loader
LSF na Mpango wa Uwezeshaji Wanawake kutambua haki kiuchumi

LSF na Mpango wa Uwezeshaji Wanawake kutambua haki kiuchumi

MWAKA 2018 Legal Services Facility (LSF), ilizindua mpango wake wa uwezeshaji wa wanawake waishio mijini ili wapate uelewa wa kisheria kuhusu masuala ya haki za mazingira, uchumi, makazi na kazi kwani ni mojawapo ya haki ambazo hukiukwa sana katika maeneo ya mijini nchini. 

Ili kuwezesha utekelezaji wa mpango huu, LSF ilishirikiana na mashirika yanayofanya shughuli zake mijini na kutoa ufadhili uliowezesha mashirika hayo kuchangia katika maeneo muhimu na kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa na LSF.

LSF ilishirikiana na Taasisi ya Chama Cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) ili kuhakikisha kila mwananchi mkazi wa Dar es Salaam anafurahia haki yake ya msingi ya kuishi katika mazingira safi na yenye afya bora kupitia mradi uliotekelezwa katika wilaya tano za jiji hilo. 

Akizungumzia ufadhili huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala anasema chini ya ufadhili wa mradi huu mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kutunga sheria ndogondogo zinazowezesha jamii kuweka vituo vya kuzolea taka mitaani, kuweka sheria kali dhidi ya uvujishaji wa maji taka na kuwatoza faini watu wanaokiuka sheria hizo ndogo. Mpango huu umeboresha kwa kiasi kikubwa usafi wa jumla wa mazingira katika maeneo mengi ya jiji na kuondoa milipuko ya magonjwa.

Kuhusu masuala ya makazi miongoni mwa jamii maskini za mijini, anasema LSF ilishirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kwa ujumla ili kuwasaidia kuelewa haki yao na kuhakikisha wanaingia mikataba ya kupangisha ili kuwazuia wamiliki wa nyumba wasikiuke haki za wapangaji.

Aidha, programu maalum inayolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi imezinduliwa na inaendelea kufanyiwa kutekelezwa katika Manispaa ya Ubungo. 

Anasema mpango huo utashuhudia zaidi ya wanawake 300 wakisaidiwa kupata hati miliki zao, na zaidi ya 2,000 wakiwezeshwa katika masuala ya kisheria yanayohusu masuala ya ardhi ambayo ni muhimu katika kushughulikia migogoro ya ardhi inayoshamiri katika maeneo mengi ya nchi.

Kwa msaada wa LSF, Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC) kinatekeleza mradi wa uwezeshaji jamii katika haki za ajira ambao walengwa wake ni wanawake na vijana wanaofanya kazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi. 

Mratibu wa mradi huo, Abia Richard anasema chini ya mradi huu jumla ya watu 1,192 wamepata msaada wa kisheria kupitia uhamasishaji, mafunzo, maigizo na usambazaji wa jumbe mbalimbali za uhamasishaji. 

“Zaidi ya hayo, wafanyakazi wanapata uelewa kuhusu uvunjaji wa mikataba ya ajira, ukiukwaji wa haki za uzazi, na unyanyasaji wa kijinsia mahali pa kazi,” anasema.

Mradi wa “Wanawake na Ajira” unaotekelezwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) unaoshughulikia changamoto za haki za ajira zinazowakabili wanawake, vijana na wasichana walioajiriwa katika sekta ya viwanda jijini Dar es Salaam. 

Afisa Mradi huo, Renatha Andreas anasema chini ya mradi huu viwanda kadhaa vimeweka utaratibu wa kuzuia aina zote za ukatili na ubaguzi mahali pa kazi, kama inavyothibitishwa zaidi na maombi ya wafanyabiashara 12 wa viwanda jijini Dar es Salaam wanaotaka kuandaliwa sera za kupinga unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi. 

Mafanikio mengine ya mradi huo ni mpango wa mwaka mmoja ambao uliandaliwa na WCPC - Ubungo ili kukabiliana kikamilifu na ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake mahali pa kazi.

Mkoani Mwanza - LSF imeunga mkono shirika la Railway Children Africa ambalo linatekeleza mpango ulioandaliwa kwa ajili ya kuboresha na kubadilisha maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Lengo ni kuwaongezea uelewa ili kukbailiana na changamoto zinazowasukuma na kuwaweka watoto katika mazingira yasiyo salama kwa kutumikishwa kufanyiwa unyanyasaji mwingine katika mazingira hayo ya mijini katika wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Kupitia usaidizi wa kisheria na mafunzo juu ya haki za watoto wa mitaani na wafanyakazi wa nyumbani, taratibu za usaidizi wa haki zimetolewa ikiwamo haki ya malezi ya wazazi au ya ulezi kwa watoto wa mitaani pia zimetolewa kwa kujumuisha.

Nambari maalum ya simu kwa wafanyakazi wa nyumbani imetolewa ili kuripoti matukio yoyote ya ukatili wanayotendewa na watu wengi wanaitumia kuripoti matukio hayo na kupata msaada.

Mjini Dodoma kulianzishwa mradi wenye lengo la kuboresha na kuwezesha haki za kuishi katika mazingira safi na salama kwa wakazi wa kipato cha chini waishio halmashauri ya jiji la Dodoma.

Mradi huo umetekelezwa na Shirika la Reaching Unreached Tanzania (RUT) ulianza mwaka jana kwa ufadhili wa LSF. 

Afisa mradi kutoka RUT, Getrude Kigala anasema halmashauri ya jiji hilo imepewa mafunzo ya namna ya kutumia sheria za taka ngumu na kusaidiwa kuitekeleza. Hatua hiyo inakuza haki za wakazi wa jiji kuishi katika mazingira safi na yenye afya.

Kwa upande mwingine jijini Mbeya, LSF inashirikiana na Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) kuwajengea uelewa na kuwapa ujuzi wa kutosha wanawake wa mijini ili kumudu masharti ya mikopo katika kata 36 za jiji la Mbeya. 

Mmoja wa maofisa wa LSF waliotoa elimu hiyo mkoani Mbeya, Aggripa Senka anasema hadi sasa mradi huo umetoa umewafikia watu 11,000 na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake kama vile kutambua na kukataa muda usiofaa wa mkataba wanapopata mkopo kwa shughuli zao za kiuchumi au kijamii.

Kwa upande wa Zanzibar, LSF inaunga mkono Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Zanzibar (ZAPAO) kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo hususani wanawake na vijana katika mkoa wa Mjini Magharibi ili kuboresha mazingira yao ya kibiashara. 

Kupitia ZAPAO wafanyabiashara hawa wamefaidika katika nyanja mbalimbali ikiwamo kupata maeneo yaliyotengwa na serikali ambapo wanafanya biashara zao bila vikwazo.

Kwa ujumla, mpango wa LSF kuhusu uwezeshaji wa kisheria katika maeneo ya mijini, kwa kiasi kikubwa umeshughulikia changamoto katika mazingira ya mijini hivyo kuongeza fursa za kuendelea kufanya kazi na serikali za mitaa na washirika wengine katika masuala ya kila siku mijini na kuwasaidia wanawake na vijana kutambua haki zao.

Tunaposherehekea kumbukumbu ya miaka 10 tunaona haja ya kuendelea kusaidia na kupanua program hii katika mikoa mingi zaidi.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/88d73d5a40cab9d7a8a90d9ced21b88a.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi