loader
Majaliwa atoa maagizo sita kukuza ajira

Majaliwa atoa maagizo sita kukuza ajira

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo sita kwa wizara na taasisi za serikali ili kukabili changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana Zanzibar wakati akizindua Matokeo ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi Tanzania uliofanywa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2020/2021.

Alisema utafiti huo una viashiria vingi muhimu vinavyohusiana na masuala ya ajira nchini, hivyo serikali itaendelea kuchambua viashiria vyote na kuhakikisha inakuwa na ripoti ya kina itakayowezesha maboresho mbalimbali ya kukuza ajira na uchumi nchini.

Kutokana na hilo, aliziagiza wizara zenye dhamana ya ukuzaji ajira na zinazohusika na kutoa fursa kwa vijana wa makundi yote, zihakikishe zinaandaa programu na mikakati bora ya ukuzaji ajira ikiwemo kuhamasisha wadau nchini kushiriki katika utekelezaji wake.

Pia alizitaka ofisi na wizara zenye dhamana ya uwekezaji na biashara kuhakikisha zinashirikiana na wadau wengine hasa sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa vikwazo, urasimu wa kufanya biashara na uwekezaji.

Alisema hilo likifanyika litakuza uwekezaji kwa kasi na kutoa fursa ya kuanzishwa kwa viwanda vipya, maeneo mapya kibiashara, fursa mpya za biashara zinazoweza kutumika na nguvu kazi iliyopo katika kufanya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira.

“Wizara na taasisi zote za elimu, hakikisheni mnasimamia utoaji wa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira na hili linatokana pia na kusisitiza mchakato wa mapitio ya mitaala yetu ya elimu inayoendelea kote nchini ili uharakishwe, ujadiliwe, uandaliwe mpango na tupate mitaala inayolenga kuongeza fursa ya watu kujiajiri wenyewe,” aliagiza Waziri Mkuu.

Majaliwa pia alizitaka Wizara za Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri na kusimamia taasisi za fedha na benki ili kuwezesha kutoa mikopo yenye masharti na riba nafuu na ikiwezekana kusiwe na riba kabisa ili kuwezesha watu kufanya biashara na uwekezaji.

Kwa upande wa halmashauri za wilaya, manispaa, miji na majiji, alizitaka zihakikishe kwenye mipango ya bajeti inayowekwa kwenye kila mwaka wa fedha, waweke kipaumbele katika kutenga fedha za kutoa mikopo yenye masharti nafuu kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Tawala za Mikoa na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa, zinatakiwa kutenga maeneo ya kufanyia shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yao, kuyawekea miundombinu zikiwemo barabara, umeme, maji, vyoo na huduma nyingine muhimu ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhakika na kuwawezesha wajasiriamali kujipatia kipato kupitia maeneo hayo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema wamejipanga kutengeneza mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya kukuza taarifa za soko la ajira ndani na nje ya nchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3750678b785c857fa7c2fb09a0170c0f.jpeg

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Michael ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi