loader
Dstv Habarileo  Mobile
Sabaya, wenzake wawili watupwa jela miaka 30

Sabaya, wenzake wawili watupwa jela miaka 30

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili, wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya unyang’anyi wa makundi na kosa moja la unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Wengine ni Silvester Nyengu (26) na Daniel Mbura (38).

Walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika tukio lililojiri Februari 9, mwaka huu katika duka la Shahiid Store linalomikiwa na mfanyabiashara wa Arusha, Mohamed Al Saad.

Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mkoa wa Geita, Odira Amworo iliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kwa siku 37 alitumia muda wa saa 5:45 kusoma hukumu hiyo na kuhitimisha kwamba mahakama yake imewakuta na hatia washitakiwa wote watatu.

Alisema mahakama iliridhishwa na ushahidi wa shahidi wa sita katika kesi hiyo, Bakari Msangi, shahidi wa pili Nurma Jussin na shahidi wa nne Hajirini Saad Hajirini kuwa kabla ya kupora fedha zaidi ya Sh 3,194,000, Sabaya na kundi lake waliwapiga watu wote waliokuwa dukani huku wakiwatishia kwa sihala.

Amworo alisema kwa mujibu wa sheria ya adhabu ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kifungu 287, kila kosa adhabu yake ni miaka 30 jela na viboko 12 kila mmoja.

Alisisitiza kwamba Sabaya na wenzake wamekutwa na hatia katika kila shitaka lakini mahakama imewaonea huruma na kuwafunga miaka 30 jela washitakiwa wote watatu na siyo miaka tisini kwa kila mmoja.

Alisema mahakama imeridhika pasipo shaka yoyote kuwa Sabaya na kundi lake walitenda makosa hayo ya jinai dukani kwa Mohamed Al Saad.

Hakimu Amworo aliukataa utetezi alioutoa Sabaya kuwa alitumwa na viongozi wake wa juu katika operesheni hiyo na kwamba ulikuwa na baraka zote za mamlaka ya juu kufanya operesheni nje ya wilaya yake ya kikazi.

Alisema tukio hilo lilikuwa na nia ovu kwani alilifanya kinyume na maadili ya kikazi kwa kuingia katika jiji la Arusha kinyemela bila taasisi zingine za kiserikali kujua.

Hakimu pia alitupilia mbali utetezi wa Sabaya kuwa wengi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo walikuwa washirika wa Bakari Msangi na kwamba wanaswali pamoja au wengine ni familia moja.

Hakimu alisema huo sio utetezi wenye tija kwa sababu kuswali pamoja au kuwa ndugu, kisheria haizuii kutoa ushahidi kwani kinachotakiwa ni kuthibitisha kile walichokiona bila shaka yoyote ili kuisaidia mahakama kujua ukweli wa kilichotokea.

Kabla ya kusoma adhabu baada ya watuhumiwa kutiwa hatiani, Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Felix Kwetukia aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa kwa sababu wametumia ujana wao kutenda makosa kwa makusudi wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Kwetukia aliomba mahakama

isiwahurumie kabisa watuhumiwa hao na adhabu iwe palepale kwa mujibu wa sheria na kwamba Sabaya alikuwa ni mtumishi wa umma na matendo yake yameidhalilisha mamlaka iliyomteua kutokana na kufanya vitu kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wake, wakili wa Sabaya, Mosses Mahuna aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake kwa kuwa ni kijana mwenye umri mdogo, tegemeo la taifa na ameifanyia mengi nchi, hivyo kumfunga na viboko ni kumuua kimaisha.

Wakili Silvester Kahunduka anayemtetea Nyengu, na wakili Fridorini Gwemelo anayemtetea Mbura wote waliiomba mahakama kupunguza adhabu kwa washitakiwa hao kwa kuwa ni vijana na kwamba kuna watu wanaowategemea.

Katika kesi hiyo, mahakama iliambiwa kwamba Sabaya na wenzake Februari 9 mwaka huu, katika mtaa wa Bondeni jiji la Arusha, wakiwa na silaha walifanikiwa kumpora Bakari Msangi Sh 390,000 na simu mbili na kwamba

kabla ya uporaji walimshambulia kwa kumpiga ngumu, mateke, makofi, kichwa na kumtishia kwa silaha.

Ilidaiwa pia kwamba siku hiyo, Februari 9, Sabaya na wenzake walipora kaunta ya duka la Mohamed Saad kiasi cha Sh 2,769,000, fedha taslimu na kabla ya uporaji walimpiga Jasin ngumi, mateke, makofi, kichwa na kumtisha kwa silaha na kisha kutokomea na kiasi hicho cha fedha kusikojulikana.

Shitaka la tatu la unyang’anyi wa kutumia silaha lililokuwa likiwakabili Sabaya, Nyengu na Mbura mahakama iliambiwa kwamba siku hiyo wakiwa na silaha walimpora simu moja ya mkononi aina ya Tecno, na fedha Sh 35,000 Ramadhani Rashid na kabla ya kufanya uhalifu huo waliwalaza chini watu wote waliokuwa katika duka hilo na kuwapiga kwa ngumi, mateke, vichwa na makofi.

Hata hivyo, baada ya hukumu, Wakili Mosses Mahuna aliwaambia waandishi wa habari kwamba mteja wake na wenzake hawakuridhishwa na hukumu hiyo hivyo watakata rufaa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/77fa31a1d683833a75b340e028ff9495.jpeg

SERIKALI imepanga kujenga ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi