loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mahakama kuamua mapingamizi ya Mbowe

Mahakama kuamua mapingamizi ya Mbowe

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo inatarajia kutoa uamuzi wa mapingamizi matatu ya upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Jaji Joachim Tiganga aliahirisha kesi hiyo Novemba 18 mwaka huu na anatarajiwa kutoa uamuzi leo.

“Nimefanya tathimini na uwezekano wa kusema mpaka kesho asubuhi utakuwa ni mgumu. badala yake tuje Jumatatu Novemba 22, 2021. Shahidi unaombwa kurudi Mahakamani. Washitakiwa wataendelea kuwa chini ya Magereza,” alisema Jaji Tiganga.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala waliwasilisha mapingamizi hayo Novemba 17 mwaka huu ukiwa ni mfululizo wa mapingamizi ambayo wamekuwa wakiwasilisha. Kabla ya mapingamizi hayo matatu Jaji Tiganga alitupa ombi la kutaka mahakama imuondoe shahidi wa pili katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, Koplo Msemwa pamoja na kufuta ushahidi wake.

Alikubali ombi la utetezi kwamba shajara aliyokutwa nayo shahidi huyo kizimbani ikaguliwe na hili lilifanyika kwa ushirikiano wa mawakili wa pande zote na ofisa wa mahakama. Baada ya ukaguzi huo shahidi huyo aliendelea na ushahidi na akaomba kuwasilisha kitabu cha kumbukumbu za mahabusu kutoka katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam ili kiwe kielelezo cha ushahidi katika mwenendo wa kesi hiyo.

Upande wa utetezi ulipinga kupokelewa kitabu hicho kwa kile walichodai mnyororo wa utunzwaji wa kielelezo ulikiukwa na shahidi alishindwa kueleza namna kitabu hicho kilivyomfikia kwa kuwa tayari kilishawasilishwa mahakamani kama kielelezo katika shauri hilo.

Kesi hiyo ndogo ilifunguliwa baada ya shahidi wa nane katika kesi ya msingi, Jumanne Malangahe kuomba kukabidhi maelezo ya onyo aliyodai aliyachukua kwa mshitakiwa wa tatu, Mohamed Ling’wenya katika kituo kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam. Jambo hilo lilipingwa na upande wa utetezi ambao walidai maelezo hayo yalichukuliwa kwa mateso na pia mshitakiwa alisainishwa kwa shuruti.

Waliomba kufunguliwa kwa kesi hiyo ndogo ili kusikilizwa mashahidi na kuthibisha hoja zao na ndani yake pia kukazaliwa mapingamizi kadhaa yakiwemo yanayotarajiwa kutolewa uamuzi leo.

Kesi hiyo ndogo ni ya pili kufunguliwa ndani ya kesi hiyo ya msingi baada ya ile ya kwanza ambayo upande wa utetezi walipinga shahidi wa kwanza wa kesi ya msingi, Ramadhani Kingai kukabidhi maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa pili, Adam Kasekwa wakidai yalichukuliwa kwa shuruti na mateso na yalichukuliwa nje ya muda.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/39a8a9542b34fcd46c6b68e081782a51.jpg

SERIKALI imepanga kujenga ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi