loader
Nilivyorubuniwa kufanyakazi kwenye danguro China

Nilivyorubuniwa kufanyakazi kwenye danguro China

Awali niliambiwa nitafanya kwenye hoteli

 

Roziline Joseph (siyo jina lake halisi) (25) anasema hatausahu mwaka 2014 kwani alipitia  changamoto na misukosuko mingi akiwa nchini China ambako wakala alimpeleka akidai  atakwenda  kufanya kazi za hotelini, lakini akajikuta akifanya kazi tofuati kabisa.

Binti huyu anasema kuwa baada ya kumaliza kidato cha nne akiwa na miaka 18 akijijishughulisha na biashara zake za kununua vitu vya urembo Kariakoo na kuuza mitaani aliona amepata ngekewa. Kwani  alifuatwa na dada mmoja ambaye alidai anataka kumsaidia kupata kazi ya hoteli yenye malipo mazuri nje ya nchi.

Hivyo, alipokubali akalipiwa kila kitu hadi kutafutiwa hati ya kusafiria kisha akampa namba ya mwenyeji wake atakaye mpokea kule China ili ampeleke kwenye hoteli husika na kuanza kazi.

Anasema alipofika nchini China alijikuta akiangukia kwenye danguro maarufu linalojulikana kama Chambuchambu ambako wanawake wa mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwemo Tanzania wanatumikishwa kingono.

Alipofika China na kupokelewa na mwenyeji wake kisha kufikishwa hotelini alikuwa bado ana fikra kuwa mamba ni mazuri. Lakini kilichomshangaza ni mara baada ya kufika usiku wake akapelekwa kwenda Chambuchambau kuanza kazi ya kuuza ngono asijue la kufanya. Kwani mwenyeji wake alipomfikisha hapo akamwacha na akaondoka zake.

 “Nilimpigia simu mwenyeji wangu kujua kinachoendelea, alinijibu, ‘acha uzembe, tafuta hela uniletee,” anasema alihisi uchungu mkali na kuangua kilio.

“Nikiwa nalia alitokea mwanaume wa Kighana alinihoji nikamueleza tatizo langu, akaahidi kunirudisha kwenye hoteli niliyofikia lakini alitaka nitimize kwanza takwa lake la kumridhisha kingono,” Rozeline anasimulia.

Licha ya Mghana kumlipa Dola 100 za Marekani baada ya kutimiza haja yake, mwenyeji wake alipofahamu alimnyang’anya fedha zote na kumwamuru arudi Chambuchambu kuendelee na kazi ili alipe deni.

“Nilitakiwa kila siku kumpa mwenyeji wangu Dola 200.”. Fedha hizo kiasi alikuwa akichukue yeye na nyingine analipwa mwenye hoteli aliyokuwa anaishi. Hivyo ilikuwa ni kufanya kazi usiku na mchana hakuna kupumzika,” anasema.

Anasema mwenyeji wake aliyempokea ambaye alikuwa ni Mtanzania pia, alikuwa akimweleza kuwa ni lazima alipe deni la ndege iliyompeleka China pia gharama za hoteli anayokaa na gharama nyingine. Hivyo ilikuwa vigumu kumaliza deni hilo.

AFANYIWA UKATILI WA KUTISHA

Kuna siku anasimulia Roziline, kuwa aliamua kwenda klabu, huko alikutana na mwanaume wa Kinigeria aliyeonekana mtanashati. “Tukakubaliana kiasi cha pesa nilichohitaji ili tustarehe, alikubali na kunipeleka nyumbani kwake, ilikuwa ni nyumba kubwa na nzuri, na alisema anaishi peke yake.”

 Anasema walipofika nyumbani alikaribishwa vizuri. Lakini wakiwa wanaendelea na starehe zao mara akashangaa mwanaume mwingine anaingia na yeye akitaka astareheshwe. Licha ya kugoma, walimkamata na kumwingilia  kimwili kwa nguvu.  Mara wawili wengine waliingia nao wakitaka hitaji hilo hilo.

“Nikajikuta nalala na wanaume wanne kwa wakati mmoja usiku ule,” anasimulia Rozeline kwa uchungu huku akiwa amejiinamia.

Kwa kuwa binti huyo alikuwa akigoma wakati wanaume hao wanne wakitaka kujistarehesha naye, walikuwa wakimpiga na kuendelea kujistarehesha kwa zamu usiku mzima.

“Niliumia sana,  kwani nilitumikishwa kingono usiku kucha na kesho yake mchana kutwa, ilipofika siku kama saa mbili walininyang’anya fedha nilizokua nazo na kuniamuru kuondoka.

Akiwa analia asijue atafikaje anapoishi, ndipo mmoja kati ya wale Wanageria akamrushia Yuan 100 atumie kama nauli. Akiwa njiani alikutana na Rafiki yake akamwona jinsi alivyokuwa akichechemea kwa maumivu kisha akampeleka hospitali.Vipimo vya ultra- sound na x-ray, vilionyesha jinsi alivyoharibiwa sehemu za uzazi.

"Nikachomwa sindano za mishipa na kutundikiwa dripu, nilichomwa pia sindano za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,” anasema. Hata hivyo akiwa hospitali alimpigia simu mwenyeji wake juu ya yaliyomsibu, alikata simu hakutaka kujua zaidi. Lakini aliporudi alianza kumdai dola zake 200 kwa siku.

Baada ya muda alijikuta mjamzito wala asijue baba wa mtoto. Akapanga kuitoa mimba. Alipewa dawa kwa masharti ya kutojihusisha na ngono kwa muda wote atakaotumia vidoge. Sharti lililomshinda kwasababau alikuwa anahitaji fedha na kujikuta mimba hiyo haikutoka. Ingawa mwishowe alifanikiwa.

Biashara ya kuuza mwili  huku afya yake ikiendelea kudhoofika anasema ilimchosha baada ya kufanya kama miezi mitano hivi na kuona haja ya kutafuta mbinu ya kutoroka. Rafiki yake, raia wa Urusi alimsaida. Alimtorosha hadi Hong Kong kisha Tanzania.

“Hata hivyo, nikiwa njiani nilikutana na kikwazo baada ya picha katika hati yangu ya  kusafiria  kuonekana haifanani na muonekano halisi niliokuwa nao kwa wakati ule wakati naandaa hati yangu ya kusafiria  maana  wakati natoroka , nilikuwa nimedhohofu sana.”

 “Waliniingiza kwenye chumba maalumu na kuanza kunikagua, wakaniambia nifumue nywele nilizosuka, ili wanihakiki, hata hivyo nashukuru baada ya kujiridhisha waliniruhusu kupanda ndege na kurejea nchini, siku natua uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere sikuamini, machozi yalikuwa yananimwagika, ilikuwa kama ndoto kuona tena ardhi ya nyumbani,” anasema.

 “Niliposhuka kutoka kwenye ndege, ndugu zangu akiwamo mama na dada zangu walinipokea nilishindwa kujizuia kuangua kilio ili  wasigundue chochote. Ingawa awali sikutaka wajue kuwa nilipitia shida kubwa... lakini moyoni mwangu najua mwenyewe nilivyokuwa najisikia,” anasema.

Anasema hata hivyo mama yake kuna kitu aligundua na kuanza kumuhoji, alimdanganya kuwa hoteli aliyokuwa akifanyia kazi imeungua moto hivyo amelazimika kurudi.,

“Mama alinitazama tu usoni ni kama alihisi kitu, ingawa hakuendelea tena kunihoji,”. anasimulia

Maisha ya Watanzania China:

Kuhusu maisha ya baadhi ya Watanzania nchini China, Rozaline anasema wapo wasichana wadogo wa Kitanzania wanapokamatwa au kutaka kusaidiwa kurudi nchini, hukataa wakiwahofia mawakala  wanaowapeleka huko.

Mawakala hao huwatisha kuwa wakiwataja au kujaribu kutoroka watawaua. Wengi wanaamini kuwa mawakala hao hutegemea nguvu za ushirikina.

Pamoja na hayo, Rozalia anasema wasichana wanaofanya biashara ya kujiuza China, hukumbana na ukatili wa kutisha, huku akitoa mfano wa binti aitwaye Zuhura ambaye aliingiliwa na wanaume kadhaa kwa nguvu na baadaye aliuawa.

 “Niliyotendewa hayawezi kufutika katika historia ya maisha yangu kamwe,” anasema.

Mama Mzazi anena

Mama mzazi wa Rozalia akizungumzia safari ya mwanae kwenda China anasema “siku zote mtoto akililia wembe mpe, mimi wakati ananiambia ile safari moyo wangu ulikuwa mzito sana, nilimkataza kwenda lakini alilazimisha sana.

Anasema  ilifika mahali akahama mpaka nyumbani akaenda kuishi hotelini huko, moyo wangu uliumia sana, lakini nikawa sina jinsi zaidi ya kumuombea, aliyopitia ni funzo tosha hata kwa wengine, namshukuru Mungu tu amerudi salama.

Takwimu za serikali

Katibu wa Sekretarieti ya Taifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Seperatus Fella, amesema kuwa watu 61 wamehukumiwa kwa kosa la kusafirisha binadamu na kesi 12 zinaendelea katika mahakama mbalimbali hapa nchini.

Amesema takwimu hizo ni za kuanzia mwaka 2016 hadi 2020, ambazo zinaonesha kuwa zaidi ya waathirika 557 wameokolewa baada ya kupata matatizo hayo na kwamba wamewasaidia kwa kuwapa huduma za ushauri nasaha, mitaji ya biashara na kuwakutanisha na ndugu zao ambao kwa sasa wanaendelea na shughuli zao nchini.

Amesema changamoto kubwa ya kuendelea kuwepo kwa biashara haramu ya binadamu ni umasikini katika jamii kwani familia nyingi zinapokea fedha kidogo kwa kudanganywa na kutoa mtoto kwenda kufanya kazi mahali bila kujua kama ni kosa na pia biashara hiyo hufanywa kwa usiri mkubwa.

Sheria inasemaje?

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Tike Mwambipile amesema biashara haramu ya binadamu inaangukia kwenye kosa la jinai ambapo sheria ya mwaka 2008 ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu inakataza na atakayebainika adhabu yake ni  kifungo cha miaka miwili hadi 10.

Vile vile atakayebainika na kosa anaweza kulipa, faini kati ya sh milioni tano hadi milioni milioni 100 au adhabu zote mbili kwa makosa yanayohusisha wahanga watu wazima na kufungwa miaka 10 hadi miaka 20, faini kati ya milioni tano na milioni 150 au adhabu zote mbili kwa makosa yanayohusisha wahanga watoto.

Takwimu za Dunia

Shirika la Kazi Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye jukumu la kushughulikia viwango vya kazi, ajira na masuala ya hifadhi ya jamii yanakadiria kuwa kuna watu milioni 12.3 wanaofanyishwa kazi kinguvu, utumwa wa madeni, ajira za kulazimishwa kwa watoto na utumwa wa kingono.

Asilimia 80 ya waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu wa kimataifa ni wanawake na wasichana na asilimia 50 ni watoto chini ya miaka 18.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/935cd23599e132784fb6bc3a1c417229.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi