya Sh milioni 400 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa manne ya maji katika vijiji vinavyopakana na hifadhi za taifa za mikoa ya Kilimanjaro na Manyara kudhibiti muingiliano wa wanyamapori na binadamu.

Meneja wa mradi wa shirika linalojishughulisha na usimamizi wa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira Tanzania (WWF), Novat Kessy, alisema hayo wakati wa semina ya mafunzo ya kamati nne za usimamizi wa mabwawa hayo, iliyofanyika jana Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kessy alisema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wanyama kutoka hifadhini na kwenda kuvamia makazi ya watu na kusababisha vifo na madhara kutokana na wanyama kutafuta maji jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro na muingiliano mkubwa.

“Tumechimba mabwawa mawili katika Wilaya ya Longido na mengine Same na Mwanga na kutengeneza maeneo maalumu kwa ajili ya kunyweshea wanyama, kila bwawa linagharimu zaidi ya Sh milioni 100 lengo likiwa ni kudhibiti muingiliano wa wanyamapori na binadamu,” alisema.

Aidha, alisema mabwawa hayo ambayo yamejengwa karibu na hifadhi hizo ni kwa ajili ya kunyweshea mifugo pamoja na wanyamapori ambao wamekuwa wakitafuta maji kwa kutembea umbali mrefu kutoka hifadhini.

“Pamoja na kuchimba mabwawa katika vijiji vinavyopakana na hifadhi za taifa katika ukanda huu pia tumechimba mabwawa ndani ya hifadhi ya mkomazi, hii itasaidia pia kupunguza idadi ya wanyama wanaotoka hifadhini,” alisema Kessy.

Aliongeza: “Tunafanya kazi katika ikolojia nne za Ziwa Natroni, Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Mkomazi kwa kutekeleza mradi wa mabadiliko ya tabia nchi tukifadhiliwa na Serikali ya Ujerumani na mafunzo haya ni kwa ajili ya kuzijengea uwezo jumuiya hizi za kijamii kutekeleza wajibu wake ikiwemo kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori.”

foto
Mwandishi: Na Upendo Mosha, Moshi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi