loader
Mikakati ya mabadiliko Mikakati ya mabadiliko ya tabianchi ianzie chini

Mikakati ya mabadiliko Mikakati ya mabadiliko ya tabianchi ianzie chini

KATIKA kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wanafunzi wa sekondari na vyuo hawana budi kufanya tafi ti za kutosha zitakazotatua changamoto za mazingira. Wanafunzi wa sekondari na vyuo kwa kufanya tafiti hizo kutawaongezea weledi na ufanisi katika masomo yao lakini pia watakuwa wamelisaidia taifa katika kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St. Crolus iliyopo Manispaa ya Singida, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo anatoa mwito kwa shule za sekondari na vyuo vikuu nchini kufanya tafiti za mazingira kwa wingi ili kupata suluhu ya changamoto zinazoikabili sekta ya mazingira nchini.

Jafo ametoa rai hiyo Agosti 5, 2021 alipotembelea mradi wa ustawishaji miche kwa kutumia vyungu unaotumia maji kidogo uliobuniwa na wanafunzi wa shule hiyo ya St Crolus katika Manispaa ya Singida.

Anatumia fursa hiyo kuwapongeza wanafunzi hao wanaosoma kidato cha kwanza katika shule hiyo kwa ubunifu wa mradi huo na kusema kuwa ni mojawapo ya mbinu za kuhifadhi mazingira.

“Nimefurahishwa sana na wanafunzi hawa na hii inanipa faraja kubwa kwani vijana hawa wakimaliza kidato cha nne watakuwa watu mahiri kabisa na ndio maana natoa wito kwa shule zingine kufanya tafiti zao kuhusu mazingira ili tupate kutatua changamoto za mazingira,” anasema Jafo.

Aidha, waziri huyo aliwapongeza wanafunzi hao kwa kuwa mradi huo unatumia maji kidogo katika kustawisha miche ya miti hatua inayosaidia kupunguza umwagiliaji wa kila siku. Jafo anasema mradi huo unasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kuwa hutumia uchafu zikiwemo ndoo kwa ajili ya kupandia miche ambazo kama zingeachwa zingeweza kuzagaa katika mazingira.

Hata hivyo, Jafo anawakumbusha wataalamu wa kilimo katika halmashauri kuzungukia vijana wanaobuni miradi kama hiyo na kuwapa elimu ya matumizi ya mbolea kwa usahihi ili miche inayostawishwa iweze kukua. Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo, Mwalimu Yesaya Bendera anasema matarajio yao katika utafiti huo ni kupata majibu ambayo yatasaidia kuifanya Singida na nchi nzima kuwa kijani. Bendera anasema kuwa kwa kutumia mbinu hiyo kutapunguza adha kubwa ya kuchota maji kwa wingi na kumwagilia miche na badala yake watatumia maji kidogo.

Anasema katika utafiti waliofanya Januari 2021 katika maeneo mbalimbali mjini Singida, asilimia kubwa ya waliohojiwa walilalamika kutumia muda mrefu kuchota maji kwa ajili ya kumwagilia badala ya kufanya shughuli za uzalishaji, hivyo waliamua kubuni mradi huo.

Kuanzia mwaka 1999 aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Fredrick Sumaye alianzisha Kampeni ya “panda mti, kata mti” iliyorudisha uhai wa misitu nchini baada ya kuwa na tishio la nchi kuwa jangwa. Misitu mingi yakupandwa inayoonekana imetokana na kampeni hiyo lakini viongozi waliofuata pia walisisitiza upandaji miti akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Kufuatia kampeni hizo zilizosimamiwa na viongozi wa ngazi za juu ya nchi kuliwezesha kuanzishwa kwa klabu mbalimbali za upandaji miti na miji mingi kuonekana ya kijani ikiwemo Singida, Shinyanga na Dodoma.

Kufanyika kwa tafiti nyingi kutasaidia taifa kuchukua tahadhari dhidi ya uchafuzi wa mazingira, athari zake kama vile mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha nchi kutokuwa na mvua ya uhakika lakini ongezeko la joto na nchi kuwa jangwa.

Mfano mzuri ni utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambao umebaini idadi ya siku za joto kali hivi sasa kila mwaka inaongezeka huku hali ya hewa ikifikia nyuzi joto 50 duniani ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na miaka 40 iliyopita (1980).

Kwa mujibu wa utafiti huo hali hiyo imejitokeza maeneo mengi duniani tofauti na miaka ya nyuma na kutishia afya ya viumbe vilivyopo duniani. Utafiti huo unaeleza kuwa kati ya mwaka 1980 hadi 2009, hali ya hewa ilipita nyuzi joto 50 kwa siku 14 ndani ya mwaka lakini sasa idadi ya siku hizo imeongezeka na kufikia siku 26 kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2019.

Katika kipindi hicho hali ya joto ndani ya mwaka ni nyuzi joto 50 hutokea kwa siku 14 ndani ya mwaka. “Ongezeko hilo linaweza kuhusishwa na uchomaji wa makaa ya mawe,” anasema Mkurugenzi wa Taasisi ya Mabadiliko ya Mazingira katika Chuo Kikuu cha Oxford, Dk Friederike Otto.

Anasema kuwa dunia nzima inapata joto ndiyo maana kuna ongezeko kubwa la joto. Dk Otto anasema joto kali kupita kiasi ni hatari kwa maisha ya binadamu na mazingira na linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa majengo, barabara na hata mifumo ya nishati.

Nyuzi joto 50 mara nyingi hufika katika maeneo ya Mashariki ya Kati na maeneo ya ghuba baada ya Italia kuvunja rekodi ya kufikia hali ya hewa ya nyuzi joto 48.8 na Canada kufikia 49.6 katika kipindi cha majira ya joto mwaka huu. Hata hivyo, wanasayansi walitaarifu kuwa huenda joto likapanda zaidi siku za usoni.

Hapa nchini Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetahadharisha kuhusu ongezeko la joto na kutaka watu wachukue tahadhari na kunywa maji ya kutosha.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/7f723cbb513aafcbcb053d58a99e8fde.jpeg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Na Dunstan Mhilu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi