MKUU wa Polisi (IG) Hillary Mutyambai, amesema maofisa 3,000 wa magereza wameingizwa katika huduma za kitaifa za polisi ili kuimarisha usalama.
Mutyambai aliwambia wanahabari kuwa, maofisa hao hao kutoka magereza
watafanya kazi na maofisa wa polisi katika kipindichote cha sikukuu za mwisho wa mwaka na kwamba, watatangazwa kuwa maofisa maalumu kabla ya kutumwa.
Alisema hayo ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa kukabiliana na matishio mbalimbali nchini.
“Magereza itatoa maofisa 3000 kushika doria katika miji
katika msimu huu wa sikukuu. Tunawahakikishia Wakenya tuko katika mambo ya juu kuhusu usalama na tunaomba ushirikiano endelevu,” alisema Mutyambai.
Akiwa ameambatana na Kamishna Jenerali wa Magereza Brigedia Mstaafu, John Kibaso Warioba na maofisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama, Mutyambai
alisema ameahirisha likizo kwa maofisa wote waliokuwa likizo na kuamuru warejelee katika kazi zao.
Ukweli kwamba viongozi wanatafuta kuongezwa nguvu kutoka kwa magereza unapendekeza majukumu makubwa yaliyo mbele yao. Kenya imekuwa katika hali ya tahadhari dhidi ya masuala ya ugaidi.