loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia aifungua Kaskazini

Samia aifungua Kaskazini

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua na kuweka mawe ya msingi kwenye baadhi ya miradi mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili iliyoanza jana na kusema kuwa ameanza rasmi ziara zake mikoani kama alivyoahidi hivi karibuni.

Akiwa mkoani humo jana, Rais Samia alizindua Barabara ya Sanyajuu-Elerai yenye urefu wa kilometa 32.2 ambayo imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 62.7.

Alisema barabara hiyo ilikuwa kero ya siku nyingi na kwamba kukamilika kwake ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inaelekeza kuangalia kero za wananchi na kuzitatua. Barabara hiyo ni sehemu ya Barabara ya Bomang’ombe-SanyajuuKamwanga yenye urefu wa kilometa 98.2.

Inajengwa katika awamu tatu ambapo kipande kilichobaki ni kilometa 44 kutoka Sanyajuu hadi Kamwanga ambazo alisema “wananakwenda kuzimaliza.” Hospitali ya Mawenzi Baada ya uzinduzi huo, Rais Samia pia aliweka Jiwe la Msingi wa Ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kilimanjaro, Mawenzi. Alisema ujenzi wa jengo hilo unagharimu jumla ya shilingi bilioni sita.

Tayari serikali yake imetoa shilingi bilioni tatu na fedha zilizobaki zitapelekwa wakati wowote ili kukamilisha ujenzi. “Sasa niwaombe fanyeni kazi, hudumieni ndugu zenu Watanzania. Jitumeni jinsi mnavyoweza kutengeneza afya za Watanzania ili wapate nguvu na afya ili wakazalishe, taifa letu lisonge mbele,” alisema Samia.

Daraja la Rau Katika ziara hiyo pia aliweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Rau mkoani humo. Alisema daraja hilo lilipoharibika lilisababisha vifo vya watu, hivyo serikali yake imetoa Sh milioni 900 kulijenga upya na ujenzi wake utakamilika mwezi Januari au Februari mwakani Mabango Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwaagiza maofisa wake kukusanya mabango yote waliyokuwa nayo wananchi yaliyoonesha kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.

Moshi kuwa Jiji Rais Samia alisema ombi la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo la kutaka Moshi liwe jiji litafanyiwa kazi japo kwa sasa mji huo haujakidhi vigezo vinavyotakiwa. Alisema kwa kuwa Vunjo waliomba kuwa halmahauri na umbali kati ya Moshi Mjini hadi Vunjo ni takribani kilometa 20, hivyo labda Vunjo ivunjwe iingizwe Moshi ili jiji litanuke na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.

Mlima Kilimanjaro Kwa kuwa Mlima Kilimanjaro ni moja ya vivutio muhimu vya utalii na umeipa Tanzania heshima kubwa, Samia aliwataka wananchi wanaoishi maeneo jirani na mlima huo kuendelea kutunza mazingira ili usiathirike zaidi. “Wakati tunafanya Royal Tour tulikwenda juu ya Mlima Kilimanjaro kwa kutumia ndege na tukauzunguka si chini ya mara sita, hali ya mlima wetu kule juu siyo nzuri. Ile theluji inayeyuka na mlima unamomonyoka.

Niwaombe wananchi tutunze hayo maeneo, mlima ule ni muhimu kwetu kama Taifa, tukisema turuhusu watu waingie, sifa ya mlima ule itapotea,” alisema. Stendi, hospitali Mwanga Kuhusu ujenzi wa stendi kubwa na ya kisasa pamoja na kituo cha afya kikubwa kitakachokuwa na hadhi ya hospitali ya wilaya Mwanga, Samia aliitaka Halmashauri ya Mwanga kupeleka maombi Tamisemi ili yaanze kufanyiwa kazi na kuahidi kuwa kituo cha afya Mwanga nacho kitajengwa ili kitumike kama hospitali ya wilaya.

Tozo Rais Samia alisema tozo za miamala zitaendelea kwa kuwa uimara wa nchi ni kujitegemea na kuongeza kuwa tozo hizo katika miezi mitatu ya mwanzo zimesaidia ujenzi wa vituo vya afya 200 na madarasa 500.

Alisema mwezi mmoja baada ya Tanzania kuweka tozo hizo, Uingereza nayo ilianzisha tozo kama hizo na kuelekeza fedha kwenye sekta ya afya, hivyo Tanzania ilifanya jambo zuri ambalo linaigwa na mataifa mengine. Chanjo Rais Samia aliupongeza Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuitikia kwa wingi kuchoma chanjo ya Covid-19.

Alitoa pongezi hizo baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Stephen Kagaigai kumweleza kuwa dozi 60,000 za chanjo zilizopelekwa mkoani humo ziliisha, ikabidi waombe zingine za ziada ambazo nazo ziko mbioni kwisha. Kagaigai alisema dozi zingine 36,864 za chanjo ya Sinopharm wameshazipokea na zitaanza kutolewa hivi karibuni. KCMC Samia alisema leo ataweka jiwe la msingi katika Hospitali ya KCMC kwenye mradi mkubwa unaojengwa ambao serikali pia ina mkono wake.

Alisema huduma bora za kibingwa zitatolewa hospitalini hapo na kuwa msaada mkubwa kwa nchi. Kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi, Rais Samia alisema serikali yake imetenga fedha na itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za maji, barabara, afya na huduma zingine za kijamii mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema barabara ya Sanyajuu-Elerai itafungua uchumi wa eneo hilo, Tanzania na nchi jirani ya Kenya kwa kurahisisha biashara na utalii. Samia alisema leo atafanya ziara mkoani Arusha na kumpokea Rais wa nchi jirani na kisha ataona aende mkoa gani.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/b86a2e488d4b76be1b4997c5625fa636.jpg

SERIKALI imepanga kujenga ...

foto
Mwandishi: Matern Kayer

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi