loader
Askofu Shoo: Msiwatumie walemavu kujinufaisha

Askofu Shoo: Msiwatumie walemavu kujinufaisha

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo ameziasa asasi za kiraia na mashirika yasio ya kiserikali kuacha kuwatumia waathirika wa ukatili wa kijinsia wakiwemo walemavu kujinufaisha.

Dk Shoo alisema hayo jana mjini Moshi katika Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Alisema baadhi ya asasi na mashirika yamekuwa yakitumia waathirika wa ukatili wa kijinsia na walemavu kwa maslahi binafsi na kuyataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Dk Shoo alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia nafasi, mamlaka na nguvu za madaraka kuwanyanyasa waathirika hao.

“Tunawanyanyasa maana hawana nguvu ya kujitetea na wanapojaribu kujitetea wanazuiwa, tunahitaji kupiga kelele kwa ajili yao wanaofanyiwa ukatili na kuwatia moyo ili waweze kujiamini na kupaza sauti zao wenyewe kujitetea,” alisema.

Alisema ukatili wa kijinsia umekuwa ukifanyika kwa siri kwa watu wenye ulemavu na sehemu nyingine umekuwa ukifanyika hadharani jambo ambalo limekuwa likiwasababishia kuathirika kisaikolojia.

“Sio jambo la siri ukatili wa kijinsia upo katika jamii zetu na sio hapa Tanzania tu, ila upo dunia nzima hasa kwa watu wenye ulemavu. Ni wajibu wetu kuungana nao kufichua vitendo hivyo, twende bega kwa bega na tuwashike mkono ili ifike mahali waweze kusimama wenyewe kutetea haki zao na  kukataa kufanyiwa ukatili,” alisema Dk Shoo.

Ofisa wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Dawati la Jinsia,  Asia Matuka alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Mkoa wa Kilimanjaro vimepungua kutokana na elimu kutolewa kwa jamii na kwamba takwimu zinaonyesha katika kipindi cha mwaka huu  walipokea taarifa za makosa ya ukatili 829  na mwaka jana yalikuwa 1,144.

“Katika matukio tuliyopokea mwaka huu ya ukatili, zaidi ya 400 ni ya watoto kufanyiwa vitendo viovu kama kubakwa, kulawiti, kunyanywaswa kingono, ukeketaji, vipigo kutoka kwa wakubwa, makosa yalikuwa ni 563, kuna upungufu wa makosa ya ukatili kwa asilimia 27, japo yamepungua bado jitihada zinahitajika kupambana nayo,” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/546fc1c452e69abc6e16b6ce6aaded07.jpg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Upendo Mosha, Moshi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi