loader
KKKT yaeleza ilivyosaidia kumaliza mauaji ya albino

KKKT yaeleza ilivyosaidia kumaliza mauaji ya albino

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria kupitia programu zake mbalimbali za mafunzo kwa jamii, limewafi kia na kuwaelimisha zaidi ya waganga wa kienyeji 2,000 kuhusu ualbino na jinsi mtu anavyozaliwa na hali hiyo.

Kanisa linaamini elimu hiyo ilikuwa na mchango mkubwa kwani kuanzia mwaka 2017 hadi leo hakuna mauaji ya albino yaliyoripotiwa. Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni mkoani Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Happiness Gefi kwenye uzinduzi wa Mradi Mpya wa miaka mitatu na nusu wa Chaguo Langu, Haki Yangu unaolenga kuwawezesha wanawake na vijana kulinda na kutunza afya na haki zao za ujinsia na uzazi bila kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Uzinduzi wa mradi huo umefanywa katika kipindi cha kampeni ya maadhimisho ya Siku 16 zinazoendelea za kupinga ukatili wa kijinsia nchini huku msisitizo ukiwekwa kwa jamii nzima kuona harakati hizo ni wajibu wao kukemea vitendo hivyo viovu. Gefi alisema Kanisa la KKKT-Dayosisi hiyo liliona katika jamii kuna tatizo hususani ukanda wao unaohusisha mikoa ya Shinyanga na Simiyu ambayo ni miongoni mwa iliyoongoza kwa mauaji ya albino kutokana na imani za kishirikina.

“Kama kanisa tulisema KKKT hatuwezi kunyamaza kuendelea kushuhudia vitendo vya ukatili kwa albino, tukasema tutoke twende kwa waganga wa kienyeji, tuzungumze nao, tuwaelimishe kuhusu albino. Mwanzoni hata makanisa mengine walitushangaa, ila tulijua tunakusudia nini kukomesha ukatili huo,” alisema Gefi.

Alisema katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga Dayosisi hiyo ambayo ina programu za huduma kwa jamii ilianza kuwafuata waganga hao wa kienyeji na baada ya muda waliwafikia zaidi ya waganga 2,000 ambao wote walielimishwa na kubadilisha mitazamo yao kuhusu ualbino.

Gefi alisema programu hiyo ilikuwa na kauli mbiu: ‘Mauaji ya Albino sasa basi!’ na baada ya kutekelezwa kwa programu hiyo waganga wa kienyeji walielewa ualbino ni nini, unatokeaje na hivyo kuondokana na imani potofu ya kuwaua kwa kuhusisha na utajiri kwa nguvu ya giza.

“Kwa kweli kama kanisa na Dayosisi tulileta mabadiliko katika mikoa ile, kuanzia mwaka 2017 hadi leo 2021 hakuna kesi ya mauaji ya albino iliyoripotiwa,” alisema Gefi. Alisema dayosisi hiyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii vikiwemo vinasababishwa na imani za kishirikina.

Katika uzinduzi huo, Askofu Mkuu wa KKKTTanzania, Dk Frederick Shoo aliitaka jamii nzima kushiriki katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia na kusema hilo ni jukumu la wote na wala sio la kundi fulani au kuiachia serikali.

Dk Shoo alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia vipo zaidi pia kwa watu wenye ulemavu na kutaka jamii kubadilika na kuacha ukatili kwa sababu wenye ulemavu ni binadamu kama walivyo wengine na wana haki ya kutotendewa isivyo, bali waishi na kupendwa kama watu wasio na ulemavu.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA)- Tanzania, Jacquline Mahon alisema wakati huu kampeni ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ikiendelea, watu wenye ulemavu wameendelea kukabiliwa na ukatili zaidi, mara mbili ya watu wasio na ulemavu.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za NBS za Sensa ya mwaka 2012, asilimia 9.3 ya watu wote nchini Tanzania wanaishi na ulemavu na miongoni mwao wanashindwa kupata haki za msingi kama elimu kutokana na ulemavu wao.

Mahon alisema hali sio nzuri kwa upande wa vijijini kwa sababu asilimia kubwa ya walemavu wanaishi katika mazingira ya kubaguliwa na kuwekewa vikwazo kwa ustawi wao, hivyo jamii, wadau, serikali kwa kauli moja inapaswa kuendelea kupinga ukatili huo

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/1f9697b62bd008c99c73cb6858516e0b.jpeg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Na Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi