loader
Barabara vijijini zafungua fursa za uchumi kwa wananchi

Barabara vijijini zafungua fursa za uchumi kwa wananchi

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza debe moja la mahindi kwa Sh 800, huwezi kufikiria kuuza gunia utalibebaje na kupita wapi?” ni kauli ya Jonathan Rugalama, mkazi wa Kijiji cha Kyamihorwa, Kata ya Kasharunga, wilayani Muleba, mkoani Kagera, kabla ya hatua ya serikali ya kukifungua kijiji hicho kwa barabara.

Rugalama anasema huwa wamekuwa wakilazimika kuamka alfajiri na kutembea umbali mrefu hadi kufika barabarani kuuza debe moja la mahindi ili wajikimu lakini mwendo huo unamfanya mtu achoke na kujaa matope mwili mzima kama ni nyakati za mvua kwa sababu tangu wazaliwe hawajawahi kuona barabara kijijini kwao.

Uwepo wa barabara zinazounganisha vijiji, vitongoji, mitaa na eneo moja na lingine ni njia moja ya kurahisisha mawasiliano, huduma za jamii lakini pia kukuza kipato cha mtu mmoja na taifa zima.

Tangu nchi ipate uhuru Kijiji cha Kyamihorwa hakijawahi kupata barabaraba na hulazimika kutembea umbali wa kilometa 20 kuifikia hivyo kwao imekuwa ni ngumu kufanikiwa kiuchumi kwani wanazalisha mazao mengi lakini uwezekano wa kuuza ni mdogo sana.

Hali hii imechangia kuzorota kwa upatikanaji wa huduma za kijamii kama afya, elimu kwa watoto na ushiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii.

Adella Shamba (58) mkazi wa kijiji hicho anasema licha ya ugumu wa maisha uliopo katika kukosa riziki, pia wanapata shida kubwa kwa wanawake wanaotaka kujifungua kwani umbali wa kilipo kituo cha afya ni kilometa 20. Anasema pia kusafirisha wagonjwa imekuwa na tatizo kubwa kwao.

Anasema kuna mambo muhimu mengine ambayo yalikuwa yakiwakosesha fursa kabisa mfano ushiriki wa kituo cha karibu cha kupiga kura, jinsi ya kuripoti uhalifu kwani kulikua na matukio ya ujangili katika Hifadhi ya Burigi, wilayani Chato kwa kutokuwa na kituo cha polisi.

Anasema akitaka kununua bidhaa ambayo haipo kijijini hapo hawezi kuipata kwa wakati, hawezi kuuza mazao yake kwa bei iliyopo sokoni lakini pia hakuweza kuhudhuria kliniki vizuri alipojifungua watoto wake na hawajaenda shule kutokana na umbali mrefu.

Hata hivyo, anakiri kuwa faraja imetua katika kijiji hicho baada ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuchonga barabara nzuri na kuweka changarawe katika kijiji hicho na kufanya wananchi kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha inakamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Charles Mbuge akiambatana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye wanatembelea maeneo mbalimbali ya Kagera ambapo wananchi wamefunguliwa barabara ikiwemo Kijiji cha Kyamihorwa na kupokelewa kwa furaha.

Wananchi wanaonesha kutoamini kama sasa barabara inafunguliwa katika kijiji hicho na kuwaunganisha na jamii nyingine.

Diwani wa Kasharunga, Theobard Marco, baada ya kupokea ugeni wa mkuu wa mkoa anasema uwepo wa barabara katika kijiji hicho unasaidia Tarafa ya Kimwani yenye zaidi ya kata 10 na visiwa zaidi ya vitano ambavyo wananchi wake walizunguka umbali mrefu hasa walipopata rufaa ya kujifungua au ugonjwa mkubwa kwenda katika Kituo cha Afya cha Kimea.

Marco anasema kuwa mwaka 2020 aliogopa kwenda katika kijiji hicho kuomba kura kwa kuhofia kuwa huenda wananchi watamfukuza na endapo barabara isipofunguliwa huenda akakosa ujasiri wa kuomba tena ridhaa ya kuwaongoza wananchi katika kipindi kijacho lakini kwa sasa hakuna kikwazo kwani serikali imefungua barabara tayari na wananchi watafanya shughuli za kiuchumi.

“Siwezi kusimulia na kumaliza visa vibaya ambavyo vimewahi kutokea katika kijiji hiki kutokana na kukosa barabara lakini kwa sasa barabara imepatikana, badala ya kutembea na mguu kilometa 20 sasa tutatumia magari na barabara yetu inayotuunganisha kote kwa kilometa tisa.

“Tutauza, tutanunua, tunasema asante Rais wetu Samia (Suluhu Hassan) kwa kutuona, asante Tarura kwa kupata watendaji wenye uadilifu mkubwa na maono ya kuona sasa na sisi tunafaa kutumia barabara,” anasema Marco.

Kutokana na serikali kujenga barabara katika kijiji hicho wananchi wana muahidi Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Tobias Nguvila kufanya kazi kwa bidii, kuendelea kuzalisha mazao kwa wingi ili kujipatia kipato, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kupeleka watoto shule na kliniki.

Meneja wa Tarura wilayani Muleba, Dativa Semforiani anasema barabara hiyo itagharimu zaidi ya Sh milioni 400 na inatarajia kukamilika Desemba mwaka huu kama sehemu ya barabara zinazofungua uchumi wa wananchi wanaoishi katika kijiji hicho na kata zaidi ya 10 zinazowazunguka.

Anasema lengo la kujenga hiyo barabara ni kurahisisha mawasiliano kwa wananchi hao ambao wameteseka miaka mingi, kuwasogezea karibu huduma za jamii.

Baada ya ukaguzi wa barabara ya Kyamihorwa, Kasharunga, Kimeya  mkuu huyo wa mkoa na mwenyekiti wa CCM walifika katika barabara  ya Katoro-Kyamuraile-Kashaba katika Halmashauri ya Bukoba ambayo mawasiliano yalikatika baada ya kujaa maji kwa kipindi cha miaka minne sasa.

Aidha, barabara hiyo iko mbioni kukamilika na gharama yake ni zaidi ya Sh milioni 400. Wananchi wanafurahia kwani wamevuka kwa mtumbwi kwa miaka hiyo minne na kwa gharama ya Sh 2,000 kwa mtu kila anapovuka.

Barabara nyingine iliyofunguliwa ni ya Kishanda-Byanturege iliyoko Kyerwa ambayo inaunganisha kata tano na miaka kadhaa wanafunzi wameshindwa kusoma shule ya karibu kutokana na barabara hiyo kujaa maji.

Ujenzi wa barabara hiyo utawasaidia wananchi kufika Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa ambayo imejengwa hivi karibuni na kuwafungulia shughuli za uchumi.

Wananchi wanapongeza hatua ya serikali kwa matengenezo ya barabara hiyo kwani ilikuwa ngumu hata kusafiri, kupata huduma muhimu na vijiji ambavyo vilijitenga na barabara vimechelewa kupata maendeleo.

Meneja wa Tarura mkoani Kagera, Avith Theodory anasema kuwa mwaka 2021/2022 bajeti ya barabara za vijijini na mijini iliyotengwa ni Sh bilioni 22.3 ikiwa ni mara mbili zaidi ya bajeti ya mwaka 2020/2021 ya Sh bilioni 9.3.

Theodory anasema wananchi wategemee kuona mabadiliko na barabara imara huku vijiji ambavyo havijapata barabara vitafunguliwa kwani serikali imetenga bajeti kubwa ya kuimarisha miundombinu.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mbuge anawasisitiza wakandarasi kufanya kazi kwa bidii kukamilisha kazi kwa wakati na kuzingatia sheria kutengeneza barabara zenye viwango pamoja na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika barabara wanazozitengeneza.

Aidha, amekemea baadhi ya wakandarasi kuacha tabia za kutowalipa stahiki zao vibarua wanaofanya kazi katika miradi hiyo.

“Kumekuwepo na malalamiko makubwa ya vibarua kutolipwa na mkandarasi akimaliza kazi anaondoka sitapenda kusikia haya mambo ya kutowalipa vibarua, lakini pia natoa wito kwa wakandarasi kuhakikisha wanatoa ajira kwa vijana na wananchi walioko eneo la mradi ili kukuza uchumi wao,” aliagiza Mbuge.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/558ac33dff6aa98c4bae3a92ee92442c.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi