loader
Mbivu za ‘Wanawake Wanaweza’ katika siasa kupitia wanahabari, viongozi wa dini

Mbivu za ‘Wanawake Wanaweza’ katika siasa kupitia wanahabari, viongozi wa dini

OKTOBA Mosi, 2020, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kilitangaza kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa mwaka mmoja wa ‘Wanawake Wanaweza’ unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake (UN-Women).

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben akasema: “Hii ni fursa adhimu kwa Tamwa ambayo baadhi ya malengo yake makuu ni kutetea haki za wanawake na watoto, kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na kuondoa mifumo kandamizi inayochochoea ukatili kwa makundi hayo maalumu kwa kutumia vyombo vya habari.”

Ikumbukwe kuwa, Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, sheria mbalimbali za Tanzania, Tamko la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW 1979) katika Kifungu cha 7: (a,b na c) na Mapendekezo ya Baraza la Usalama (UNSC 1325 (2000) yanatoa na kutambua haki za wanawake kushiriki katika uchaguzi kama wapiga kura na wanaowania nafasi za uongozi, wanaoteuliwa na kugombea hatimaye kushinda katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa kupitia uchaguzi. 

Katika mradi wa ‘Wanawake Wanaweza,’  jukumu  kubwa la Tamwa lilikuwa kuongeza uelewa kwa umma juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi pamoja na madhara ya magonjwa ya mlipuko kama Covid-19 kwa wanawake na wasichana.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya Mwaka 2016, asilimia 17 ya mawaziri ni wanawake, makatibu wakuu wanawake ni asilimia 11, wakuu wa mikoa ni asilimia 23, wakuu wa wilaya ni asilimia 28. Hii inaonesha kuwa, bado nafasi ya mwanamke katika ngazi za uongozi ni mdogo.

Katika utambulisho huo, Dk Rose akasema: “Hata hivyo, bado tunaupongeza Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli (sasa ni marehemu); …Kwa mara ya kwanza amechaguliwa Makamu wa Rais mwanamke nchini, Mama Samia Suluhu Hassan (Sasa ni Rais wa Tanzania).”

Akaongeza: “Hivyo basi katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi huu, Tamwa na wadau wake, tunatarajia kutumia nyenzo muhimu zilizopo kuongeza uelewa kwa jamii na kuhakikisha wanawake wanaonekana kuwa viongozi halali na madhubuti katika jamii.”

Anashukuru ushirikiano mkubwa walioupata katika ngazi mbalimbali za serikali yaani kata wilaya, mikoa na hata ngazi ya kitaifa, viongozi wa dini, taasisi za habari, taasisi za jinsia na viongozi wa kimila.

Hivi karibuni katika mkutano wa kupeana mrejesho uliofanyika Dar es Salaam mintarafu hali ya utekelezaji wa mradi huu ulioanza Agosti 2020 na kutarajiwa kuhitimishwa Novemba 30, mwaka huu, Meneja wa Mradi wa Wanawake Wanaweza, Sylvia Daulinge, alisema Tamwa kupitia mradi huo, kimewajengea uwezo wanahabari katika kuripoti habari za jinsia na ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika uongozi na siasa kama lengo kuu sambamba na madhara ya Covid-19 kwa wanawake nchini.

 “Tuliendesha pia midahalo ya kihabari ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi,” anasema Sylvia na kwamba, mradi ulitekelezwa katika mikoa 17 ikiwamo ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara, Wilaya 112 za mikoa hiyo na kata 458.

Uchunguzi wa HabariLEO umebaini kuwa, wadau wengine walioshiriki katika mradi huo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salam (UDSM), Kitivo cha Sayansi ya Jamii, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shirika la Wanasheria Wanawake na Maendeleo Afrika, (WILDAF), na viongozi wa dini na viongozi wa kimila.

Wengine ni Mtandao wa Radio za Kijamii nchini (TADIO), Wizara ya Habari na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika (AWLN) na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Kwa mujibu wa Tamwa, wakati wa utekelezaji wa mradi wadau hao kwa nafasi zao, walikuwa na mengi ya kuishirikisha Tamwa na kwamba, umoja huo ndicho chanzo cha mafanikio ya utekelezaji wa mradi.

Kuhusu mafanikio Meneja wa Mradi, Sylvia, anasema ni pamoja na hasa kuimarisha uwezo wa wanahabari kuandika na kutangaza habari kwa kuzingatia usawa wa kijinsia sambamba na kuchora taswira bora ya mwanamke katika jamii hususan katika ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi katika maeneo mbalimbali zikiwamo taasisi, kampuni na masharika.

 “Tunashukuru kwamba sasa, jamii inazidi kuelewa na wanawake wanazidi kuchukuliwa kama viongozi halali kama walivyo wanaume,” alisema Sylvia na kuongeza: “Kubwa zaidi, tunampongeza Mama Rais Samia kwani tangu aingie madarakani, amezidi kuwatambua na kuwainua wanawake wenye uwezo na sifa na kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi.”

Katika mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam kupata mrejesho wa utekelezaji, Mwakilishi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Ingiahedi Mduma, alisema serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inafurahi kuona mradi huo ulianza, umetekelezwa sawia na sasa unaelekea hitimisho huku ukionesha matunda mengi chanya.

 “Tamwa wanafanya juhudi kubwa kuelimisha umma kupitia wanahabari kuhusu haki za wanawake kushiriki katika siasa na uongozi. Hili ni moja ya haki za watu ambazo Rais Samia Suluhu anazisisitiza na kuzipigania kwa vitendo kwa ajili ya ustawi wa Watanzania,” alisema Ingiahedi.

Naye Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Tumaini (TURDAco), Mary Kafyome, anasema mradi umekuwa na manufaa hata kwa wanafunzi kwa kuwa umewapa wigo mpana wa namna ya kushughulikia habari kwa mtazamo wa kijinsia katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Dk Rose, katika utekelezaji wa mradi huu unaoshirikisha taasisi mbalimbali wadau, radio za kijamii 50 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara zilishirikishwa na kwamba zilitumika pia televisheni 10, magazeti 20 na radio 10 za masafa marefu.

“Katika kufanikisha lengo kuu la mradi huu, Tamwa iliwajengea uwezo wanahabari katika kuripoti habari za jinsia na ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika uongozi na siasa na kuwafikia pia wazee maarufu, wazee wa jadi na viongozi wa dini,” alisema Dk Rose.

“Kutokana na mafunzo kupitia mradi huu, vipindi 150 vinavyoelimisha kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi vilirushwa kupitia radio na televisheni na vingine vilihusisha viongozi wa dini 23 na wa kijamii 22 wakiwamo wanawake 5 katika mikoa 127 ya Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Tamwa, changamoto zilizoonekana katika mradi ni pamoja na nafasi ndogo katika vipindi vya redio na televisheni na pia, kuwapo mitazamo duni yua watu kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.

Sauda Msangi kutoka Tamwa anasema miongoni mwa mambo yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa mradi wa Wanawake Wanaweza, ni pamoja na baadhi ya wandishi waliopewa mafunzo kushinda tuzo mbalimbali kutokana na makala kuhusu agenda za mradi.

Anasema: “Tamwa ilifanikiwa kuchangia kuzalisha maudhui kwa vyombo vya habari,” anasema Sauda.

Katika majadiliano wakati wa mkutano huo, wandishi mbalimbali wa habari walikiri mafunzo kua Tamwa kupitia mradi huo kubadili mtazamo na uandishi wao mintarafu habari zinazohusu masuala ua jinsia.

Shehe wa Mkoa wa Dares Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Amani, Alhad Mussa, anasema uwepo  wa Rais mwanamke (Samia) sambamba na mafunzo, utekelezaji wa Wanawake Wanaweza na wadau wengine, umekuwa na maendeleo makubwa ya wanawake kushirikishwa katika uongozi katika taasisi mbalimbali.

 “Rais wetu naye anawasha na kuchochea moto sana kwa wanawake kujitambua na kujitokeza katika siasa na uongozi…,” anasema Shehe Salumu na kuongeza: “Mradi huu umefikia watu wengi maana hata mimi nilikuwa mkufunzi kwa watu wa kada mbalimbali hivyo, niliona watu walivyonufaika na kufurahi...”

Shehe Salumu anasema katika taasisi anazoongoza, sasa wanawake wanazo nafasi mbalimbali za uongozi na wanaonesha uwezo mkubwa hivyo, wanaume wajitokeze zaidi kuwasaidia ili wafanikiwe. “Unajua kumsaidia mwanamke ni ibada,” anasema.

Watu mbalimbali wanapongeza juhudi za Rais Samia kutambua uwezo wa wanawake katika uongozi na kuwateua katika nyadhifa mbalimbali wakiwamo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na mawaziri na mfano ni uteuzi wa hivi karibu wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Stergomena Tax.

Huyu kama ilivyo kwa Samia kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kushika nafasi ya Umakamu wa Rais na hata kuwa Rais, Dk Tax naye amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT nchini.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/55a72b5c4739fca758f8d7c7fc22e1fa.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi