loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mchengerwa awapa maneno mazito vigogo Takukuru

Mchengerwa awapa maneno mazito vigogo Takukuru

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutenda haki na kujiepusha kuonea watu kwa tuhuma za uongo.

Aidha, ameitaka taasisi hiyo ilinde maslahi ya taifa na izuie mianya ya wizi na rushwa kwenye miradi. Amesema fursa zilizofunguliwa za kiuchumi ikiwamo miradi ya maendeleo si njia ya kuneemesha watu binafsi kupitia mikopo na mikataba yenye madhara kwa nchi.

Mchengerwa alisema hayo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa viongozi wa Takukuru, mjini Dodoma. “Tutafakari, Tanzania mikataba na mikopo yote je, ndani kwa ndani hakuna mifereji ya kutorokea maslahi ya taifa? Mikopo yote na mikataba yote je, ina uadilifu wa yale yanayotangazwa ya kuondoa umaskini ama kuondoa uduni na udumavu kwa mambo mtambuka ya maslahi ya taifa?” alisema.

Alisema Takukuru ina wajibu mkubwa wa kuiwezesha nchi kushinda vita vya maendeleo na akaitaka iongeze ujuzi, maarifa na weledi. “Tegemeo la wananchi ni viongozi waliowachagua na viongozi walioteuliwa, viongozi wa karne ya leo hatutegemei kufikiri katika maisha yao na wengi wao wametekwa na hofu ya rushwa na ubadhirifu mioyoni mwao.

Wengi wao wamekuwa wazembe wakifikiria maisha bila Watanzania waliochagua, viongozi wengi wa majiji makubwa wametekwa mifukoni mwa matajiri wadhulumaji na watoa rushwa, waonevu, wanyonyaji wasiolitakia mema taifa lao,” alisema Mchengerwa.

Waziri huyo alikumbusha kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni Aprili 22, mwaka huu aliposema: “Hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wezi wa mali za umma, tutaendeleza juhudi za kupambana na rushwa katika utumishi wa umma...” Alisema Takukuru iliundwa ili kujenga nguzo kuu za serikali za kuinua ufanisi wa uwajibikaji na watumishi wa umma wazingatie miiko na maadili.

“Kitaifa taasisi hii ni nanga ya taifa letu kwa usalama wa tija ya kutoa wajibu wa uwazi na ukweli wa kuchangia utawala bora hususani katika kuchuja na kuondoa kasoro zioteshazo maovu yanayoambatana na yaliyofichika katika kurasa za mikataba hasi,” alisema.

Mchengerwa aliitaka taasisi hiyo iache tabia ya kuamini shutuma kwa haraka kwa kupokea taarifa za kutoka upande mmoja, kwani kufanya hivyo ni kuingiza ubabaishaji na kudhalilisha weledi. “Viongozi wa Takukuru msikimbie changamoto za mitego ya kuletewa mambo ya ukweli na bandia, hivyo mkiyabaini siyo aibu kufuta shutuma. Epukeni dhambi za kutafuta uongo mtamu wa kuthaminisha mambo ya kutengenezwa na ukweli bandia wa kuumiza utu na ubinadamu wa watu wanaobambikiziwa kasoro za makosa potofu,” alisema.

Aliwataka wafanyakazii wa taasisi hiyo watambue kuwa wao ni kioo cha jamii na walinzi wa haki za jamii na za taifa. “Kwa hiyo sasa mnapaswa kuwa na matendo yenye usafi wa moyo na muwe na nafasi zenye taratibu za kuitwa ni za watu wenye sifa ya watenda haki.

Kumbukeni, watu na haki zao ni pete na kidole visivyoachana,” alisema. Mkutano huo unajumuisha viongozi wakuu 60 wa Takukuru akiwemo Mkurugenzi Mkuu, Naibu Mkurugenzi Mkuu, wakurugenzi, wakuu wa vitengo, wakurugenzi wasaidizi na wakuu wa taasisi hiyo wa mikoa.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/9de0ea750772aef5d6d7183e74e67495.jpeg

SERIKALI imepanga kujenga ...

foto
Mwandishi: Na Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi