loader
Naibu Waziri aipa neno Ofisi ya Mwanasheria Mkuu

Naibu Waziri aipa neno Ofisi ya Mwanasheria Mkuu

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Geoffrey Pinda amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutambua uzito na dhamana ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika uendeshaji wa serikali, huku akiitaka kuandaa mikataba yenye tija kwa taifa.

Aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema kwa mujibu wa majukumu ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepewa kikatiba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni nguzo na mhimili wa uendeshaji wa serikali na kwamba ufanisi wa serikali kwenye masuala ya kisheria unawategemea watumishi wa ofisi hiyo.

“Kwa muktadha huu, ni vema mtambue kuwa mmepewa majukumu nyeti, na mmebeba dhamana kubwa ya kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake, na nyinyi ndiyo taswira ya Taifa letu kwenye masuala ya utawala na sheria,” alisisitiza Naibu Waziri Pinda.  

Aidha, alitoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu na kwa maslahi mapana ya nchi.

“Kwa kufanya hivyo mtaiwezesha serikali kupata ushindi kwenye kesi nyingi na kupunguza migogoro ya kisheria baina ya serikali na wabia,” alibainisha Naibu Waziri.

Katika baraza hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi, Naibu Waziri pia ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuendeleza juhudi za serikali za kuondokana na sheria zenye mianya ya rushwa kwa kuandaa mikataba yenye tija na inayozingatia maslahi ya taifa.

Vile vile alisisitiza watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuvitambua vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita na jinsi gani vinatekelezwa kwa kuzingatia majukumu ya ofisi.

Pamoja na kusisitiza matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika utoaji haki, pia alisisitiza umuhimu kwa watumishi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kiutumishi na kiutendaji ikiwamo kuweka mfumo wa kufuatilia utendaji wa wanasheria wa serikali na wa mawakili kupata uzoefu wa kazi mahakamani.

Akimkaribisha Naibu Waziri kufungua mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi alisema ofisi yake haitamvumilia mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa.

“Katika eneo hili la uadilifu, niwasihi watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Muu wa Serikali mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu ya kazi kwa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma, Sheria na Kanuni. Mla rushwa hatavumiliwa hata kidogo,” alionya Dk Feleshi.

Kuhusu idadi ya watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema kwa mujibu wa muundo wa ofisi, inahitaji kuwa na watumishi 477 ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika mikoa yote 26, lakini waliopo ni 121, kati ya hao mawakili wa serikali ni 54 na watumishi wa kada nyingine ni 67, idadi aliyosema ni ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji ya mawakili wa serikali 241 wanaohitajika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6efd95d961c84f04993bad3bb08697bd.jpeg

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Michael ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Mwanza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi