loader
Serikali yalipa watumishi bil 30/-

Serikali yalipa watumishi bil 30/-

SERIKALI imetangaza kulipa kiasi cha Sh bilioni 30 kwa watumishi wa umma waliokuwa na madai mbalimbali ya kiutumishi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa alisema hayo mjini Kigoma akizungumza na watumishi wa umma akiwa ziarani mkoani Kigoma.

Mchengerwa alisema malipo hayo kwa watumishi 18,000 yalitarajiwa kuanza kutolewa jana kwa malipo hayo kulipwa kwenye mfumo wao wa malipo.

Sambamba na hao, Mchengerwa alisema serikali inatarajia kulipa Sh bilioni 40 kwa watumishi wa umma zaidi ya 20,000 ambao walikuwa na madai mbalimbali ya kiutumishi na malipo hayo yanatarajia kufanyika Januari.

“Mpango wa serikali ni kuhakikisha madeni yote ya kiutumishi kwa watumishi wa umma yanalipwa ili kumaliza madeni yote na kuanzia mwezi Februari serikali haitaki kuona kunakuwa na deni lolote la kiutumishi kwa watumishi wa umma,” alisema.

Aidha, serikali imetangaza kuwa malipo ya mshahara wa mwezi huu wa Desemba kwa watumishi wote wa umma utaanza kulipwa kuanzia jana ili kuwafanya watumishi hao kuanza mapema maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

“Tunaelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka hivyo Mheshimiwa Rais hataki kuona sikukuu zinakuwa na unyonge na malalamiko ya kukosa pesa hivyo malipo ya mishahara italipwa mapema kila mtumishi awe na uhuru na furaha ya sikukuu,” alisema Mchengerwa.

Katika mkutano huo, waziri huyo wa Utumishi alisema serikali imedhamiria kuufanya utumishi wa umma kuwa nguzo kuu ya utumishi nchini ili kuwafanya watu kukimbilia kuomba ajira serikalini badala ya taasisi binafsi.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kurudisha hadhi na heshima ya utumishi wa umma kwa kuondoa changamoto zilizokuwepo na kwa miezi tisa ya utawala wake, watumishi 196,000 wamepandishwa madaraja na mishahara na hivi karibuni watumishi 96,000 wameongezwa katika kupata stahiki hiyo.

Amewaonywa maofisa utumishi nchini wasiotekeleza maagizo na maelekezo yanayotolewa na Rais Samia kwamba watachukuliwa hatua kali. Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Rashidi Mchatta alisema mkoa unakabiliwa na changamoto ya kiutumishi kwa watumishi wengi wa umma wanaopangiwa kuomba kuhama hivyo kusababisha kuwa na idadi kubwa ya upungufu wa watumishi.

Mchatta alisema sambamba na hilo, watumishi wengine wanaopangwa mkoani humo wamekuwa hawaripoti na kuacha kazi wakihofia usalama kutokana na dhana kwamba mkoa huo una hali ya usalama kama zilivyo nchi za jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameipongeza serikali kwa kuboresha hali ya utumishi wa umma nchini kwa watumishi kupata stahiki zao na kuboreshewa miundombinu ya kufanyia kazi na kuishi.

Alisema jambo bado zipo changamoto chache za kiutumishi kama mkoa wataendelea kushirikiana na wizara na mamlaka nyingine kuhakikisha changamoto za kiutumishi zinafanyiwa kazi kwa wakati.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3b42dda117500a5e53c14a9836719eae.jpeg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah, Kigoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi