loader
Watanzania tuwe wazalendo kulinda miundombinu

Watanzania tuwe wazalendo kulinda miundombinu

KATI ya kero kubwa iliyosumbua wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu ni msongamano wa magari na foleni kiasi cha kusababisha hasara kubwa katika uzalishaji nchini.

Hali hiyo ilitokana na ufinyu wa miundombinu ya barabara isiyoendana na ukuaji wa idadi na mahitaji kwa wakazi wa jiji hilo, kiasi cha kusababisha suala la usafiri kuwa kero kubwa kwa muda mrefu.

Hata hivyo, serikali imekuwa ikibuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo upanuzi wa barabara zinazoingia na kutoka kwenye maeneo yenye uhitaji lakini kubwa zaidi kujenga miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi katikati ya jiji hilo.

Mradi huo utakaokuwa na awamu sita za ujenzi, tayari awamu ya kwanza imekamilika na kuanza kutumika na kuonyesha wazi namna inavyosaidia kupuguza foleni huku awamu ya pili ambayo ni ya Mbagala iliyofikia sasa asilimia 42.

Pamoja na nia njema ya serikali ya kumaliza tatizo la usafiri katika jiji hilo, bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa uzalendo kwa baadhi ya wananchi wanaohujumu mradi huo kwa kujihusisha na wizi wa vifaa na mafuta ya mitambo ya ujenzi.

Jana Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka, Awamu ya Pili, Mbagala Rangi Tatu aliwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo kwa hali na mali kwa kuwa pamoja na kuwa na faida kubwa kwao na taifa kiuchumi lakini pia serikali imetumia fedha nyingi kuijenga.

Tunawaomba Watanzania kutambua umuhimu wa mradi huo na kuwa wazalendo kulinda na kuhakikisha kwamba unakamilika kwa wakati bila changamoto zilizotajwa ili kuinua uchumi wa watu binafsi na wa taifa.

Ukweli ni kwamba, kuhujumu miradi hiyo si jambo jema kwani barabara hizo zinajengwa kwa manufaa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa kwa ujumla.

Pamoja na uhujumu wa miundombinu pia, wapo baadhi ya watumiaji wa barabara wanaomwaga mafuta barabarani, kuzidisha uzito wa mizigo, kuziba mifereji ya maji, uegeshaji holela wa magari na kulima kandokando ya barabara mambo yanayoharibu barabara na kuleta hasara kwa serikali .

Ni wakati sasa kwa Watanzania kuiunga mkono serikali chini ya Rais Samia na kwa pamoja kuilinda miundombinu ya nchi ambayo si tu inasaidia serikali pekee bali Watanzania wote kiujumla.

Nchi yoyote yenye miundombonu imara na bora, inayorahisisha mambo mbalimbali muhimu hususani ya huduma za kijamii kufikika kwa urahisi ni wazi kuwa nchi hiyo uchumi wake utafunguka na maendeleo ya wananchi wake yataimarika.

Kwa misingi hiyo shime Watanzania popote tulipo tulinde miundombinu yetu kwa manufaa yetu na taifa

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3218e4be5e0acac67918d036992f57ef.jpg

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi