loader
Vuna Zaidi na NBC Shambani yatikisa Lindi, Mtwara

Vuna Zaidi na NBC Shambani yatikisa Lindi, Mtwara

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi baiskeli, pikipiki, guta na trekta kwa washindi wa droo ya sita ya kampeni ya ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’ kwa mikoa ya Mtwara na Lindi.

Akikabidhi zawadi hizo kwa washindi, Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Abdallah Malela alisema zawadi hizo zimekuja wakati muafaka kwani zitasaidia washindi kutekeleza kwa vitendo mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kutoka tani 280,000 hadi kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Hivi karibuni Mkoa wa Mtwara uliweka azimio kwamba kuanzia msimu ujao wa kilimo kila chama kikuu cha ushirika lazima kiwe na shamba darasa lenye ukubwa wa ekari 1,500. Katika mpangilio wa zawadi, trekta limekwenda kwa Chama kikuu cha Ushirika wa wakulima MtwaraMasasi ( MAMCU) huku zawadi zingine 26 ikiwemo pikipiki 7, baiskeli 9, pampu za kupulizia dawa mikorosho 8, guta 1, kanga, mabegi ya shule na madaftari zikienda kwa wakulima mmoja mmoja. Malela pamoja na kuwapongeza Mamcu kwa trekta alielezea matumaini yake kwamba zana hiyo itasaidia kutekeleza malengo ya mkoa ya kupanua kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dastan Kyobya aliahidi kutoa eneo la ekari 1,500 kwa MAMCU ili liweze kutumika katika kufanikisha shughuli za kilimo cha ushirika huo, ikiwa ni ishara pia ya kuunga mkono nia njema ya benki ya NBC katika kuwasaidia wakulima hao.

“Kwa kuwa NBC tayari wameanza kwa kuwazawadia zana za kilimo ikiwemo trekta na sisi serikali ya mkoa tunawapatia eneo la kutosha ekari 1,500 ili muweze kufanikisha azimio la kulima ekari 1,500 katika msimu ujao wa kilimo,” alisema Kyobya. Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Waziri Barnabas alisema tangu kuanza kwa kampeni hiyo jumla ya washindi 139 wamejipatia zawadi mbalimbali zilizotengwa kwa kampeni hiyo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo wa Benki ya NBC, Raymond Urassa aliwataka wakulima waendelee kupitishia fedha zao katika akaunti ya NBC Shambani ili wawe kwenye nafasi kujishindia zawadi lukuki katika droo zinazofuata.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/eaab13d23b671c2129b86d33f8d63a84.jpeg

MGODI wa kati wa madini ya dhahabu ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi