loader
Zanzibar ilivyotulia chini ya Dk Mwinyi

Zanzibar ilivyotulia chini ya Dk Mwinyi

NOVEMBA 2, mwaka huu umetimia mwaka mmoja tangu kuapishwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Nane, Dk Hussein Mwinyi. Sherehe za kuapa kuongoza Zanzibar kwa uaminifu zilifanyika katika Uwanja wa Amaan, mjini Unguja

. “Mimi Hussein Ali Mwinyi, naapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu kwamba, nitakuwa mwaminifu kwa Zanzibar na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda, nitaitii na kuitetea Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake kwa mujibu wa sheria iliyowekwa…,” ndivyo alivyoapa kiongozi huyo.

Wakati akiapa, Dk Mwinyi ambaye ni mpole, mwenye maneno machache lakini mkali kwa wazembe na wasiofuata maelekezo, alieleza namna serikali yake itakavyokuwa, hasa katika kuleta umoja wa kitaifa, kuondoa ubaguzi, rushwa, kurejesha utulivu wa kisiasa na kukomesha vitendo vya udhalilishaji hususani kwa watoto na wanawake.

Hotuba yake ya kwanza, ikazisuuza na kuzikonga nyoyo za Wazanzibari kwani jambo kubwa ambalo anapotimiza mwaka mmoja madarakani anakumbukwa nalo, ni kukaribisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Siasa za Zanzibar hazikuwa zinatabirika, vyama vilikinzana kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF), chini ya kiongozi wao visiwani humo, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu). Siasa hizo zilitikisa na kuleta ushindani mkubwa kati ya vyama hivyo viwili vilivyokuwa na nguvu kubwa na wafuasi wengi miaka mingi kabla ya migogoro ndani ya CUF kuibuka na kukigawa chama.

Hata hivyo, baada ya migogoro hiyo ya CUF, Maalim Seif alihamia Chama cha ACT-Wazalendo na kuendeleza harakati visiwani humo huku wafuasi wengi wa chama hicho wakimfuata. Umaarufu wa Maalim Seif na siasa za Zanzibar uliendelea na kumpa umaarufu ndani ya chama hicho kipya hadi kufikia hatua ya kumpitisha kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Haikuwa bahati kwake kwani uchaguzi huo ndio uliompa ushindi Dk Mwinyi ambaye baada ya kuapishwa, aliona ni busara kumaliza tofauti na mvutano wa kisiasa visiwani humo na kukaribisha SUK. Kitendo cha kukaribisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ni ishara nzuri kwa Rais Dk Mwinyi aliyeangalia mustakabali wa wananchi wake na kufanya uamuzi wa busara kumaliza tatizo lililokuwapo.

Kupitia SUK, Rais Mwinyi alimteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais ikiwa ni muda mfupi umepita tangu Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo iazimie kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa visiwani humo. Hatua hiyo ilimmwagia sifa kiongozi huyo aliyeanza kuonesha kwa vitendo kile alichokiapa kurejesha utulivu wa kisiasa visiwani humo jambo ambalo lilikuwa pasua kichwa kwa miaka mingi.

Januari mwaka huu, Dk Mwinyi alikutana na kuzungumza na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Ikulu Zanzibar, Joseph Butiku na kumwambia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kumeimarisha amani, umoja na mshikamano Zanzibar hatua inayochochea kasi ya maendeleo

Serikali hiyo si tu kwamba imeleta mshikamano Zanzibar, bali pia imerejesha maelewano na ushirikiano mkubwa kati ya viongozi na wananchi wengi wa Zanzibar, hivyo kuimarisha umoja, amani na mshikamano tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Ndani ya mwaka wa utawala wa Rais Dk Mwinyi, hali ya siasa Zanzibar imekuwa shwari.

Ikumbukwe kuwa, Dk Mwinyi aliingia madarakani na mbinu ya kusikiliza changamoto za sekta mbalimbali na kuzitafutia utatuzi. Kubwa analosimamia kiongozi huyo ni kauli yake ya kutokuwa na muhali kwa wazembe.

KAISAFISHA SMZ

Zanzibar ya leo si ya jana, ndani ya mwaka mmoja wa utawala wa Dk Mwinyi, ameamua kusafisha ofisi mbalimbali za serikali visiwani humo na kuibua ‘madudu’ kwa kuyaweka hadharani, akilenga si tu kuyaanika, bali kuyakemea na kuyatafutia ‘mwarobaini’ huku akiwaonya wazembe na wala rushwa.

Kasi aliyoanza nayo, ilifanana na kasi ile ya Rais John Magufuli, amefanya ziara kadhaa za kushtukiza huku akiengua na kuteua sura mpya za viongozi kwenye maeneo tofauti na kubwa linaloonekana, ni imani yake kwa vijana huku akiwapa fursa sawa Wazanzibari.

Watanzania wameshuhudia fursa za uongozi zikitolewa kwa watu wa Pemba na Unguja bila kujali itikadi zao na kubwa zaidi amezingatia elimu, uwezo na kipaji cha mtu kwa kuweka kando itikadi za kisiasa na ukabila.

Mwenyekiti wa Chama cha Siasa cha Ada-Tadea, Juma Ali Khatib, anasema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, kubwa zaidi alilolifanya Dk Mwinyi ni kuwaunganisha Wazanzibari na kuondoa chuki na uhasama miongoni mwao.

Khatib anasema uwepo wa amani ya kudumu umefungua fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kutafuta maisha kwa amani na utulivu, hatua ambayo pia imewavutia wawekezaji kwenda Zanzibar kuwekeza katika miradi mbalimbali.

“Maridhiano ya kisiasa yamefungua milango ya amani na utulivu wa kisiasa, kitendo ambacho kimemnyanyua juu kisiasa Rais Mwinyi na kuwa kipenzi cha Wazanzibari wote kwa kuwaunganisha na ndio maana tunaona hata wawekezaji wamejitokeza kwa kasi kuwekeza Zanzibar,” anabainisha Khatib.

Kwa mwaka huu mmoja wa utawala wake kuna mwanga mbele ya Zanzibar, amani imetawala, utulivu unashuhudiwa hususani wa kisiasa na hiyo ni dalili njema kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Sasa wananchi wa Zanzibar wanapaswa kuunganisha nguvu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi ili yale marashi ya karafuu yanukie pote visiwani humo na kuleta maendeleo zaidi chini ya uongozi wa Rais Dk Mwinyi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/691be25b677935dfbffb1a9823fc7fa7.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi