loader
Kunahitajika jitihada za  pamoja tatizo la maji

Kunahitajika jitihada za pamoja tatizo la maji

MAENEO mbalimbali nchini kwa sasa yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na kusababisha kero na usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Hali hiyo inaelezwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa mvua.

Hata hivyo, pamoja na tatizo la uhaba wa mvua, tunasikitishwa kuona tatizo hilo pia linachangiwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu na wanyama hasa katika vyanzo vya maji.

Katika maeneo mengi nchini kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwamo ukataji misitu ovyo, shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Pamoja na tatizo hilo, baadhi ya watendaji wameshindwa kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kusimamia sekta hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe vingine, kwa kutokuwa makini katika usimamizi na uratibu wa matumizi ya maji pamoja na udhibiti wa uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Juzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikwenda kuangalia vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kushuhudia hali isiyoridhisha ya usimamizi wa sekta hiyo.

Alitoa siku tatu kwa wasimamizi wa Bonde la Mto Ruvu wafuatilie njia za kuingiza maji zilizochepushwa ziwe wazi ili maji yaingie katika mto huo ambao maji yake yanatumiwa na wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Pia, aliwaagiza wasimamizi wa mabonde yote nchini wasikae ofisini, wapite katika maeneo wanayoyasimamia kuhakikisha maji yapo salama.

Inasikitisha kuona watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia matumizi endelevu ya maji wanashindwa kuwajibika kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa na kulindwa pamoja na kuweka uratibu mzuri wa matumizi ya rasilimali hiyo muhimu.

Wito wetu kwa watendaji hao, waaache kukaa maofisini badala yake wawe na utaratibu wa kutembelea na kukagua maeneo ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha wakati wote maeneo hayo yapo salama.

Pia jamii inapaswa kutambua kuwa maji ni uhai, hivyo ina wajibu mkubwa wa kuilinda na kuitunza rasilimali hiyo kwa kuwa na matumizi mazuri pamoja na kulinda vyanzo vya maji kwa nguvu zote.

Aidha, tunatoa wito kwa watafiti kufanya tafiti za maji na mazingira ya mito kwa ajili ya kuisaidia serikali kupanga mipango ya namna bora ya kuyahifadhi na matumizi yake.

Tafiti hizo zijikite kuangalia masuala ya mazingira yakiwamo ya umwagiliaji, kilimo kando ya kingo za mito, ufugaji na mifugo ndani ya madakio ya mito na mabonde  na ongezeko la watu.

Tatizo la maji limekuwa likimnyima usingizi Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihangaika usiku na mchana kuhakikisha huduma hiyo inapatikana bila ya matatizo tena karibu na makazi ya wananchi. 

Hivyo, jamii kwa umoja wetu, watendaji katika sekta hiyo ikiwamo Wizara ya Maji na wadau wengine tunatakiwa kulinda vyanzo vya maji kwa kuhakikisha shughuli za kilimo, ufugaji, viwanda, ukataji miti ovyo na nyingine hazisababishi upungufu wa maji.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/85d7b0a44f8722e574a0338bc34c9bed.jpg

KATI ya kero kubwa iliyosumbua wakazi wa Jiji ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi