loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali yaagiza anayeingia, kutoka viwanja vya ndege akaguliwe

Serikali yaagiza anayeingia, kutoka viwanja vya ndege akaguliwe

USAFIRI wa anga duniani umekuwa na changamoto kutokana na uwepo wa vitisho au vitendo vya kigaidi hasa baada ya tukio la Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani.

Katika tukio hili, ndege za abiria zilitumika kama silaha kutungua majengo pacha ya biashara na Jengo la Wizara ya Ulinzi.

Kutokana na umuhimu huo wa usalama katika usafiri wa anga, Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameagiza kila mtu anayeingia na kutoka katika viwanja vya ndege hapa nchini lazima akaguliwe.

Anasema agizo hili la kukaguliwa pia linawahusu watumishi wote na wakuu wa taasisi zinazofanya kazi kwenye viwanja vya ndege ili kuhakikisha maisha ya wasafiri wa anga na mali zao wanakuwa salama.

Profesa Mbarawa ametoa maagizo hayo hivi karibuni wakati akizindua Mwaka wa Utamaduni wa Kiusalama wa Usafiri wa Anga kwenye Makao Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Dar es Salaam.

Kaulimbiu ya mwaka huu wa utamaduni wa kiusalama wa usafiri wa anga inasema “Usalama wa Usafiri wa Anga ni Jukumu letu sote: Timiza Wajibu.”

Profesa Mbarawa anaonesha dhamira ya serikali ya CCM kulinda usalama wa wananchi na nchi na anasema kuwa suala la usafiri wa anga duniani limekuwa na changamoto kutokana na uwepo wa vitisho au vitendo vya kigaidi.

Anasema vitisho au vitendo vya kigaidi vimesababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha ya wasafiri wa ndege na wasiosafiri, uharibifu wa mali na miundombinu, kuzorota kwa shughuli za utalii na biashara kote duniani.

Kutokana na changamoto hii, anasema mbinu za kukabiliana nayo zinapaswa kuwa endelevu na shirikishi ili ziwe na tija zaidi.

“Naagiza taasisi zote zinazotoa huduma za usafiri wa anga nchini ikiwemo TCAA, mashirika ya ndege, waendeshaji wa viwanja vya ndege, mawakala wa huduma za ndege katika viwanja vya ndege, watoa huduma za vyakula kwenye ndege na watoa huduma nyingine kwenye viwanja vya ndege kuwa na mikakati endelevu ya kuboresha na kuendeleza usalama wa usafiri wa anga kwenye viwanja vyetu,” anasema Profesa Mbarawa.

Anaongeza: “Hapa naongea kwa masikitiko makubwa kwani nina taarifa ya baadhi ya watumishi wakiwemo wakuu kwenye baadhi ya taasisi zinazofanya kazi kwenye viwanja vya ndege wakikaidi kutekeleza matakwa ya kiusalama kwa baadhi yao kudharau taratibu za ukaguzi, hili jambo si sahihi, sisi viongozi tunawajibu mkubwa wa kusimamia sheria. Usalama wa viwanja hivi upo mikononi mwetu, tukitimiza kila mtu wajibu wake, viwanja vyetu vya ndege vitakuwa salama na kila mgeni atapenda avitumie.”

Kwa umuhimu huo, amewataka wakuu wa taasisi hizo kuhakikisha kila mtumishi aliyeko au anayefanya kazi kwenye viwanja vya ndege, mashirika ya ndege na watoa huduma zote wanatii sheria na kanuni za viwanja vya ndege.

Pia ameiagiza Kamati ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri wa Anga nchini kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa utamaduni wa usalama kwa kupata taarifa ya utekelezaji kutoka kwa wadau katika kila kikao cha kamati kinapofanyika na iwe ajenda muhimu na ya kudumu.

Profesa Mbarawa anasema mwaka huu ni mwaka muhimu katika historia kwa sababu ni mwaka wa kumbukizi ya miaka 20 wa tukio la utekaji nyara wa ndege nne za abiria ambazo magaidi walizitumia kama silaha kwa kuyagonga majengo mawili pacha ya kibiashara na Jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi nchini Marekani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCAA, Profesa Longinus Rutasitara, anabainisha kuwa mwaka wa utamaduni wa usafiri wa anga umetokana na azimio la 40 kwenye kikao cha 11 cha Mkutano wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) ambao uliazimia kuwa ICAO kupitia nchi wanachama iendelee kukuza uelewa wa utamaduni wa usalama wa anga kwa jamii.

Profesa Rutasitara anasema miongoni mwa mambo yanayotakiwa kufanyika katika mwaka huu wa utamaduni wa usalama wa usafiri wa anga kama kipaumbele ni pamoja na kampeni ya uelewa wa utamaduni wa kiusalama utakaozisaidia taasisi kitaifa, kikanda na kidunia kukuza uelewa wa utamaduni wa usalama wa anga.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, anasema kabla ya tukio la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani, kulikuwa na viambatisho 16 vya kiufundi kuhusu masuala ya usafiri wa anga katika sheria ya kimataifa ambayo ni Mkataba wa Chicago wa mwaka 1944. 

Anasema viambatisho hivyo vimekuwa vikiongezeka kutokana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya usafiri wa anga.

Johari anabainisha kuwa baada ya tukio la Septemba 11, 2001, Baraza la Shirika la Usafiri wa Anga Duniani katika kikao chake cha Oktoba 22, 2001 kilipitisha azimio namba 33 na kuanza kazi rasmi mwaka 2002 kwamba waje na mikakati ya kuwa na mifumo ya kuimarisha usalama na kuanzishwa kwa kiambatisha kipya namba 17 kinachohusu usalama wa usafiri wa anga.

Anasema kiambatisho hiki namba 17 kinaitaka Tanzania kama nchi iliyoridhia Mkataba wa Chicago, kuwa na sheria ndogo za ndani zitakazo kuwa zinasimamia masuala ya usalama pamoja na kuwa Kamati ya Kitaifa itakayokuwa inasimamia masuala ya usalama.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/039234a536d8c6ba4575717af16d7a0f.JPG

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi