loader
Dk Mwinyi: Tumezingatia maslahi ya nchi 

Dk Mwinyi: Tumezingatia maslahi ya nchi 

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema mikataba minne iliyosainiwa jana kwa ajili ya kuboresha huduma katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, imezingatia maslahi ya kiuchumi ya Zanzibar.

Dk Mwinyi alisema jana Ikulu Zanzibar kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilitumia muda mrefu kutafuta kampuni zenye sifa za kutoa huduma katika Jengo la Tatu la Abiria katika uwanja huo.

Alisema kazi hiyo haikuwa rahisi na wakati mwingine walilazimika kurudia michakato ili kulinda maslahi ya nchi.

“Serikali imeamua kutafuta makampuni yenye sifa duniani kuja kushirikiana nasi katika uendeshaji wa kiwanja chetu cha ndege kwa madhumuni ya kutoa huduma bora na za kiwango cha kimataifa. Lengo letu ni kwamba huduma hapa Zanzibar katika uwanja wetu wa ndege ziwe za kiwango cha kimataifa,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema serikali imewekeza Dola za Marekani milioni 128 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria kwa kuimarisha miundombinu ya barabara nje ya kiwanja, imejenga uzio na maegesho ya magari.

Aliipongeza Kamati ya Majadiliano ya Serikali kwa kazi waliyofanya hadi kuwezesha kusainiwa kwa mikataba hiyo yenye maslahi kwa nchi.

Alizitaka taasisi za serikali zitoe ushirikiano kwa kampuni zilizopewa jukumu la kutoa huduma kwenye jengo hilo.

 

Dk Mwinyi pia alizitaka taasisi za fedha zikiwemo benki, idara ya Uhamiaji na idara za afya zinazotoa huduma za chanjo kwa watalii wanaoingia nchini ziongeze kasi ya kutoa huduma na kuepuka urasimu.

Alisema mikataba iliyosainiwa jana inahusu utoaji wa huduma za abiria na mizigo, huduma za uendeshaji uwanja wa ndege, huduma za kumbi za wageni uwanjani hapo na huduma za maduka na migahawa.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Rahma Kassim Ali alisema serikali imeamua kutafuta kampuni yenye sifa za kimataifa katika utoaji wa huduma ili ziende katika misingi ya kimataifa zaidi.

Jumla ya mikataba minne imetiwa saini ikiwemo wa uendeshaji wa viwanja vya ndege pamoja na jengo la Abiria la Abeid Amani Karume, huduma za mizigo na migahawa.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Dubai National Air (DNATA), Steve Allen alisema wamejipanga kufanya kazi kwa ufanisi utakaozingatia ubora wa huduma katika viwanja vya ndege vya kimataifa duniani kote.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Amour Hamil alisema utiaji saini wa mikataba hiyo inamaanisha kuwa utoaji huduma zote katika Jengo la Tatu la Abiria kwenye uwanja huo utakuwa chini ya Kampuni ya DNATA ya Dubai.

Mwakilishi wa Kampuni ya Emirate Leasure Retail (ELR), Christian Laugier alisema wamejipanga kutoa huduma inazokwenda na hadhi ya kimataifa.

Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Khalifa Abdulrahman Almarzouqi alisema amefurahishwa na kuingia kwa mikataba hiyo kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi katika viwanja vikubwa vya kimataifa vya ndege.

Jengo la Tatu la Abiria limejengwa na Kampuni ya BCG ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China huku eneo hilo likiwa na ukubwa wa eneo la mita za mraba 25,000 likiwa na uwezo wa kupokea wageni wapatao milioni 1.6 kwa mwaka.

Kampuni ya DNATA inatarajia kusimamia safari 4,000 kwa mwaka za usafiri wa anga kutoka Zanzibar katika Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amani Karume.

Aidha, itawekeza katika kituo cha kisasa cha mizigo katika uwanja huo na kusaidia biashara ndani ya uwanja kwa kuzingatia viwango vya kimataifa zaidi. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/37592b4b9f8c0a1a0b707725c65b7d60.JPG

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Michael ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi