loader
Waandishi 12 Tanzania kinara mafunzo ya Uongozi

Waandishi 12 Tanzania kinara mafunzo ya Uongozi

WAANDISHI  wa habari wanawake 12 kutoka Tanzania ni miongoni mwa wanahabari 91 waliohitimu mafunzo ya miezi tisa ya uongozi yanayoendeshwa na Taasisi ya Kimataifa inayojulikana kama WAN-IFRA/Women in News katika nchi mbalimbali duniani.

Waandishi waliohitimu na taasisi wanazotoka ni  Vicky Kimaro (Tanzania Standard Newspapers)  Sophia Kessy (Clouds Media);

Vumilia Mwasha (Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC1), Oliver Nyeriga (East Africa Radio/TV),  Elizabeth Nyivambe (Ushindi Radio); Kisali Simba, (Star TV);  Feliciana Manyanda (Radio Kwizera);  Haika Kimaro (Mwananchi Communication); Grace Mwakalinga (The Guardian Limited ); Mei Charles (Newala FM Radio);  Regina Muziwanda, (Idhaa ya Kiswahili ya BBC) na Stella Setumbi (Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC-Taifa).

Hadi sasa jumla ya waandishi 40 kutoka Tanzania wamepitia mafunzo hayo tangu yalipoanza kutolewa nchini mwaka 2015 na hivi sasa wanafanya vizuri katika maeneo yao ya kazi huku baadhi wakiwa ni wahariri na viongozi wa taasisi mbalimbali za kihabari ndani na nje ya Tanzania

Miongoni mwao, ni Beatrice Bandawe ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la kila siku la Nipashe linaochapishwa na kampuni ya The Guardian Limited ambaye kwenye hafla hiyo ya mahafali, alipata nafasi ya kueleza namna mafunzo yanayotolewa na WAN-IFRA Women in News yalivyomjengea uwezo wa kuwa kiongozi bora.

Mbali na  Tanzania, nchi nyingine za Afrika zilizoshiriki mafunzo hayo ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Botswana, Malawi, Zambia na Zimbabwe. 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WAN-IFRA/Women in News, Melanie Walker amesema mwaka 2021 umekuwa mwaka wenye changamoto nyingi duniani kote na sekta ya habari katika katika nchi za Afrika imeathirika zaidi na changamoto hizo.

“Tunatambua kuwa kila mmoja wenu, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, amekuwa akikabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya kifedha, kiusalama, kitaaluma, kiafya na kutokuwa na uhakika wa nini cha kufanya kuimarisha ustawi wake,” amesema Melanie.

Aidha amesisitiza kuwa  licha ya changamoto hizo, janga la Covid 19  limeongeza umaskini na pia kuongezeka kwa ukosefu wa usawa katika njanja mbalimbali.

Kwa upande wa taaluma, Melanie amesema Covid 19  imechochea hali ya jamii kukosa imani kwa vyombo vya habari hasa katika kipindi hiki ambacho kimegubikwa na wimbi la taarifa zisizo sahihi na zenye upotoshwaji wa hali ya juu.

Nae Mkurugenzi wa Afrika Women in News, Jane Godia amesema licha ya changamoto nyingi  mwaka huu umekuwa wa mafanikio makubwa katika Nyanja mbalimbali ikilinganisha na miaka mingine. 

“Idadi ya wahitimu imekuwa kubwa, kati ya wanafunzi 92 waliochaguliwa kushiriki kwenye mafunzo hayo, 91 wote wamehitimu, hili ni jambo la kujivunia,’’ alisisitiza.

Jane Godia, amesema mafunzo hayo ya  miezi tisa huwajengea uwezo waaandishi wa habari na wahariri wanaofaninikiwa kujiunga, katika masuala mbalimbali yakiwemo ya  uongozi wa taasisi za habari, uandishi wa habari za takwimu, uandishi wa habari za mitandaoni, masuala ya fedha, maadili ya uandishi wa habari, namna ya kutambua na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia, kingono, unyanyasaji wa mitandaoni, namna na kuongeza usawa wa kijinsia katika taarifa zinazoandikwa na pia katika taasisi za habari na namna ya kuwa waandishi bora na wenye maarifa na ujuzi wa kuhimili ushindani katika ulimwengu wa kidijitali.

Kwa upande wa Meneja mfawidhi wa program na mtaalamu mbobezi wa masuala ya demokrasi, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza  na  Mwakilishi wa SIDA, Fredrik Westerholm,  akizungumza katika hafla hiyo kazi zinazofanywa na Women in News kuwajengea uwezo wanawake ni muhimu sana na ziko sambamba na mikakati ya serikali ya Sweden katika kulinda na kutetea masuala ya haki za binadamu na uhuru wa kutoa maoni.

Amesema serikali ya Sweden kupitia shirika lake la SIDA wamekuwa wafadhili wakubwa wa programu hiyo.

“Wanawake katika vyombo vya habari wana mchango mkubwa sana katika kuchochea mabadiliko na pia wana nafasi kubwa katika kulinda na kutetea haki za binadamu na kudumisha amani na ustawi katika mataifa yao,’’ amesema

Katika hafla hiyo, serikali ya Norway ambaye imekuwa pia ikifadhili harakati hizo, iliwakilishwa na Harriet Berg ambaye ni Mkurugenzi wa Haki za binadamu, demokrasia na usawa wa jinsia katika wizara ya Mambo ya Nje.

Chushi Kasanda, Waziri wa Habari wa Zambia ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo kwa upande wake amesema kukosa ujuzi, sifa za kitaaluma, sera zinazoelekeza taasisi za kihabari namna bora ya kuajiri na kupandisha vyeo wanawake wenye uwezo na kukosekana na sera za jinsia kwenye vyombo vya habari, ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuwepo kwa idadi ndogo ya wanawake katika nafasi ya juu za uongozi.

“Nina furaha kuona Women in News wamekuwa wakijitahidi kupambana na changamoto hizo,’’ amesema Chushi.

Amesema Programu hiyo hadi sasa inaendeshwa katika nchi 17 na jumla ya wanawake 1,500 wamefaidika moja kwa moja.

Amesema kitendo cha mataifa mbalimbali ikiwepo Tanzania kuwakabidhi wanawake nafasi za juu za uongozi  ni ishara kwamba  wanawake wanao uwezo mkubwa na wana haki ya kushika nafasi yoyote katika jamii zao kama ilivyo kwa wananaume.

Kadhalika, Waziri huyo  aliwataka wahitimu kutumia uwezo na nguvu ya kushawishi waliyonayo katika jamii kuelimisha watu ili waondokane na fikra potofu kuhusu uwezo wa wanawake wa shirika hilo.

Naye Tamala Chirwa, Mkurugenzi wa shirika hilo anayeshughulikia utendaji na raslimali watu aliwataka wahitimu  kutumia maarifa na ujuzi waliyopata kwenye mafunzo hayo kuleta mabadiliko katika taasisi zao, kwenye sekta ya habari na katika bara la Afrika kwenye suala zima la usawa wa kijinsia.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2f4bb20924e696fad6593984c481f2b1.jpg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi