loader
Tume ya Madini na mapinduzi ya sekta ya madini Tanzania

Tume ya Madini na mapinduzi ya sekta ya madini Tanzania

ILI kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kufanya Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. 

Mabadiliko hayo yaliyofanyika Mwaka 2017 yalisababisha kuanzishwa kwa Tume ya Madini na kuvunja Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na TANSORT.

Katibu Mtendaji wa Tume, Yahya Samamba, anazungumzia kuanzishwa kwa Tume ya Madini akisema ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017.

“Lengo la kuanzishwa tume hii lilikuwa kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa sera na Sheria ya Madini ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali,” anasema.

Kuhusu majukumu ya tume kwa ujumla, Samamba anasema ni pamoja na kutoa na kusimamia leseni za madini, kusimamia shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini pamoja na kusimamia ukaguzi wa migodi na mazingira kwa ujumla.

Mbali na kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Samamba anasema tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini wananchi wengi wameshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya madini nchini.

Kwa mujibu wa katibu mtendaji huyo, imani ya wananchi kwa Rais na Serikali kwa ujumla pia imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Kuhusu ukusanyaji maduhuli kabla na baada ya kuanzishwa kwa Tume, anasema umeongezeka kutoka Sh bilioni 168 katika Mwaka wa Fedha 2014/15 hadi Sh bilioni 584.8 mwaka 2020/2021.

“Katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 kama Tume ya Madini, tulipewa lengo la kukusanya Sh bilioni  526, lakini tukafanikiwa kukusanya Sh bilioni 584, hivyo tukawa tumevuka lengo kwa  kufikia asilimia 112 na katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022 tumepewa lengo la kukusanya Sh bilioni 650 ambalo ninaamini kabisa tutalivuka,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Samamba, mafanikio hayo katika ukusanyaji maduhuli pamoja na mambo mengine yanatokana na uzalendo na ubunifu wa  watumishi wa Tume ya Madini Makao Makuu, ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa, maofisa migodi wakazi na ushirikiano bora kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Madini.

“Waziri wa Madini, Doto Biteko, amekuwa msimamizi wa karibu sana juu ya shughuli zote zinazofanywa na watendaji wa Tume hivyo kuongeza uwajibikaji,” anasema.

Kuhusu masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini, Samamba anasema yalianzishwa kama njia mojawapo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika la madini yao baada ya kuchimba.

Sababu nyingine ya kuanzishwa masoko hayo anasema ni kuisaidia serikali kupata mapato na takwimu sahihi za madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo, pamoja na kuuza madini kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume ya Madini kwa mujibu wa soko la dunia. 

Aidha, vyanzo vingine pia vinabainisha sababu nyingine kuwa ni pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Samamba anasema: “Hadi sasa Tume ya Madini ina masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 59 nchini ambavyo vimeongeza mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye mapato kutoka asilimia tano hadi asilimia thelathini mwaka 2020/2021.” 

Anasisitiza kuwa masoko ya madini yamepunguza kwa kiasi kikubwa kiwango na kasi ya utoroshaji wa madini nchini na kuleta ushindani kwa wafanyabiashara wa madini kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini.

Akielezea mikakati zaidi ya serikali kudhibiti utoroshaji wa madini na kuhakikisha thamani ya madini ya tanzanite inazidi kuimarika, katibu mtendaji huyo wa Tume ya Madini anasema mwaka 2018 serikali iliamua kujenga ukuta wa Mirerani wilayani Simanjiro katika Mkoa wa Manyara ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa wachimbaji na serikali kwa ujumla. 

“Kumekuwa na mafanikio makubwa sana kwenye uzalishaji wa madini ya tanzanite. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2016 uzalishaji wa madini ya tanzanite katika eneo la Mirerani ulikuwa kilo 161, lakini baada ya ujenzi wa ukuta wa Mirerani uzalishaji umeendelea kuongezeka hadi kufikia kilo 2,172 katika kipindi cha mwaka  2020,” anasema.

Anasema mikakati mingine iliyowekwa na serikali ni pamoja kuwahamisha wafanyabiashara wa madini kutoka Arusha hadi Mirerani ili kuinua uchumi wa eneo la Mirerani na kudhibiti utoroshaji wa madini.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa mfumo maalumu wa kudhibiti mnyororo mzima wa madini ya tanzanite kuanzia kwenye uchimbaji, biashara, uongezaji thamani hadi usafirishaji wake kuhakikisha thamani ya madini hayo inazidi kuongezeka duniani. 

Kuhusu namna serikali inavyosimamia ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, anasema kwa kutambua umuhimu wake, mwaka 2018 serikali iliweka kanuni na miongozo mbalimbali ya kuhakikisha Watanzania wanashiriki katika shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini kupitia utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini kama vile usafiri, bidhaa za kilimo, ulinzi, bima, sheria, benki na nyingine.

Imebainika kuwa hadi sasa asilimia 63 ya bidhaa na huduma zinatolewa na wananchi wa Tanzania kwenye kampuni kubwa za uchimbaji wa madini huku asilimia 37 zikitolewa na kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalumu kinachotolewa na Tume ya Madini.

Kuhusu ajira katika migodi ya madini, imebainika kuwa asilimia 96 ni Watanzania huku raia wa kigeni wakiwa ni asilimia nne.

“Ieleweke kuwa hakuna kampuni yoyote inayoruhusiwa kuagiza bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi bila kupata kibali kutoka Tume ya Madini; lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na sekta ya madini,” anasema.

Uchunguzi wa HabariLEO umebaini kuwa, Tume ya Madini pia imekuwa makini kuhakikisha kampuni za uchimbaji wa madini zinarejesha sehemu ya mapato kwa jamii kupitia michango ya huduma mbalimbali kwa jamii (CSR) inayozunguka machimbo yake kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.

Samamba anadokeza kuwa, katika sekta ya madini suala la usalama kwenye  migodi haliachwi nyuma na kwa kutambua hilo, Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira imekuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara katika migodi ya madini.

Aidha, imekuwa ikitoa elimu. Katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2020/2021 migodi 89 ya uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa ilikaguliwa.

Mafanikio mengine kwa mujibu wa Katibu Mtendaji Samamba ni pamoja na ongezeko la utoaji wa leseni za madini kutoka leseni 5,094 katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 hadi leseni 7,968 mwaka 2020/2021. 

 “Katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2021, mchango wa sekta ya madini umefikia asilimia 7.7. Hii inaonesha ni namna gani sekta inaendelea kukua kwa kasi,” anasema.

Samamba anazidi kufafanua akisema hadi sasa kampuni nyingi za uchimbaji mkubwa wa madini zimeonesha nia ya kuwekeza Tanzania na sasa zipo katika taratibu za maombi ya leseni.

Anasema kampuni hizo zikipewa leseni za madini na kuanza kuchimba madini, mapato yataongezeka kwa kasi na kuifanya sekta ya madini nchini kufikia asilimia 10 ya mchango wake katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025. 

Samamba anadokeza kuwa migodi mikubwa mitatu inatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni hapa nchini.

Anaitaja kuwa ni Mgodi wa Kabanga utakaokuwa unachimba madini aina ya ‘nickel’ Mgodi wa Nyanzaga utakaokuwa unachimba dhahabu na mgodi wa Ngwala utakaokuwa unachimba madini aina ya ‘Rear Earth Element (REE)’. 

Anasema: “Migodi hii itakapoanza kazi, mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa utaongezeka na kuimarika zaidi.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/af1161db3e10763b979b430ef1558a8f.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi