loader
Majina ya kihistoria, mitaa Z’bar yanapotea

Majina ya kihistoria, mitaa Z’bar yanapotea

MJI wa Zanzibar umebadilika katika miaka ya hivi karibuni na sehemu kuwa na sura mpya. Hii imefanya sio kupotea kwa sura iliyokuwepo miaka mingi bali hata majina ya sehemu hizo.

Siku hizi ukimuelekeza mtoto au kijana kwenda sehemu kwa kumtajia jina la huo mtaa ambalo alilisikia tokea alipokuwa mdogo mpaka miaka ya 1970 atakushangaa. Si ajabu akakuuliza ndio wapi hao na hajawahi kusikia eneo lenye jina hilo.

Hii inatokana na kuvumbuliwa majina mapya, baadhi yao yakiwa hayana kabisa asili na Zanzibar na mengine mtu anaweza kuona tabu hata kuyatamka hadharani.

Baadhi ya majina yana historia yake katika mji, lakini kwa bahati mbaya hili halonekani na kuachiwa kwenda na maji.
Orodha ya majina ya mitaa ambayo majina yake yamekuwa sehemu ya historia ya mji wa Zanzibar na vitongoji vyake ni ndefu.

Miongoni mwa majina ya hiyo mitaa ni Kwa Bi Jokha, Six Four, Kwa Saidi Kibiriti, Kwa Ndarama, Uwanja wa Ganda, Ngazi Nje, Kwa Salim Beni, Mwembe Kidundo, Uwanja wa Chapapunga na Miafuni.

Majina mengine ni Kilimatindi, Mwembe Sanda, Mabatini, Mbuyu Kidambwita, Mji Mpya, Mkungu Malofa, Kachorora, Kwa Kimoto, Kwa Kamanda, Kiinua Miguu, Kibiriti Ngoma na Mapipa ya Ngozi.

Majina mapya ni pamoja na Bondeni, Kilimani, Kariakoo, Kwa Kisasi, Jazira, Kigamboni, Urusi, Magomeni, Nyerere, Magogoni, Uholanzi, Nyarugusu, Kanyeni na Daraja Bovu.

Watu wengi wanaona hali hii ni nzuri na haina tatizo lolote lile kwa maelezo ya kwamba kila kiingiacho mjini sio haramu. Wanasahau kuwa pia sio kila kinachoingia mjini ni halali na kinafaa kukumbatiwa.

Kwa mfano inakuwaje hata jamii inayojigamba kuwa na historia ya kujivunia na ustaarabu uliokuwa ukipigiwa mfano miaka ya nyuma kukubali kuwa na mtaa unaoitwa Kanyeni.

Au tujiuliza ipo faida gani kulitupa jina asilia na kupachika jina lisiokuwa na asili hata chembe na watu wa Zanzibar?

Hapa nataka kukumbusha jinsi baadhi ya wenzetu nchi za nje wanavyojivunia majina ya asili ya nchi na mitaa yao.

Kwa mfano, mara baada ya kupata uhuru mwaka 1957 nchi ilijulikana kama Gold Coast ilibadili jina na kuweka lile lenye asili na watu wa nchi hiyo. Nalo ni Ghana.
Hivyo hivyo ni kwa nchi zifuatazo na majina yake yaliyowekwa na wakoloni katika mabano ni Benin (Dahomey), Bukirna Faso (Upper Volta), Malawi (Nyasaland), Zambia (Northen Rhodesia), Zimbabwe (Southern Rhodesia), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (Congo Leopodville), Namibia (South West Africa) , Djibuti (Afars and Isars), Lesotho (Basutoland), Botswana (Bechuanaland) na Guinea (French Guinea).

Baadhi ya nchi pia zimebadili majina ya miji kama Laurenqo Marques kuitwa Maputo (Msumbiji) na  Salisbury kuitwa Harare (Zimbabwe).
Kwa upande mwengine inafaa kuzingatia wasia wa wazee usemao: ‘Usiwache cha mbachao kwa msala upitao”.

Usemi huu unasisitiza umuhimu wa mtu kulinda na kuhifadhi historia yake kwa sababu baadhi ya haya majina yana  sehemu yake katika historia ya mji wa Zanzibar.

Ni vizuri kwa Wazanzibari kuitafakari hali hii kwa sababu ni kwa kuelewa tu unakotoka ndio unaweza kwenda safari yako kwa usalama bila ya kujikwaa au kutuleza.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/235da3c53d1a728cea3a5c0e08264160.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Na Salim Said Salim

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi