loader
Tuhakikishe wanafunzi wote wa kidato cha kwanza wanaanza masomo

Tuhakikishe wanafunzi wote wa kidato cha kwanza wanaanza masomo

JUZI serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, ilitangaza uchaguzi kwa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2022.

Ummy aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa wanafunzi 907,802 waliofaulu wakiwemo wasichana 467,967 na wavulana 439,835 ambao ni sawa na asilimia 81.97 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu, wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.

Alisema kwa mwaka 2022, kumekuwa na ongezeko la wanafunzi 73,932 sawa na asilimia 8.87 ya wanafunzi waliofaulu ikilinganishwa na mwaka jana ambao wanafunzi 833,872 walifaulu na kupata sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza. Alibainisha kuwa wanafunzi wote 907,802 waliofaulu mtihani wa darasa la saba wataanza masomo siku moja.

Hizi ni habari njema kwani kwa mara ya kwanza wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wamechaguliwa kwenda kidato cha kwanza.

Tunaamini kwamba wanafunzi wote hawa waliochaguliwa wataripoti shuleni kama walivyopangiwa ili kuendelea na elimu ya sekondari wakifahamu kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo. Aidha, tunaamini kama alivyoeleza Waziri wa Tamisemi wanafunzi wote hawa wataanza shule siku moja ya Januari 17, mwakani, wakati muhula mpya wa masomo utakapoanza kwa shule zote za umma nchini.

Tunasema hivyo kwa sababu tayari serikali imetoa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa yatakayochukua wanafunzi hawa wapya wa kidato cha kwanza. Kwa mujibu wa Waziri Ummy, hatua ya serikali ya kutoa Sh bilioni 240 kujenga madarasa 12,000 nchi nzima, imeongeza nafasi kutoka nafasi 430,604 zinazoachwa na wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne mwaka 2021 hadi kufikia nafasi 1,030,604 pindi madarasa yanayojengwa yakikamilika yatakayoongeza nafasi 600,000.

Kwa hiyo, hatutarajii kusikia sehemu yoyote ile nchini kwamba wapo wanafunzi ambao hawataingia darasani Januari 17, 2022, kwa sababu majengo au madarasa yatakuwa hayajakamilika.

Tunasema hivyo kwa sababu fedha zimetolewa na serikali tena kwa uwazi, kwa karibu kila halmashauri nchini kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo ambayo yanatakiwa kukamilika Desemba 15, mwaka huu. Tunawaomba waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa madarasa haya kuyakamilisha kama walivyoagizwa na Tamisemi, ili kusiwepo na sababu za wanafunzi kushindwa kuripoti shuleni masomo yatakapoanza.

Tunawatakia kila la heri katika maandalizi ya kuanza kwa kidato cha kwanza kwa wanafunzi hawa waliochaguliwa, pamoja na shule katika kuwapokea wanafunzi.

Serikali imetimiza majukumu yake kwa kiasi kikubwa na sasa ni jukumu la wasimamizi nao kutimiza majukumu yao ili watoto wa Kitanzania wasome katika mazingira mazuri, wapatikane wahitimu wenye uwezo wa kushindana kimataifa.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/941130bde4585675a3feae0918682158.jpeg

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ...

foto
Mwandishi: NA MWANDISHI WETU

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi