loader
REDNOTICE NI VITA YA UTATU KWA MAYAI YA MALKIA CLEOPATRA

REDNOTICE NI VITA YA UTATU KWA MAYAI YA MALKIA CLEOPATRA

NCHINI Misri kunatarajiwa kufanyika harusi kubwa ya mtoto wa mmoja wa wafanyabiashara mashuhuri nchini humo. Kwa kuwa huyu anayeolewa ni binti wake wa pekee, mfanyabiashara huyo anataka amzawadie zawadi ya tofauti na ya kihistoria binti wake.

Anaahidi kutoa dola milioni 300 za Marekani kwa yeyote ambaye atafanikiwa kuleta hazina ya utatu wa mayai ya Malkia Cleopatra yaliyopotea zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko Misri.

Mayai haya Malkia Cleopatra alizawadiwa na Jenerali wa Kiroma, Marcus Antonius miaka 2000 iliyopita. Mchongo huu unatua kwa Nolan Booth, mwizi maarufu mwenye shahada za sanaa katika ukwapuaji duniani. Huyu jamaa ni noma sana. Baada ya kusikia kuhusu kitita hicho cha dola milioni 300 Nolan anaingia kazini kuyasaka mayai hayo ili ayapeleke Misri akavute donge nono.

Ugumu ni kwamba yai moja kati ya mayai hayo matatu kwa sasa lipo chini ya mamlaka ya Makumbusho ya Taifa ya Roma nchini Italia, limewekewa ulinzi mkubwa. Yai la pili lipo kwenye himaya ya muuza silaha maarufu na tishio nchini Hispania, Sotto Voce, na ulinzi wake pia si wa kitoto. Yai la tatu…

hili hakuna anayefahamu lilipo isipokuwa Nolan Booth pekee ndiye anayejua wapi pa kulipata. Patamu hapo! Wakati Nolan anajipanga kuanza mishe ya kuyasaka mayai hayo matatu, anagundua uwepo wa mtu anayeitwa John Hartley, wakala wa FBI anayejua thamani ya mayai hayo na jinsi yanavyosakwa tangu dau lilipotangazwa nchini Misri.

Hartley anafahamu fika kuwa mmoja wa watu watakaojitosa kuyasaka mayai hayo na hata kuyaiba ni Nolan Booth. Leo ndiyo siku ya kwanza ya kusaka yai la kwanza na Polisi macho yao yote yapo katika makubusho ya taifa ya Roma, wakala Hartley pia anatua Roma kuhakikisha hakuna yeyote atakayeligusa yai hilo.

Lakini baada ya muda Hartley anagundua kuwa kuna kitu hakipo sawa katika eneo hilo, na anahisi kuwa huenda tayari ‘wameshapigwa’ maana kila anapojaribu kulitazama yai hilo ni kama halielewi! Anapohakikisha kama ni kweli wamepigwa anagundua kuwa tayari limeshaibiwa kitambo! Na ni nani anayeweza kuliiba yai hilo katikati ya ulinzi mkali kama si Nolan Booth?.

Nolan akiwa maskani kwake akijipongeza kwa kuliiba yai hilo, anahisi kama kuna kitu hakiko sawa, anageuka na kukutana na wakala Hartley akiwa ametulia hana wasiwasi. Nolan anashangaa, huyu mtu amejuaje kama yeye amejichimbia hapo? Kumbe Hartley alikwisha shtukia mchongo mzima kuwa Nolan akifanikiwa kuliiba yai hilo atakuja mahali hapo. Amemwibukia kumwonesha kuwa yeye ni mafia zaidi yake.

Kitendo cha kufumba na kufumbua polisi wanalizingira jengo hilo na kumkamata Nolan kirahisi baada ya kuwasumbua kwa muda mrefu na yai linatua mikononi mwa polisi tayari kurudishwa makumbusho ya taifa ya Roma. Shukrani za dhati ziende kwa Hartley. Kesho yake mpelelezi huyu akiwa anajipongeza baada ya mpango huo kukamilika, ghafla anazungukwa na polisi wa Italia na kuwekwa chini ya ulinzi.

Inasemekana kuwa jana baada ya kumkamata Nolan na yeye kulichukua lile yai, eti lilibadilishwa na kuweka yai feki tofauti na lile walilolikamata. Na mtu aliyefanya mchongo huo hajulikani! Kwa kuwa Nolan alishakamatwa sasa Hartley anakuwa mshtakiwa namba moja kwa sababu yeye ndiye aliyekabidhiwa yai. Lakini… ngoja kwanza! Hartley anawezaje kuwa mwizi wakati yeye ndiye anayepambana na wezi kiasi cha kumkamata mwizi wa yai hilo, sasa iweje tena awe mwizi?

Hapana! Hapa kuna kitu hakipo sawa! Kumbe jana wakati Hartley analihifadhi lile yai kuna askari mmoja ni kama alifunga mlango wa gari lililobeba yai na kuufungua tena akiwa ana yai jingine mkononi! Huyu ni nani? Mbona kama… Oh yeah… huyu ni Sarah Black maarufu kama ‘The Bishop’, mwizi maarufu anayetafutwa kwa miaka mingi na ni mpinzani mkubwa wa mwizi aliyekamatwa, yaani Nolan Booth.

Huyu mwanadada ni noma mno kuliko hata Nolan, hata polisi wanamwogopa. Huyu Sarah pia ameingia kwenye mpango wa kuyasaka mayai hayo matatu ili akalambe donge nono. Tayari analo yai moja mkononi, bado mengine mawili. Kwa upande mwingine mpelelezi Hartley ndo kishadakwa akihisiwa kuliiba yai hilo, mwanzoni alidhani mbaya wake ni Nolan pekee kumbe kuna kiumbe mwingine hatari kinoma. Sasa Hartley anaingizwa mahabusu na huko anakutana na Nolan Booth. Hapa ngoma inogile. Kumbuka Nolan alikamatwa na Hartley, na sasa Hartley amekamatwa kisa Sarah, na Sarah ni mpinzani wa Nolan.

Sasa, vita ya Hartley inahamia kwa Sarah, na ili ampate Sarah na aweze kujisafisha kule polisi kuwa hakuiba inabidi amtumie Nolan. Ili kumtumia Nolan inabidi amsaidie kuyapata mayai yote matatu ndipo ampate Sarah, na Sarah naye ili ayapate mayai yote inabidi ampate Nolan kwani ndiye anayefahamu lilipo yai la tatu maana yeye ana yai moja na la pili anafahamu lipo Hispania.

Sijui kama tumeelewana! Hakuna namna, mpelelezi Hartley anaungana na mhalifu kumsaidia apate mayai ili aweze kumpata Sarah. Sasa huo mtafute mtafute unaopigwa ndani ya sinema hii ni noma sana.

Kama wewe ni mpenzi wa movie za aksheni usiikose sinema hii. Ni filamu ya Marekani yenye dakika 118 iliyotoka Novemba 2021, imesambazwa na Netflix na imetengenezwa kwa bajeti ya dola milioni 200.

Hii ndiyo filamu iliyoweka rekodi ya kutazamwa zaidi kwa muda wote katika mtandao wa Netflix.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/6ed15b350308c2febd617cc9798716b0.jpeg

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Na Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi