loader
Kahawa inavyoweza kunufaisha wazalishaji mkoani Kagera

Kahawa inavyoweza kunufaisha wazalishaji mkoani Kagera

“TUNAFANYA kosa kubwa la kupenda kutumia tusichozalisha na tunachokizalisha hatupendi kabisa hata kukigusa; kasumba hii ni mbaya na inaumiza sana… Tazama Mkoa wa Kagera unazalisha kahawa nyingi na bora, lakini kwa nini hatutumii kahawa tunayoizalisha!”

Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora anasema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Kunywa Kahawa  Duniani mwaka huu.

Maadhimisho hayo hufanyika kila Oktoba Mosi kwa wadau wa kahawa kuungana na kutoa elimu na faida za kunywa kahawa.

Katika Mkoa wa Kagera, maadhimisho haya yalifanyika Oktoba 15, mwaka huu kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa kahawa na kujadili changamoto zinazoikumba sekta ya kahawa.

Katika maadhimisho hayo ya kimkoa, anasema: “Nani anatuzuia tusitumie kahawa yetu? Kwa nini hatunywi kahawa tunayoizalisha? Hebu kila mmoja wetu ajihoji na kupata majibu.”

Profesa Kamuzora anasema katika muda aliokulia mkoani Kagera amebaini kuwa, ni watu wachache wanaokunywa kahawa wanayoizalisha na badala yake wengi wanauza kahawa yote katika vyama vya msingi kama ulivyo utamaduni wa kila msimu mkoani Kagera kwamba kahawa hukusanywa katika vyama vya msingi.

Uchunguzi wa HabariLEO kupitia vyanzo mbalimbali vya habari umebaini kuwa, matumizi duni ya bidhaa au huduma unazozalisha kwa namna moja ama nyingine hupunguza thamani ya bidhaa yako kwa kuwa wewe mwenyewe huonekana kutojali au kutoukubali ubora na umuhimu wa bidhaa unayozalisha.

Mwananchi mmoja mjini Bukoba aliyekataa jina lake kutajwa anasema: “Wewe mwenyewe kama unapika halafu unakataa chakula ulichopika, ina maana hukiamini ubora wake na unawafanya wengine nao wakufuate na hiyo inafanya bidhaa yako inakuwa nyingi sokoni.”

Anaongeza: “Kwa kanuni za kibiashara na kiuchumi, bidhaa inapokuwa nyingi sokoni hata kuzidi mahitaji, bei hupungua na kufanya bidhaa hiyo iuzwe bei ya kutupwa, lakini wewe mwenyewe unapoitumia, unawavutia na kuwatamanisha wengine na hivyo kuchochea thamani ya kitu unachozalisha…”

Kamuzora anasema bahati nzuri kahawa inayonyweka sehemu mbalimbali duniani kutokaa nchi za Afrika inasifika kwa ubora hivyo ni vema wazalishaji nao wakaongeza juhudi kuthibitisha ukweli huu kwa wao wenyewe, kuikubali, kuipenda na kuitumia kama mfano bora badala ya kuuza yote.

“Nikiwa nje ya nchi na kufuatilia matumizi ya unywaji wa kahawa nilijikuta naipenda sana na ninaitumia; ukawa utamaduni wangu wa kunywa kahawa na kila siku nikiamka natumia,” anasema Profesa Kamuzora na kuongeza kuwa, alipoteuliwa kuwa RAS wa Kagera, alitembelea migahawa mbalimbali lakini hakuona sehemu ambayo watu wanakutana maalumu kwa kunywa kahawa.

Inaelezwa kuwa, kutokana na hali hiyo mwaka 2019 alishawishi kampuni mbalimbali ikiwamo TANICA, AMIMUZA na HAKIKA zinazojihusisha na kuuza kahawa ya unga nje ya nchi kufungua migahawa wa kuwakutanisha wadau kunywa kahawa nazo zikaitikia na kuahidi kufungua migahawa mingine katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam.

Anasema hakuishia hapo, bali alitembelea wadau wengine pia wanaojihusisha na masuala ya kahawa ili kuwashawishi kufungua migahawa ili kufanya manufaa ya kinywaji hicho yazidi kufahamika zaidi kwa umma.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa kihabari wa HabariLEO, ushawishi alioufanya Kamuzora unaelekea kuzaa matunda kwani sasa mkoani Kagera kuna migahawa kadhaa inayowakutanisha watu kunywa kahawa na hata katika mikoa mbalimbali nchini.

Mwenyewe anafafanua akisema: “Lengo kubwa hapa ni kupata soko la ndani maana kama watu wataweza kunywa kahawa yao kwa kiasi cha kutosha, hakutakuwa na haja ya watu kulilia bei ya kahawa kwani nje wasiponunua, wenyeji wataitumia kama sehemu ya faida ya zao hilo.”

Anahimiza wadau wa elimu kuhusu kilimo cha kahawa kuwahimiza vijana kupenda kilimo cha kahawa na kuiongezea thamani kama njia ya kupata ajira kwa kutengeneza ladha ya kahawa katika vyakula jambo ambalo limeanza kuonekana.

Aliwashauri maofisa katika halmashauri mbalimbali kuwa na utamaduni wa kuwakaribisha wageni kwa kahawa wanapotembelea ofisi zao ili kuitambulisha kahawa ya Mkoa wa Kagera kwa watu wa maeneo mbalimbali.

Meneja wa Bodi ya Kahawa katika Kanda ya Kagera, Melkiad Massawe, anatumia maadhimisho hayo kuwaambia wananachi faida za kunywa kahawa, faida za kutumia pembejeo katika kilimo cha zao hilo, kuhakikisha kahawa inaanikwa katika ubora pamoja na vijana kushiriki katika kilimo cha kahawa ili kujipatia fedha.

Anataja faida za kunywa kahawa kuwa ni pamoja na kutibu na kukabiliana na presha ya kupanda na kushuka, kupambana na kisukari na magonjwa ya akili, kuzuia kupatwa na ugonjwa wa kibofu nyongo, kupambana na ugonjwa wa kusahau hasa kwa wazee.

Faida nyingine za kahawa kwa mujibu wa Massawe ni pamoja na kupambana na ugonjwa wa figo, kuongeza uwezo wa ufahamu na akili, kuzuia ugonjwa wa uvimbe wa mikono na miguu, kuratibu homoni pamoja na kuongeza kipato kwa familia na taifa kwa jumla.

Anasema kwa msimu wa Mwaka 2021/2022 kilogramu moja ya kahawa imenunuliwa kwa Sh 1,600 kutoka Sh 1,200 kwa mwaka 2020/2021 na kwamba, matumizi ya ndani kahawa yakiongezeka, mkulima anaweza kupata kipato kikubwa zaidi kutokana na zao hilo.

“Kwa sasa watumiaji wa kahawa Tanzania ni asilimia 5 hadi 7. Mkakati uliopo ni kuhakikisha walau tunafikia asilimia 30 baada ya miaka ijayo hivyo tunaendelea na hamasa ya ufunguzi wa migahawa katika maeneo mbalimbali ya nchi.”

“Kupitia jambo hili, matumizi ya kahawa yatakuwa makubwa na mkulima atapata kipato zaidi kama ilivyo kwa nchi nyingine…”

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge, anasema ameanza kujifunza masuala ya kahawa ingawa ana kipindi kifupi tangu afike mkoani Kagera.

Anasema anatamani kuona vijana wanashiriki kwa namna moja ama nyingine katika masuala ya kahawa ama iwe kwa kulima, kuongeza thamani au kujiajiri.

Anasema kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kunywa Kahawa Duniani mwaka 2021 inayosema: “Wezesha Ushiriki wa Vijana na Wanawake Katika Sekta Endelevu ya Kahawa” inasisitiza kuwa, ni zamu ya vijana na wanawake kushiriki moja kwa moja katika masuala ya kilimo cha kahawa.

Pamoja na kukagua shughuli zinazofanywa na vyama vya ushirika na kampuni zinazouza kahawa ndani na nje ya nchi, alitoa Sh 800,000 kwa ajili ya ununuzi wa mashine mbili za kukoboa kahawa za wakulima pamoja na kutoa zawadi ya vipima unyevu kwa vyama vitano vilivyofanya vizuri katika msimu wa mavuno wa 2021/2022.

Vyama vilivyopata zawadi ni Juhudi Amcos, Mkombozi Amcos, Buguruka Amcos, Rubibi Amcos na Tukutuku Amcos.

Ilielezwa kuwa, vipima unyevu hivyo vitasaidia kuhakikisha kahawa inakuwa bora na inaendelea kupanda thamani.

Mbuge alisema kila mwaka Bodi ya Kahawa itakuwa inaweka vigezo na atakayeshinda atakuwa anapata zawadi.

Mratibu wa shirika la Cafe Afrika linaloshughulikia utoaji huduma za ugani na elimu kwa wakulima wa kahawa mkoani Kagera, Daniel Mwakalinga, anasema ili kuunga mkono juhudi za RAS wa Kagera kuhusu kilimo cha kahawa na ushiriki wa vijana, shirika limetoa mafunzo kwa vijana 147 kushiriki kilimo cha kahawa.

Vijana waliopata mafunzo wanaotokea katika halmashauri 8 za Mkoa wa Kagera, wanatumika kujenga ushawishi kwa vijana wengine kujifunza kilimo cha kahawa na kufungua migahawa ya kunywa kahawa katika maeneo ya vijiji vyao.

“Vijana wetu ni wa kiume wa kike wanapewa mbinu na mitaji ya kuhakikisha kilimo katika Mkoa wa Kagera kinainuka na si vinginevyo, lengo letu ni wakulima wote tukiwalenga zaidi vijana ili wawe chachu kwa jamii na kuhakikisha azma ya Mkoa wa Kagera na Watanzania kunywa kahawa wanayoizalisha inatimia,” anasema Mwakalinga.

Kwa kipindi cha miaka miwili tangu elimu ianze kutolewa vijana 147 wameshiriki kufufua mashamba 137 ya kahawa, kufanya ushawishi kwa vijana wengine walioanza kujihusisha na kilimo cha kahawa na kuanza kufungua migahawa ya kunywa kahawa vijijini.

Vijana wengine wamemudu kutumia kahawa katika vyakula na vitafunio mbalimbali kama keki katika sherehe ikiwa ni sehemu ya manufaa  yatokanayo na zao la kahawa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ed7bd12e400baf9b8b82ae6d87f79a79.png

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi