loader
Uvaaji barakoa na mitindo Uvaaji barakoa na mitindo kinzani ya maisha

Uvaaji barakoa na mitindo Uvaaji barakoa na mitindo kinzani ya maisha

NJIA mojawapo ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) ni kuvaa barakoa katika maeneo hatarishi, yenye msongamano wa watu wengi.

Hata hivyo, pamoja na hamasa kubwa inayotolewa na serikali kupitia viongozi wa kitaifa, kiimani na kijamii, bado wananchi wengi wamepuuza uvaaji wa barakoa na kusababisha kuwa katika hatari ya kuambukiza na kuambukizwa ugonjwa huo.

Mkazi wa Chanika Buyuni, jijini Dar es Salaam, Amina Haule, anakiri kuwa hajaona umuhimu wa kuvaa barakoa hata anapokuwa katika msongamano wa watu kama sokoni, kwenye daladala kwa kuwa hajawahi kuugua corona wala kumuona mtu aliyeugua ama kufa kwa ugonjwa huo.

"Najua kuna umuhimu lakini mimi sijawahi kuvaa barakoa popote, lakini ninajikinga na maambukizi kwa kunawa mikono pamoja na kutoshikana mikono na watu,” anasema Amina huku akiahidi kuanza kutumia barakoa atakapokuwepo kwenye msongamano wa watu.

Kauli hii ya Amina inawahusu watu wengi nchini ambao licha ya kutambua kuwa uvaaji barakoa ni muhimu kujikinga na Covid-19, lakini bado hawaoni umuhimu huo na hivyo kuongeza tatizo katika jamii.

Ufuatiliaji kama watu wanazingatia kanuni na miongozo ya afya kuhusu janga hilo uliofanywa na HabariLEO hivi karibuni umebaini kuwa, hivi sasa katika maeneo mengi nchini watu hawachukui tahadhari tena ya janga hilo hasa kuvaa barakoa wakidai kipindi cha joto maambukizi si mengi huku wakisahau kuwa maambukizi yako pale pale kwa kuwa tatizo bado halijamalizika.

Hata hivyo, HabariLEO imebaini kuwa, tahadhari ya kutokusalimiana kwa kushikana mikono bado inaendelea kuchukuliwa ingawa katika sherehe na mikutano ya familia hasa mkoani Dar es Salaam, watu wanashikana mikono bila kujitakasa au kunawa kwa maji tiririka.

Gazeti hili katika ufuatiliaji wake kuhusiana na uvaaji wa barakoa limebaini kuwa katika maeneo ya watu wengi kama sokoni, kwenye usafiri wa umma, ofisini na hata kwenye msongamano mkubwa wa watu, watu wengi hawavai barakoa. Ufuatiliaji wa siku mbili wa gazeti hili katika maeneo ya soko la Kariakoo na la matunda Tazara, usafiri wa daladala wa kwenda Yombovituka, usafiri wa treni na sehemu za baa hasa za Tabata, uvaaji wa barakoa kwa asilimia kubwa umepungua.

Soko la Matunda Tazara ni kati ya masoko yanayotembelewa na watu wengi kwasababu linauza aina mbalimbali za matunda kwa bei ya jumla na rejareja, lina eneo kubwa na ukaribu wake na kituo cha daladala kutoka na kuelekea sehemu mbalimbali za jiji unakaribisha wateja wengi zaidi.

Lakini kwa siku mbili ambazo gazeti hili lilitembelea soko hilo hakuonekana muuzaji aliyekuwa amevalia barakoa, wengi walionekana wakiendelea na biashara zao huku wateja nao hawakuwa na barakoa. Akizungumza na gazeti hili muuza parachichi aliyejitambulisha kwa jina la Juma Amir alisema haoni sababu ya kuvaa barakoa kwa kuwa amekuwa akiendesha biashara yake siku zote tangu wimbi la kwanza mpaka sasa na hajawahi kuugua. Amir anasema barakoa inamkosesha pumzi na haoni sababu ya kuvaa kwa kuwa ameshachanja chanjo ya Johnson Johnson hivyo ana uhakika hawezi kupata madhara makubwa hata akipata maambukizi.

Hoja ya Amir ni ya kweli lakini kauli mbalimbali za Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu vita ya janga hilo, amekuwa akisisitiza hata kama mtu amechanja, aendelee kuchukua tahadhari zote ili kumlinda mwingine hasa kutokana na ukweli kwamba, chanjo ya Covid-19 nchini ni hiari.

Kwa upande wake muuza chakula katika eneo hilo, Eva Mwanda anasema kuwa kutokana na asili ya kazi yake hiyo anahitajika kushughulika zaidi hasa kuwasha na kuchochea moto jikoni, kuchambua mboga na kisha kuhudumia wateja hivyo havai barakoa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke ambaye soko hilo lipo eneo lake, Jokate Mwegelo anasema kuwa bado kuna haja ya wananchi kuendelea kuvaa barakoa hata kama wamechanja. “Uvaaji wa barakoa si urembo na wala si sehemu tu ya kumridhisha mtu ila ni wajibu wa watu kuwalinda wengine kwa kuvaa barakoa, kuchanja na kuendelea kuchukua tahadhari zinazotakiwa,” anasema Jokate.

Kwa upande wa usafiri wa umma, asubuhi na jioni ni nyakati zenye abiria wengi hivyo wanajaa sana kwenye mabasi na asilimia kubwa hawavai barakoa. Johnson Mori, mkazi wa Yombo- Vituka kwa Gude, Dar es Salaam, anasema kuwa hajawahi kuvaa barakoa kwa kuwa si mtindo wake wa maisha ingawa anajua umuhimu wake. Serikali imekuwa ikitaja uvaaji wa barakoa kama njia muhimu ya kujikinga dhidi ya Covid-19 na hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, aliagiza na kuweka lazima kila mtu kuvaa barakoa mkoani humo.

Uvaaji barakoa nchi za Ulaya Upuuzwaji wa kuvaa barakoa si kwa Tanzania tu bali hata baadhi ya nchi za nje nako kuna hali hiyo ya kupuuza kuvaa barakoamfano Uingereza imetajwa kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi ya Covid-19 ikilinganishwa na nchi nyingine za Ulaya ambapo kati ya sababu ni watu kutovaa barakoa.

Kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa na Chuo cha Imperial College London, Uingereza imekuwa ikisisitiza zaidi uvaaji wa barakoa kwa watu wanaokuwa kwenye shughuli za ndani kama ofisini, darasani, chuoni na sehemu nyingine za ndani lakini kampeni za uvaaji barakoa sehemu za umma haijawekewa msisitizo wa kutosha.

Utafiti huo pia umebaini kuwa wananchi wa Uingereza wakienda sehemu za starehe, wakiwa kwenye mikusanyiko ya watu na hata wakitumia usafiri wa umma hawavai barakoa. Inaonekana kuwa wananchi wanachukulia kuvaa barakoa kama mtindo tu wa maisha usio wa lazima badala ya kuchukua kama sehemu muhimu ya kujilinda dhidi ya Covid-19. Ipo haja ya nguvu kubwa kuwekwa katika kinga kuliko tiba.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/a641943fb73cc2c3218e597dbd0b439e.jpeg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Na Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi