loader
Aveva afungwa, Kaburu huru

Aveva afungwa, Kaburu huru

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu aliyekuwa Rais wa Klabu la Simba Evans Aveva, kifungo cha miezi sita nje kwa sharti la kutokutenda kosa lolote la jinai ndani ya kipindi hicho.

Aveva amepata hukumu hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa tisa ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka. Mahakama hiyo pia imemwachia huru aliyekuwa Makamu wa rais, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake na mahakama hiyo kushindwa kumtia hatiani.

Hukumu hiyo ilisomwa jana mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba baada ya pande zote mbili kukamilisha ushahidi ambapo upande wa mashtaka walipeleka mashahidi 10 na upande wa utetezi washtakiwa walijitetea wenyewe.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29, 2017 na kusomewa mashtaka 10 ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kughushi nyaraka zilizoonesha kuwa klabu hiyo ilikuwa ikilipa mkopo wa dola za Marekani 300,000 kwenye akaunti ya Aveva na utakatishaji haramu wa fedha.

Kesi hiyo iliendelea kutajwa washtakiwa hao wakiwa mahabusu hadi ilipofika Septemba 19, 2019 walipoandika barua ya kukiri na kuomba kumaliza kesi hiyo kwa njia ya majadiliano na Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) lakini upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa walikuwa katika mchakato wa kuwafutia mashtaka ya utakatishaji fedha washtakiwa hao na ikalazimu majadiliano hayo kusubiri, hata hivyo hayakufanyika.

Oktoba 11, 2019 washtakiwa hao walifutiwa mashtaka ya utakatishaji fedha haramu na kupewa dhamana kwa masharti ya kupeleka wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh milioni 30 kila mmoja masharti ambayo waliyatimiza na kuachiwa huku mahakama hiyo ikiwakuta na kesi ya kujibu katika mashtaka manane yaliyobaki.

Katika shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu walidaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka na katika shtaka la pili walidaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha dola za Marekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Katika shtaka la tatu, Aveva walidaiwa kwa pamoja kughushi nyaraka zilizoonesha kuwa Simba ilikuwa inalipa mkopo wa kiasi hicho cha fedha kwa Aveva jambo ambalo walijua si kweli.

Katika shtaka la nne Aveva alidaiwa katika benki ya CRDB alitoa nyaraka za uongo akionesha klabu ya Simba wanalipa mkopo huo.

Aveva alidaiwa kuwa katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia dola za Marekani 187,817 wakati akijua zimetokana na kosa la kughushi nyaraka. Katika shtaka la sita, Kaburu alidaiwa kumsaidia Aveva kujipatia kiasi hicho cha dola 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na kughushi nyaraka.

Pia walidaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba Simba ilinunua nyasi bandia kwa gharama ya dola za Marekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli.

Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola za marekani 40,577 huku shtaka la tisa ilidaiwa washtakiwa hao waliwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola za Marekani 40,577.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/68825c2f8031a598d7d5d4226f32bcd5.jpg

MAKOCHA wa Simba Pablo Franco na wa Yanga, ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi