loader
Serikali yaonya halmashauri zinazosuasua miradi ya afya, elimu

Serikali yaonya halmashauri zinazosuasua miradi ya afya, elimu

HALMASHAURI zote nchini zilizopokea fedha za miradi ya ujenzi wa madarasa na vituo vya afya, zimetakiwa kuhakikisha kwamba zimekabidhi kazi hizo zikiwa zimekamilika ifikapo Desemba 16, mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wakati akikagua utekelezaji wa miradi hiyo wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.

Naibu Waziri huyo akizungumza baada ya kutembelea miradi kadhaa ya elimu na afya wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi, alisema ofisi yake imebaini kuna kasi ndogo ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na lazima wakurugenzi kuwajibika katika hilo.

Dk Dudange alisisitiza kuwa Mkoa wa Lindi bado uko nyuma katika ukamilishaji wa miradi hivyo amewataka viongozi na watendaji kusimamia miradi hiyo usiku na mchana huku wakizingatia ubora na thamani ya fedha iliyotolewa na kutumika.

 “Nawataka wakurugenzi wa halmashauri chini ya usimamizi wa wakuu wa wilaya kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi ukamilike kwa wakati,” alisema. 

Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Dk Dudange ya utekelezaji wa miradi hiyo Wilaya ya Kilwa, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga alisema Kilwa imepokea takribani Sh bilioni 2 kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na madarasa katika shule za sekondari na shule shikizi.

Ndemanga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainabu Kawawa alisema kutokana na fedha hizo tayari ujenzi wa miradi hiyo unaendelea na kuahidi miradi hiyo itakamilika kwa wakati sahihi pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali.

Shaibu alisema Wilaya ya Kilwa kupitia fedha zilizotolewa za Covid-19, EP4R, mfuko wa elimu pamoja na mapato ya ndani unatarajiwa kukamilisha ujenzi wa madarasa 74 ya shule za sekondari na madarasa 29 ya shule shikizi ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Mandawa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/28ed87d71af244f2fec99d9e73a291f0.jpg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Kilwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi