loader
Bei za saruji, nondo, mabati kudhibitiwa

Bei za saruji, nondo, mabati kudhibitiwa

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amesema ongezeko la bei ya saruji si halali na ametangaza mikakati kudhibiti kupanda bei ya bidhaa hiyo, nondo na mabati. 

 

Profesa Mkumbo alitangaza mikakati hiyo jana Dodoma wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za vifaa vya ujenzi kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba mwaka huu.

 

"Wizara imekuwa ikifanya tathimini ya mara kwa mara ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za bidhaa muhimu nchini ikiwemo vyakula, sukari, mafuta ya kula na vifaa vya ujenzi hususani saruji, mabati na nondo,"alisema.

 

Profesa Mkumbo alisema tayari tathmini imefanyika katika mikoa tisa inayotumia zaidi bidhaa hizo ukiwemo wa Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Ruvuma.

 

Alitaja mikakati ya kudhibiti bei hizo kuwa ni pamoja na utaratibu wa wizara wa kutoa taarifa ya wastani wa bei kila mwezi kwa mikoa yote.

 

"Hatua hii itawapa walaji au watumiaji wa bidhaa uelewa wa kutosha kuhusu uhalisia wa bei za bidhaa hizo na hivyo kuwawezesha kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe kisheria”alisema Profesa Mkumbo.

 

Alitaja hatua nyingine kuwa ni Tume ya Ushindani (FCC) kuendelea kufuatilia mwenendo wa upandaji bei na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaokiuka sheria.

 

Alisema pia sheria na kanuni zitarejebishwa ili kuruhusu kuingizwa kwa urahisi zaidi malighafi zinazohitajika katika uzalishaji wa bidhaa za vyuma ikiwemo kuruhusu kuingizwa kwa vyuma chakavu kutoka nje kwa utaratibu utakaohakikisha inapatikana bila kuathiri mazingira ya nchi.

 

Profesa Mkumbo alisema utawekwa mpango wa muda mrefu wa serikali kutekeleza miradi kielelezo itakayowezesha kuzalisha chuma kwa wingi kwa ajili ya viwanda vya ndani na kuuza nje ya nchi.

 

Pia Serikali imepiga marufuku uuzaji nje ya nchi shaba chakavu inayotumika katika uzalishaji wa bidhaa za vyuma nchini.

 

Profesa Mkumbo alisema nchi ina viwanda tisa vinavyozalisha saruji vyenye uwezo wa kuzalisha tani 9,080,000 kwa mwaka na tathmini ikionesha kuwa katika mikoa hiyo bei za saruji zimepanda kwa wastani wa Sh 1,000.

 

Alitoa mfano wa Mkoa wa Mwanza kuwa bei imeongezeka kutoka Sh 19,000 kwa mfuko kwa Septemba hadi kufikia Sh 20,000 kwa Novemba mwaka huu.

 

"Kwa Mkoa wa Dar es Salaam bei imepanda kutoka shilingi 14,000 kwa mwezi Septemba hadi shilingi 15,000 Novemba wakati Ruvuma bei ikishuka kwa asilimia 15 kutoka Sh 17,000 hadi 14,500 kwa kipindi hicho,"alisema Profesa Mkumbo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ccfb2c4cd2b7f0a86e1bf21115f4781c.jpeg

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Michael ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi