loader
Watoto wa kike Kilwa wanavyopambana na hali zao

Watoto wa kike Kilwa wanavyopambana na hali zao

UTAFITI uliofanywa na Jukwaa huru la Wanawake wilayani Kilwa, TUJIWAKI, umebaini maovu mengi yanayofanyika miongoni mwa wanafunzi ambayo yanahatarisha ustawi wa mtoto wa kike katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.

Kutokana na umaskini na kutojaliwa kwa mtoto wa kike, mabinti wamekuwa wakitumika kama chombo cha starehe huku wengine wakiwa na moyo wa kushawishi wavulana wawashike sehemu zao za faragha ikiwamo matiti na makalio wakati wapo chooni au hata katika makundi na kupokea malipo ya Sh 1,000.

Pia wapo wavulana hushawishi wasichana kukengeuka kimaadili na kukubali kufanya nao mapenzi kwa ujira wa Sh 10,000. Pamoja na maelezo hayo ya mambo ya aibu wanayofanya wanafunzi, Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2016 zinaonesha kwamba Mkoa wa Lindi ambao Wilaya ya Kilwa imo, kwa wastani wananchi wake wamevuka kiwango cha umaskini uliokithiri cha watu kuishi chini ya dola moja kwa siku.

Imeelezwa kuwa mwaka 2009 pato lilikuwa Sh 767,948 na mwaka 2015 liliongezeka na kufikia Sh 1,901,044 ikiwa ni ongezeko la asilimia 148 kwa wastani wa ongezeko la asilimia 21 kwa mwaka.

Pia pato la mkoa limeendelea kuongezeka kutoka Sh 695,361,000 mwaka 2009 hadi kufikia Sh 1,690,403,000 mwaka 2015, hili ni ongezeko la asilimia 143 kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka.

Hata hivyo katika tovuti ya mkoa kumeelezwa kuwa pamoja na kuwepo kwa ongezeko hilo la kipato bado kuna changamoto kubwa ya umaskini miongoni mwa wananchi.

Katibu Mkuu wa Tujiwaki ambaye pia ni msaidizi wa kisheria, Pili Kuliwa akizungumza na mwandishi wa makala haya anasema kwamba utafiti wenye majibu ya wanafunzi kushiriki vitendo vya aibu kwa ajili ya kujikimu na mambo mengine ya kuudhi ulifanywa mwaka huu.

Anasema ulifanyika kwa ufadhili wa Mashirika ya ActionAid na TCRS Kilwa kutokana na kuonekana kuwa kuna wimbi kubwa la mdondoko wa wanafunzi na watoto wa mtaani wilayani humo.

Anasema kukosekana kwa mabadiliko huendana na matakwa ya sasa ya dunia na kung’ang’aniwa kwa mila ambazo zinamfanya mtoto wa kike kutokuwa na nafasi katika jamii. Hali hiyo imesababisha mgongano wa kifikra na kuwafanya wasichana wengi kufanya njia ya mkato kurahisisha maisha yao, wakiamini kwamba wanawamudu wanaume.

Mathalani anasema katika tafiti hizo pamoja na wasichana hao kueleza wanachofanya kujikimu pia walisema kuna haja ya wasichana kupelekwa kwenye unyago wakishamaliza miaka 14 na zaidi kwani kipindi hicho kwa malezi mazuri wanaweza kuanza kuwajibika si kama sasa wakifundishwa ukubwa kabla ya akili zao kukomaa.

Pia wanafunzi hao katika mahojiano kwenye mikutano, kwa mujibu wa Kuliwa, walizungumzia familia kuwa chanzo cha mabadiliko yao kifikra kutokana na matatizo ya kutelekezwa na wazazi, baba zao kutojali na pia wazazi kukaribisha wageni ambao si waaminifu kwa watoto na kuwafanyia ukatili unaomalizwa kifamilia lakini ukiwa na kovu kubwa kwa maisha yao.

Suala la utelekezaji wa watoto limezungumzwa na mfanyakazi wa Action Aid ambaye ni mhamasishaji wa masuala ya wanawake na vijana, Joyce Kessy. Anasema kwamba tafiti walizofanya zinaonesha utelekezaji watoto ni tatizo kubwa linalosababisha watoto wa mitaani na mdondoko wa wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari.

Anasema wamebaini kwamba mahusiano yanapovunjika wazazi wa kiume huacha mzigo wote kwa wazazi wa kike (mama) ambao nao kutokana na kuzidiwa wanashindwa kutoa malezi bora kwa watoto.

Kessy anasema Wilaya ya Kilwa inaongoza katika utelekezaji watoto kutokana na familia kutengana kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kuanzisha familia katika umri mdogo, (hasa watoto wa kiume kuoa mapema kabla ya wakati).

Anasema kutokana na mazingira yaliyopo wao wakishirikiana na majukwaa mbalimbali ya wanawake na vijana wilayani humo huzunguka kutoa elimu na pia kuendesha miradi ambayo husaidia kuwakomboa watoto wa kike.

“Hiki ni kizazi cha kidijiti lakini ni kizazi chetu kinahitaji kuelekezwa ili kuweza kusonga mbele kwa kuwezesha fursa sawa kwa watoto wa kike na kiume,” anasema Kessy. Anasema watoto wa kiume wakifundishwa kuheshimu dada zao jamii itakuwa na nafasi kubwa ya kulea watoto wa kike kwa usalama. Kuliwa anasema kwenye utoaji wa elimu ya haki ya mtoto wa kike pia wamebaini kwamba shughuli mbalimbali za kijamii zimekuwa na urithi mbaya kwa watoto wa kike na kuwavurugia maisha yao ya baadae.

Anasema pia katika kuwapatia wanafunzi nafasi ya kujieleza wamewaambia kwamba kuna changamoto ya walezi kuwataka kimapenzi watoto wa kike wanaowalea, kukaribisha ndugu ambao wanawabaka n.k.

Anasema taasisi ya Tujiwaki kwa ufadhili mbalimbali wameweza kufanya utafiti uliozaa mafunzo na mikutano katika kata za Masoko, Kivinje/Singino, Miteja, Tingi, Lihimalyao, Njinjo, Mingumbi na Namayuni na kuzungumza na watoto wa kike moja kwa moja katika shule za msingi na sekondari za Kilwa, Kivinje, Lihimalyao, Miteja, Namayuni; na shule za msingi za Ukombozi, Mnazimmoja, Singino, Matandu, Miteja, Mtukwao, Mtandango, Naipuli, Mingumbi na Namayuni ambapo watoto wa kike 1,760.

Watoto 1,200 ni wa msingi na 560 sekondari. Mambo mengi ya aibu yanayofanyika miongoni mwa wanafunzi katika makundi na vyoo vya shule zao yanadaiwa kulenga kupata mahitaji na kupunguza dhiki za umaskini.

Mambo mengine yanatokea ambapo katika siku ya mtoto wa kike juma lililopita yalizungumzwa katika warsha mjini Kilwa, ni kuona haja ya shule zote kujengewa hosteli kutokana na watoto wengi kupangishiwa nyumba na wazazi wao na hivyo kuwa huru kufuata mihemko yao huku wakiwa na elimu ya unyago lakini hawana elimu rika inayowasaidia kudhibiti mihemko.

Katibu Tawala wa Kilwa, Haji Balozi anasema katika mazungumzo yake kwamba wazazi ni lazima watoe malezi ya kweli kwa watoto wakati serikali inahangaika kurekebisha mazingira na kusimamia haki za mtoto wa kike.

Balozi anaitaka jamii kubadilika na kusaidia serikali kumwendeleza mtoto wa kike kwa kuhakikisha vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto vinafikishwa katika vyombo vya usalama ili wahusika wapate adhabu kali na kuwa funzo kwa wengine.

Anasema kwa sasa serikali ina mikakati mbalimbali inayochukua kukabiliana na vitendo hivyo wilayani Kilwa ikiwamo kuwapeleka mbele ya sheria wahusika wote akitolea mfano mzazi aliyedaiwa kulawiti watoto wake maeneo ya Somanga shauri lake lipo mahakamani na aliyelazimisha kutembea na binti yake wa kambo naye lipo mahakamani.

Mwanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa, Elizabeth Kalonga kwa upande wake anawataka watoto kujiondoa katika tamaa za kurahisisha maisha na kwa kukubali kiholela wanapotongozwa au kujinadi kushawishi wavulana kwa sababu za umaskini.

Pia katika mahojiano anasema wazazi ni lazima kupata muda wa kukaa na watoto kuwaelimisha kuhusu makuzi yao na wajibu katika taifa. Anasema wakati mwingine tamaa za watoto zinasababishwa na changamoto zilizopo majumbani ambapo zikimalizwa hakutakuwa na shida.

Akizungumzia changamoto za wasichana dawati la jinsia, Mariam Raymond anasema kwamba jamii inasababisha ugumu katika maisha ya watoto wa kike kutokana na kukataa kushirikiana na Polisi kuwapatia haki watoto hao haki zao baada ya kudhulumiwa.

Alisema makosa mengi wanayokutana nayo katika dawati kama mimba za utotoni yanashindwa kupata ufumbuzi kutokana na mabinti wenyewe na wazazi kuficha wahusika.

Mmoja wa wakazi wa Kilwa, Mwanaidi Bilal anasema kwamba mila na desturi zimekuwa kikwazo kikubwa katika maendeleo ya mtoto wa kike. Anasema mila hizo zinawaona watoto wa kike hawana nafasi katika jamii na hivyo kutosaidiwa kufikia malengo.

Msaidizi wa kisheria Kuliwa anasema pamoja na juhudi za taasisi mbalimbali za kumuelimisha mtoto wa kike, serikali inatakiwa kuingilia kati na kusoma tafiti hizo na mapendekezo yake ili kukomesha mdondoko wa wanafunzi na kumsaidia mtoto wa kike kufikia ndoto zake.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7e7ed680759fba2c0f8e2b836be1c1d5.JPG

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: BEDA MSIMBE

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi