loader
Shirecu na safari ndefu ya kumkomboa mkulima

Shirecu na safari ndefu ya kumkomboa mkulima

USHIRIKA ulianzishwa kwa lengo la kumsaidia mkulima ili kujinyanyua kiuchumi kipindi cha ukoloni baada ya kuanzishwa kwa mashamba makubwa ya mazao ya biashara kama vile pamba, katani na tumbaku.

Aliyekuwa Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) na baadaye Mjumbe wa Bodi ya Pamba, Joseph Mihangwa anasema kuwa ushirika wa kwanza hapa nchini ulianzishwa mwaka 1925 kupitia Kilimanjaro Native Plants Association (KNPA).

“Katika muundo wa kuanzisha ushirika kwa Sheria namba 2013 ya mwaka 1976, ndipo Shirecu Ltd ikaanzishwa mwaka 1984 mkoani Shinyanga ambayo inahusisha mikoa ya Simiyu, Geita kwa wilaya ya Bokombe na Mbogwe na Mkoa wa Simiyu kwa wilaya za Bariadi na Maswa,” anasema Mihangwa.

Mihangwa anasema kuundwa ushirika kulilenga wakulima kuungana ili kuweza kukidhi mahitaji ya kiuchumi na mwaka 1932 sheria ya kwanza ya ushirika ikatungwa wakati wa ukoloni kuwahamasisha wajiunge kwenye vikundi lengo waingie kwenye ushirika.

Anasema kuwa baada ya kupata uhuru kukawepo sheria mbalimbali ikiwamo ya mwaka 2013 ikitaka ushirika ujitegemee na kuwakomboa wakulima kwa kuunda vyama vya msingi (Amco’s) na sheria ya kimataifa iitwayo ROCHDALE iliyobuniwa na wanaushirika wenyewe.

“Kuna misingi ambayo ilianzishwa mwaka 1932 kwenye ushirika mpaka sasa yapo mfano kuunganisha wakulima na kuwashawishi wajiunge kwenye Amco’s, kuwa na mkutano mkuu na kusikiliza ushauri pande zote,” anasema Mihangwa. Mihangwa anasema katika misingi iliyowekwa kwenye sheria ya 2013 ya mwaka 1932, wanaushirika walisisitizwa mambo matatu; lazima kufuata msingi wakianzia kwa mwanachama wa hiari.

Anasema la pili ni ushirika na uongozi wa pamoja na tatu kukidhi matakwa ya kiuchumi ya wanachama. Mihangwa anasema kabla ya kupata uhuru mwaka 1955 uliundwa ushirika uliokuwa ukijulikana kama Victoria Federation of Coopetives kwa Kanda ya Ziwa na baadaye kujulikana kama Nyanza.

Anasema kuwa ushirika wa Nyanza ulijumlisha mikoa ya Mara, Geita, Mwanza na Shinyanga na kilikuwa chama kikubwa cha pili barani Afrika. Mihangwa anasema kuwa ushirika huo ulishiriki katika harakati za kupigania uhuru mwaka 1961 na mwaka 1972 ikagawanyika kwa misingi ya kikoloni ikimaanisha sera ya madaraka mikoani na kila mkoa ukagawanyika na kuunda ushirika wake, mojawapo ni Mkoa wa Shinyanga.

“Na mwaka 1976 baada ya kupata uhuru vyama vyote vya ushirika vikafutwa na badala yake ikaundwa mamlaka ya pamba na mamlaka ya tumbaku na kurejeshewa tena ushirika kwa sheria ya mwaka 2013 iliyotungwa mwaka 1984 na ndiyo chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (Shirecu 1984) kikazaliwa,” anasema Mihangwa.

Anasema mwaka 1966 ushirika ulikuwa na nguvu na baadaye ulipunguza nguvu hiyo baada ya kuingiliwa na siasa na mwaka 1976 mali zote za ushirika kama vile benki ya ushirika, shule, vituo vya mafuta, vilichukuliwa na serikali.

Mihangwa anasema sheria ya mwaka 1991 ilibadilishwa na kutaka vyama vyote vya ushirika wanunue mazao ya aina yote. Mihangwa anasema kuwa mwaka 1984 Shirecu ilikuwa haina fedha na matokeo yake walidhaminiwa na serikali kupata mkopo kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na walipokuwa wakitaka kununua mazao serikali ilikuwa ikipanga bei na ushirika kujiendesha.

Mihangwa anasema kuwa mwaka 1992 hadi 1993 kuliingia soko huria na kukawa na viwanda vingi vyenye ushindani vilivyojengwa, mfano viwanda vya mafuta ya pamba vilivyokuwa Uzogore, Mhunze iliyopo Kishapu, Shinyanga Oil Milling, Maswa Oil, Malampaka Oil na Uluguru Oil.

“Viwanda hivyo kwa serikali na Shirecu mwaka huo iliweza kupata faida ya Sh bilioni 1.2 hali ambayo haijawahi kutokea. “Miaka hiyo ushirika ulifanya kazi nzuri kwa kujenga jineri za kuchambua zao la pamba ambazo ni Mhunze, Maswa –Sola, Malampaka, Luguru na Masumbwe,” anasema Mihangwa. Mihangwa anasema vyama viwili ambavyo vimebaki na nguvu kubwa nchini ni Shirecu na Nyanza. Vingine vipo lakini havisikiki sana.

Mwenyekiti wa Shirecu, Kwiyolecha Nkilijiwa, anasema kuwa wameunda Umoja wa Wakulima wa Mazao (TANCOPS) ambapo wanashughulika na kuongelea changamoto za wakulima wa mazao yote. Nkilijiwa anasema mfumo wa stakabadhi ghalani umemsaidia mkulima kunufaika na mazao anayoyazalisha na kuacha kuibiwa na walanguzi. Anasema manufaa yaliyopatikana ni kuwepo soko la uhakika na bei ya pamba kufikia asilimia 100 pamoja na kuongezeka kwa ajira.

“Shirecu imepiga hatua kubwa kuwa na vyama vya msingi 142 na watumishi 80 na kuhakikisha wakulima kuwa wanalipwa kwa mfumo wa kielektroniki na kuhamasisha wakulima kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),” anasema Nkilijiwa. Kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniface anasema mfumo wa stakabadhi ghalani unasaidia kuziwezesha halmashauri kupata mapato yake bila usumbufu, kutokana na kuwa na sehemu maalumu ya kuuzia mazao yao.

Boniphace anasema kuna vyama vya msingi (Amco’s) 462 ambavyo wakulima wa mazao ya nafaka na biashara wamejiunga na kupata soko lenye uhakika kupitia stakabadhi ghalani na jumla ya Amco’s 197 ndizo zinazojishughulisha na kilimo cha pamba. Mpaka sasa Shirecu ina Amco’s 142 na kwa msimu wa mwaka uliopita kilo milioni 14 za pamba zilinunuliwa baada ya wakulima kuuza pamba kwenye vyama vya msingi.

Wanaushirika kutoka Amco’s ya Mwalukwa, Dotto Jilindu na Ngassa Mhoja wanasema kwa nyakati tofauti kuwa Shirecu imepiga hatua ingawa bado inakumbwa na changamoto nyingi, imetoa elimu ya kilimo cha kisasa na kuzingatia kanuni 10 za kilimo bora na kibiashara zaidi kuuza mazao yao kwenye stakabadhi ghalani.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga, Emanuel Kaptila na Suzana Mori wanaelezea kuwa Shirecu ilikuwa ikitikisa hasa kwenye miaka ya 91 hadi 99 hata kuwafanya wafanyakazi wa ushirika huo kuonekana mitaani kuwa wenye fedha na kumiliki gari na nyumba za kifahari enzi hizo.

SHIRECU IMEINGIA KWENYE HISTORIA NYINGINE

Mwanasheria wa Mkoa wa Shinyanga, Lightness Tarimo anasema kuwa vyama vikuu vitatu vya ushirika nchini vilivyokuwa ndani ya Shirecu vimesaini makabidhiano ya kugawana mali, madeni pamoja na watumishi.

Tarimo anasema kuwa Sheria namba 2013 kifungu namba 11 kipengele cha namba 98 na kifungu xii, kipengele cha 99 ambacho kimetaka kugawanyika kwa ushirika kwa hiari na sheria hizo hizo ndizo zinataka kugawanywa kwa mali za ushirika kwenye ushirika ulioundwa upya.

Mgawanyo huo umetokana na kuundwa kwa mikoa ya Simiyu na Geita ambapo baadhi ya maeneo yalikuwa yakihesabika kiutendaji kuwa chini ya chama kikuu cha ushirika Shinyanga (Shirecu 1984) na sasa mikoa hiyo imeunda ushirika wake. Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Benson Ndiege ambaye aliwahi kushiriki kwenye makabidhiano ya mali za ushirika yakiwemo madeni na ikama ya watumishi wa vyama vilivyoanzishwa na Shirecu, anasema uthamini wa mali za vyama hivyo kama vile viwanda, ardhi na madeni ulifanywa kwa mujibu wa sheria.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge, anasema kuwa amefurahi kukamilika kwa kazi hiyo imepunguza kazi na Shirecu kuwa kwenye historia bila kuwepo migogoro. Kaminyoge anasema Simiyu kuna jineri za Maswa –Sola na Uluguru wanawajibu mali hizo walizopata waziendeleze kwa kuzifufua kwa ushirika wa Mkoa wa Simiyu kulingana na ilivyopata mgawo kutoka Shirecu.

Mrajisi Msaidizi, Doreen Mwanri kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Geita anasema kuwa baadhi ya wajumbe wa bodi wamekuwa wakikiuka sheria na kushindwa kusimamia mali vizuri kwani zipo ambazo hazifanyi kazi na ni wajibu wa viongozi kufufua na kuomba msaada wanapokwama.

Mwenyekiti wa Shirecu, Kwiyolecha Nkilijiwa anasema kuwa historia hii ya kugawana mali haijaanza leo kwani ilifanyika kwa chama kikuu Nyanza cha mkoani Mwanza kugawana na Shirecu.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/dddfe756f978e5a1a200661b7f356c1c.jpeg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Na Kareny Masasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi