loader
‘Serikali inataka kuona vijana mnanufaika na fursa’

‘Serikali inataka kuona vijana mnanufaika na fursa’

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema msimamo wa Serikali ni kuona vijana wanachangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa na kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo. Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kilele cha shindano la wazo bunifu la biashara lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Helvetas chini ya mradi wa Youth Employment Through Skills Enhancement (YES).

Shirika hilo lilishirikiana kuandaa shindano hilo na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Dodoma na Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA). Shekimweri alisema Serikali inaunga mkononi juhudi za wadau mbalimbali wakiwemo wadau wa maendeleo kama Halvetas, mashirika na asasi zisizo za Serikali na sekta binafsi zenye lengo la kuwapatia vijana ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kuwapatia ajira au kujiajiri.

“Serikali inaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za wadau mbalimbali zinazolenga katika kuwasaidia vijana kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa ili kuwezesha kila fursa inayopatikana inaleta manufaa na kubadilisha maisha ya kijana wa Kitanzania,” alisema. Aliwataka vijana kufanyia kazi mawazo ya biashara waliyonayo ili kuleta tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla.

Alisema vijana wamekuwa na ndoto na mawazo mengi lakini yamekuwa yakipotea kutokana na kukosa uthubutu. Alisema kama vijana watakuwa na uthubutu watakuza dhana ya uwekezaji na kukuza mitaji. Pia aliwataka vijana kujiunga kwenye vikundi ili wafaidike na fursa za mikopo zinazotolewa na halmashauri. Alisema katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu Halmashauri ya Jiji la Dodoma limetoa mikopo ya Sh bilioni 1.3 kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.

Alisema ana mfano wa kikundi cha vijana wasomi waliojiunga kwenye kikundi na kufungua biashara ya masuala ya kompyuta kwa kuzitengeneza na kuingiza mifumo na sasa wanapata kazi kutoka taasisi za umma na binafsi katika mikoa ya Singida, Dodoma na Arusha. Alisema kikundi hicho cha vijana kimepata mkopo wa Sh milioni 40 kutoka halmashauri na hivyo kuweza kununua gari na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya kazi zao.

“Vijana mjiunge kwenye vikundi mpate sifa za kukopesheka. Ni fursa nzuri sana ya kuwatoa kimaisha na kutimiza ndoto zenu,” alisema. Kwa upande wake, Meneja mradi wa YES kutoka Shirika la Helvetas, Africano Chalamila alisema lengo la shindano hilo ni kuonesha ari na ubunifu kwa vijana Alisema shindano hilo lilianza Septemba mwaka huu ambapo jumla ya fomu 176 zilichukuliwa na fomu 72 zilirejeshwa.

Alisema washiriki waliandika wazo la biashara na majaji waliwatembelea washiriki kuona shughuli wanazofanya. Alisema mchujo mwingine ulifanyika na kubakiza washiriki 18 ambao walipata kura za kutosha. Washindi katika shindano hilo walitajwa kuwa ni Ijen Group waliopata zawadi ya Sh milioni 1.5, na Dell Food waliopata zawadi ya Sh milioni 1.5. Kwenye kipengele cha wazo binafsi mshindi alikuwa Fred Julius aliyepata zawadi ya Sh 1,000,000.

Mshindi mwingine alikuwa Gerald Mlyomi aliyepata Sh 500,000 na kikundi cha Youth Group kilipata zawadi ya Sh 700,000, mshindi mwingine alikuwa Nuru Mollel aliyepata zawadi ya Sh 600,000.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/6611b3518408b9ddd44f15d352f4fe30.jpeg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Na Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi