loader
TALGWU yataka usalama kwa maofisa watendaji

TALGWU yataka usalama kwa maofisa watendaji

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kimeiomba Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na waajiri katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaweka mazingira salama kwa ajili ya maofisa watendaji wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima alisema hayo katika tamko la chama hicho kulaani mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya mwanachama wake, mtendaji wa Mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi, Manispaa ya Ubungo, Kelvin Mowo yaliyotokea Oktoba 11, mwaka huu akiwa ofisini kwake.

Alisema TALGWU inalaani vikali mauaji yaliyofanywa dhidi ya mwanachama wao na kuwa kitendo hicho hakikubaliki na ni kinyume cha sheria za nchi, haki za binadamu na wala siyo utamaduni wa Watanzania.

“Ikumbukwe kwamba maofisa watendaji ndio watumishi wa umma wanaofanya kazi kwa karibu kabisa na wananchi kwa kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi,” alisema.

Mtima alisema kitendo cha watu wasiojulikana kumuua kikatili tena akiwa kazini Mowo ambaye mpaka umauti unamfika alikuwa mwanachama wa TALGWU, kinaweza kuleta hofu miongoni mwa watendaji wengine nchini.

“Watendaji wanaweza kujiona wanafanya kazi katika mazingira ambayo si salama, hali hiyo inaweza kusababisha maofisa watendaji kukata tamaa, kuvunjika mioyo na imepunguza ari na morali ya kufanya kazi,” alisisitiza.

Alisema chama hicho kinaviomba vyombo vya dola mara baada ya uchunguzi kukamilika wahusika wote wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe funzo na kukomesha kabisa vitendo hivyo viovu na vya kinyama.

Mowo aliuawa akitekeleza majukumu yake baada ya kuvamiwa ofisini na kukatwa mapanga na kupoteza maisha.

Alizikwa juzi katika makaburi ya Kondo yaliyopo Ununio, Bahari Beach Mkoa wa Dar es Salaam.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b223585e84af2beef27d02086bb1bedb.jpeg

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Michael ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi