loader
Tafiti za kilimo zaipa mwelekeo   Serikali kukabili tabianchi

Tafiti za kilimo zaipa mwelekeo  Serikali kukabili tabianchi

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo amesema serikali inachukua kila hatua kuhakikisha kwamba inawakinga Watanzania na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwepo kwa usalama wa chakula.

Aliiambia HabariLEO kwamba juhudi hizo za kukabili mabadiliko ya tabianchi zinazofanywa zinashirikisha pia wadau mbalimbali wa kilimo.

Alisema kwamba, Wizara ya Kilimo imefanya tafiti za kutosha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kuweka mikakati ya kukabiliana nayo hasa kwa kuhakikisha uwapo wa chakula cha kutosha, nafuu na chenye lishe. 

Aidha, alisema pamoja na kuangalia upatikanaji wa chakula pia serikali imejipanga kuinua kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua ambazo hazina uhakika wa kuanza na kuisha na mtawanyiko wake.

Katika mahojiano hayo yaliyogusa mkutano unaoendelea wa Umoja wa Mataifa wa tabianchi (COP26) mjini Glasgow, Scotland, alisema ni dhahiri kinachozungumzwa kuhusu tabianchi kina athari kubwa kwa dunia, Tanzania lazima ijizatiti kuhakikisha kwamba athari zake zinazuiwa.

Imeelezwa katika mkutano huo ulioanza Novemba 1 na kutarajiwa kumalizika Novemba 12 kwamba, janga la kwanza linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ni upungufu mkubwa wa chakula duniani.

Katika mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan alielezea utayari wa Tanzania katika kutekeleza mikakati ambayo inakabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutaka mataifa yaliyoendelea kutekeleza ahadi zao na kuwasilisha fedha zilizolenga kusaidia mikakati hiyo kwa wakati.

 Katika mkutano huo Rais wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA), Dk Agnes Kalibata alitaka jamii kusaidia kilimo kinachofanywa na wakulima wadogo wa Afrika ikiwamo Tanzania.

Alisema kwa kuwepo na mifumo endelevu ya chakula kutawezesha wakulima wadogo kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kuhusu kauli hiyo, Profesa Tumbo alisema Tanzania imeshaanza kutekeleza hatua muhimu za kusaidia wakulima wadogo na kutaka wadau kuchangia hasa kwenye  kuboresha mifumo ya kilimo na kilimo cha kisasa.

Aidha, alisema serikali imeona haja ya kuwa na maghala ya kuwekea chakula na pia kuendeshea mifumo ya amana kusaidia wakulima wanaposubiri bei nzuri ya mazao yao.

Pia alizungumzia umuhimu wa taarifa sahihi za utabiri wa hali ya hewa kuwafikia wakulima na kuwapo kwa utabiri sahihi wa hewa.

“Ili kufikia malengo hayo, wakulima wadogo ni lazima wabadilike na kuendesha kilimo cha kisasa ikiwa na matumizi sahihi ya tabiri za hali ya hewa  na kuwa na mfumo sahihi wa baada ya mavuno,” alisema Prof Tumbo.

Naye mwakilishi mkazi wa AGRA nchini Tanzania, Vianey Rweyendela, akizungumzia mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi alisema mifumo endelevu ya chakula ni jibu kwa maendeleo yenye uhakika.

Alisema ipo haja kwa wadau wote kushirikiana kuhakikisha kwamba kunakuwa na miradi inayowezesha usalama wa chakula kama taasisi yake inavyofanyakazi nchini Tanzania.

AGRA imesaidia katika miradi kadhaa nchini kuwezesha uwapo wa mifumo sahihi ya uhifadhi wa chakula baada ya mavuno na pia kupigania elimu kwa wakulima wadogo ili kuongeza tija.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2bfdb922b7115c967f49a51146ad9c3e.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi