loader
KUELEKEA MIAKA 60 YA UHURU:    Ushuhuda waliofanya kazi na Nyerere  

KUELEKEA MIAKA 60 YA UHURU: Ushuhuda waliofanya kazi na Nyerere  

DESEMBA 9 mwaka huu, Tanzania Bara inatimiza miaka 60 ya Uhuru wake uliopatikana kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na waasisi wa taifa wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Yapo mafanikio mengi yaliyopatikana kwa muda wa miaka 60. Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa yenye ushuhuda juu ya mafanikio hayo. Mkoa ulianzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne kwa tamko la Rais Jakaya Kikwete Oktoba 18 la mwaka 2015.

Tamko hilo lilifuatiwa na Tangazo la Serikali katika Gazeti la Serikali (GN) Na 461 la Januari 29, mwaka 2016 lililotolewa katika uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

Songwe ilipata hadhi ya kuwa mkoa kutokana na kupiga hatua kubwa katika uzalishaji, miundombinu, kilimo, mipaka, mapato, elimu bora na utalii.

Mwandishi wa makala haya kwa msaada wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, amewatembelea baadhi ya Watanzania walioshuhudia uhuru ukipatikana, waliofanya kazi wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere wakibainisha namna nchi ilivyopiga hatua kubwa ndani ya miaka 60 ya uhuru.

Wanasema kuanzishwa kwa mkoa huo kumechochea  kupiga hatua kubwa za kimaendeleo miongoni mwake ikiwa ni kusogezewa huduma mbalimbali za kijamii karibu na kuondokana kuzifuata mbali. 

Nelson Mwampashe mwenye umri wa miaka 86, anajitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa kwanza na mwanzilishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Katibu ALAT Taifa na Katibu wa TANU katika miaka ya 1960. 

Mwampashe anasema miaka 60 ya Uhuru kuzaliwa kwa mkoa mpya wa Songwe kumesogeza huduma nyingi za kijamii ambazo 

“Maendeleo haya yote ambayo tunayapata hivi sasa ni jitihada kubwa ambazo zilifanywa na sisi kipindi hicho, kuanzishwa kwa Mkoa wa Songwe mwaka 2016 ninakifananisha na kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa ambavyo lengo kubwa la Mwalimu Nyerere lilikuwa ni kuwawaweka Watanzania pamoja ili serikali iwasogezee huduma karibu,” anasema. 

Mzee huyu anasimulia, “Mimi nikiwa mwenyekiti wa kwanza wa Halmashauri ya Mbozi na kipindi nilichokuwa kiongozi wa TANU nilikuwa natumia baiskeli kutembelea wanachama na wananchi wote wa Wilaya ya Mbozi ambayo ndio Mkoa wa Songwe hivi sasa.” 

“Viongozi wetu wa awamu zote sita wanastahili pongezi kwa kulifikisha taifa sehemu nzuri ambayo huduma zote ziko karibu. Kabla ya uhuru mkoa huu hatukuwa na shule hata moja, bali shule moja ya wamisionari na hospitali moja,” anasimulia Mwampashe.

Anasema anafurahishwa na maendeleo yaliyopo katika mpaka wa Tunduma na Zambia ambao unategemewa na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) . Anasema umepiga hatua kubwa na kuingiza mapato kwa Mkoa wa Songwe na taifa kwa ujumla tofauti na kipindi cha ukoloni.

Mwampashe anawataka vijana na Watanzania kudumisha amani, ushirikiano na kuacha kugombania madaraka kwa kutumia nguvu bali kutanguliza maslahi ya taifa siku zote ili miaka 60 ijayo taifa lipige hatua zaidi. 

Kwa upande wake, Asha Myombe ambaye alishiriki mikutano ya Mwalimu Nyerere ya kudai Uhuru na kuhudumu ngazi mbalimbali za uongozi kwenye chama na serikali, anasema viongozi na waasisi wa Tanzania walifanikiwa kutengeneza misingi mizuri ambayo imefanikisha kuzaliwa Mkoa wa Songwe. 

“Nafurahi sana kushuhudia mambo mengi yaliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere namna ambavyo yanatekelezwa kwa vitendo na viongozi wetu awamu zote zilizopita na awamu ya sita chini ya Rais Samia,” anasema Myombe na kuongeza:

“Tulikuwa tunatengeneza barabara kwa majembe ya mkono, shule tulijenga wenyewe, kazi nyingi tulifanya kwa wakoloni tena tulilipwa ujira mdogo ambao haukukidhi mahitaji. Sasa tupo huru serikali inafanya kazi kubwa kutuletea maendeleo na kutusogezea huduma mfano kuanzishwa kwa mkoa wetu kumetusaidia sana sisi wananchi wa Songwe.”

Nyerere kijijini Igamba

Myombe anasema: “Ilikuwa mwanzoni mwa mwaka 1960 mimi nikiwa darasa la sita wananchi walisafiri umbali mrefu kutoka maeneo mbalimbali ya Mbozi (hivi sasa Mkoa wa Songwe) kwa lengo la kumsikiliza Mwalimu Nyerere aliyekuja kutueleza na kutusihi kumuunga mkono katika harakati za kudai uhuru.

“Jambo ambalo sitalisahau siku ile ni namna ambavyo wananchi wa Mbozi walivyofurika licha ya miundombinu ya barabara kuwa migumu na vyombo vya usafiri kutokuwepo kabisa. Wananchi waliobahatika kumsalimia Nyerere kwa mkono walirudi nyumbani kwa furaha huku wakidai hawatanawa mikono kwa madai kuwa wangetoa baraka za Mwalimu Nyerere.”

Anasimulia kuwa miti iliyotengenezea jukwaa la kuhutubia mkutano wa Nyerere iliyoguswa na kushikwa na Mwalimu, wananchi waliing’ang’ania na kubandua maganda yake na kwenda kuichanganya na mboga kwa madai kuwa watazaa watoto wenye akili kama Nyerere. 

Anasema mkoa umesaidia kuongezeka kwa barabara za lami na changarawe, vituo vya afya, kuboreshwa kwa elimu za msingi, chekechea na sekondari. Anasema watoto wengi wamepata elimu kirahisi huku vifo vya mama na mtoto vikipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuboreshwa huduma za afya.

Magreth Nyilenda ambaye ni miongoni mwa walioshuhudia harakati za uhuru na mwaka 1963 baada ya uhuru aliajiriwa kama Bibi Maendeleo katika Wilaya ya Mbozi na baadaye kuwa Diwani wa Kuteuliwa, anasema Watanzania wanapaswa kujivunia kutokana na maendeleo yaliyopatikana katika afya, elimu, barabara, uchumi, kilimo, biashara na utawala bora.

Anasema kulikuwa na ubaguzi mkubwa katika huduma zote muhimu za kijamii kabla ya uhuru. Anakumbuka kulikuwa na shule za Wazungu na za Waafrika. 

Kwa upande wa usafiri, anasema kulikuwa na mabasi ya Railway na treni ambapo Waafrika walipanda daraja la tatu huku Wazungu wakipanda daraja la kwanza na la pili kupandwa na Wahindi.

Nyilenda anasema anafurahishwa namna Mkoa wa Songwe ulivyoanzishwa na kusaidia mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, elimu, miundombinu na maendeleo kwa kasi.

“Makao makuu kuhamishiwa Dodoma pia ni jambo ambalo limenifurahisha sana, mawazo ya Nyerere na waasisi wa taifa hili yanatekelezwa kwa vitendo na viongozi wetu," anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba akizindua sherehe za miaka 60 ya Uhuru hivi karibuni wilayani Momba, anasema licha ya  Mkoa wa Songwe kutimiza miaka mitano tangu kuanzishwa, wanajivunia kushika nafasi ya tatu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula ukichuana kwa karibu na mikoa mikongwe ya Ruvuma na Rukwa kama ambavyo takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/9bc71180b5904597a0abd2f4dc74b7be.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Baraka Messa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi