loader
Ongezeko hili la watoto gerezani halikubaliki

Ongezeko hili la watoto gerezani halikubaliki

TAARIFA ya Mkuu wa Magereza Wilaya ya Geita, Inspekta Samweli Juma inaonesha kuwapo kwa ongezeko la idadi kubwa ya watoto wanaoshikiliwa mahabusu na magereza ya Wilaya ya Geita mkoani Geita kila mwaka.

Kwa mujibu wa Inspekta Juma, Januari hadi Desemba mwaka jana, walipokea wafungwa watoto 20 jinsi ya kiume na mahabusu watoto 116.

Kati yao, 111 ni wavulana na wasichana watano.

Amefafanua kuwa kwa Januari hadi Oktoba mwaka huu, gereza limepokea wafungwa watoto 29 wote wakiwa ni jinsi ya kiume na mahabusu watoto 192 wamepokelewa, kati yao 190 ni jinsi ya kiume na wawili ni jinsi ya kike.

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la NELICO la mkoani Geita, Paulina Majogoro, mbali ya kueleza kuwa takwimu hizo zinatisha, alitaja sababu za ongezeko la watoto mahabusu ni maadili mabaya yanayochagizwa na tatizo la umaskini, migogoro ya kifamilia, makundi rika, kuacha shule na kwa Geita tatizo likichagizwa na shughuli za migodini.

Kwa hakika takwimu hizo zinatisha na zinasikitisha, na kwa ujumla zinatuma ujumbe kwa jamii kwamba iamke na ichukue hatua za haraka za kukomesha au kudhibiti sababu zinazowafanya watoto hawa wawe mahabusu badala ya kuwa majumbani kwao au shuleni wakipata elimu.

Sisi tunaamini kuwa kama jamii ya Geita na kwa Tanzania kwa ujumla ikiamua, matatizo haya yanayosababisha watoto kuwekwa magerezani yanaweza kupungua kama siyo kwisha kabisa. Ni suala la kurejea katika maadili na kusimamia malezi ya watoto kwa mapana yake badala ya kuwaacha watoto wajiamulie wenyewe maisha yao.

Tunasema hivyo kwa sababu matatizo mengi ya watoto yanaanzia katika ngazi ya familia kabla ya sababu nyingine nyingi zilizotajwa hapo juu. Hivyo familia zinapaswa kuzingatia na kuimarisha malezi ya watoto ili wasijiingize katika vitendo viovu vinavyosababisha kupelekwa magerezani.

Ni ukweli usiofichika kwamba migogoro ya familia imekuwa chanzo kikubwa cha watoto kukosa malezi bora na baadhi yao kujikuta katika kuingia kwenye makundi maovu, hivyo tunaposema familia zichukue jukumu lao la malezi na kusimamia maadili, zitasaidia kuepusha matatizo haya ya watoto kusukumwa magerezani.

Kwa Geita, limetajwa suala la kuwapo kwa shughuli za migodi kwa maana ya watoto hawa kujiingiza katika kufanya kazi wakiwa bado wadogo, ni vyema mamlaka husika zihakikishe hakuna watoto wanaotumikishwa migodini ama kwa kupenda au kwa wale wanaolazimishwa kufanya hivyo.

Hiki kilichojitokeza Geita ni ishara mbaya kwa ustawi wa watoto nchini.

Tuchukue hatua za kukomesha tatizo hili haraka kwa ajili ya kuhakikisha watoto hawa wanarejea katika familia zao na wanakwenda shuleni kupata elimu itakayowawezesha kuwa tegemeo kwa familia zao na taifa kwa ujumla.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/026142d6c1135c472c4621bec67ae30d.JPG

KATI ya kero kubwa iliyosumbua wakazi wa Jiji ...

foto
Mwandishi: MHARIRI

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi