loader
Dk Mwinyi: Tudumishe muungano, biashara isiwe na bughudha

Dk Mwinyi: Tudumishe muungano, biashara isiwe na bughudha

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amewataka Watanzania kuendelea kudumisha Muungano kwa kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kufanya biashara bila bughudha yoyote.

Alisema hayo jana baada ya kuzindua miradi minne ya Jeshi la Magereza iliyopo mkoani Morogoro.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa nafasi ya kuhudhuria shughuli hiyo ya uzinduzi wa miradi minne ya Ngome ya Gereza la Mkono wa Mara, jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto, nyumba za makazi ya maofisa na askari pamoja na kiwanda cha maziwa cha Kingolwira kwa niaba yake.

Pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

Dk Mwinyi alisema kuwa mongoni mwa faida za Muungano ni wananchi wa pande zote mbili za muungano kufanya biashara ikiwemo mchele.

“Kama tunavyotambua kule Zanzibar ni walaji wakubwa wa mchele ambao mwingi unatoka Tanzania Bara ikiwemo Morogoro, hivyo tuendelee kudumisha Muungano wetu kuhakikisha wananchi wetu wanapata fursa ya kuendelea kufanya biashara bila ya bughudha yoyote,” alisema.

Kuhusu miradi ya Jeshi Magereza nchini, Dk Mwinyi alisema kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Jeshi hilo, hiyo ni sehemu ya miradi mingi inayoendelea kutekelezwa na jeshi hilo ndani ya mkoa huo na maeneo mbalimbali nchini.

Alisema hatua ya Jeshi la Magereza kuwa na ubunifu wa miradi mbalimbali ya maendeleo inafaa kuigwa kwani ni kielelezo kizuri kwa taasisi nyingine kujiongeza na kujipatia kipato kutoka kwenye miradi yao pamoja na kuimarisha ustawi wa maisha ya wananchi ya kuwapatia huduma mbalimbali.

“Kwa hatua hii kwa mara nyingine napenda kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia Jeshi la Magereza,” alisema.

Dk Mwinyi alisema kuwepo kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni mojawapo ya kigezo kimoja wapo cha tathimini ya maendeleo katika nchi yoyote na miradi hiyo huleta manufaa kwa jamii na ni dhahiri kiwanda cha maziwa kilichozinduliwa kinaliwezesha Jeshi hilo kuzalisha, kujiongeza pato na kutoa soko kwa malighafi ya maziwa kwa watu wanaokizunguka.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akimbaribisha Dk Mwinyi alisema majukumu ya msingi ya jeshi hilo kuanzia serikali ya awamu ya tano na ya sita ni kujenga uwezo wa kujitengemea kwa chakula.

Simbachawene alisema jeshi hilo kwa sasa lina uwezo wa kulisha wafungwa na mahabusu kwa asilimia 100.

Alisema kupitia uongozi wa Kamishna Jenereli wa Magereza, jeshi limeweza kujitegemea na kufanikiwa kuokoa takribani shilingi bilioni moja kwa mwezi.

Alisema jeshi hilo katika mikakati ya maboresho limeweza kujenga nyumba mpya za makazi ya askari na maofisa zipatazo 400 na nyingine bado zinaendelea kujengwa nchi mzima “Ninapongeza mkuu wa Jeshi hili, wasaidizi wake pamoja na wafungwa kwa kutekeleza maelekezo ya serikali na kazi kubwa inayofanyika,” alisema Simbachawene.

Kwa upande wake Kamishna Jenereli wa Magereza, Suleiman Mzee pamoja na kueleza mafanikio na changamoto mbalimbali alisema kuwa miradi hiyo minne ambayo ilizinduliwa na Dk Mwinyi kwa pamoja imegharimu kiasi cha Sh milioni 611.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c2e1e2ae5a863461f1f7d98b301a4d02.jpg

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Michael ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi