loader
Watumishi wa umma tutimize wajibu, serikali inazidi kutujali

Watumishi wa umma tutimize wajibu, serikali inazidi kutujali

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa ametangaza kuwa serikali inalipa kiasi cha Sh bilioni 30 kwa watumishi wa umma waliokuwa na madai mbalimbali ya kiutumishi.

Waziri Mchengerwa alisema hayo wakati akizungumza na watumishi wa umma juzi akiwa ziarani mkoani Kigoma, ambapo alibainisha kuwa, malipo hayo kwa watumishi 18,000 yameshaanza na kwamba serikali inatarajia kulipa Sh bilioni 40 kwa watumishi wa umma zaidi ya 20,000 ambao walikuwa na madai mbalimbali ya kiutumishi na malipo hayo yanatarajiwa kufanyika Januari, mwakani.

Binafsi napongeza uamuzi huo wa Serikali wa Awamu ya Sita chini ya Rais

Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha madeni yote ya kiutumishi kwa watumishi wa umma yanalipwa ili kumaliza madeni yote na nia yake ya kutaka kuanzia Februari, mwakani serikali haitaki kuona kunakuwa na deni lolote la kiutumishi kwa watumishi wa umma.

Hatua hii inanifanya nione ni kwa kiasi gani Rais Samia amenuia kuwainua watumishi wa umma na familia zao kwa ujumla kwani madeni hayo yakilipwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ugumu wa maisha.

Fedha hizo zitawawezesha watumishi hao kufanya malipo mengine mbalimbali na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii.

Lakini nimeguswa na kauli ya Mchengerwa ya kutangaza kuwa malipo ya mshahara wa mwezi huu wa Desemba kwa watumishi wote wa umma yalianza kulipwa kuanzia juzi na jana kwa maana ya Desemba

20 na 21 ili watumishi hao waanze mapema maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Hii ndiyo mifano midogo inayoonesha kuwa serikali hii ya awamu ya sita ni ya kusikiliza na kuwajali wananchi wake.

Napongeza harakati za kuufanya utumishi wa umma kuwa nguzo kuu ya utumishi nchini itakayokimbiliwa na watu kuomba ajira serikalini badala ya taasisi binafsi kwa kurudisha hadhi na heshima ya utumishi wa umma.

Ninaiona nia ya dhati ya Rais Samia kufanikisha hilo kwa kuwa kwa miezi tisa ya utawala wake ameondoa changamoto zilizokuwepo za watumishi wa umma, watumishi 196,000 wamepandishwa madaraja na mishahara na hivi karibuni watumishi 96,000 wameongezwa katika kupata stahiki hizo.

Natoa rai kwa watumishi wa umma kuunga mkono kivitendo nia ya Rais Samia

ya kuboresha utumishi wa umma na hii inaweza kufanikiwa hasa kwa kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu katika kazi.

Kutimiza wajibu kunaweza kusababisha kudai haki zaidi na kuzipata kwa kuwa hakuna haki bila ya utimizwaji wa wajibu wa shughuli husika hasa kwa watumishi wa umma.

Siyo muda wa kuendelea kuwa na watumishi ambao hawatekelezi maagizo na maelekezo yanayotolewa na serikali kwa ngazi yoyote ile kwa kuwa kwa kufanya hivyo kunakwamisha mambo mengi kuendelea.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a6238ba6adafab1f52ea152b5703eb72.jpeg

SERIKALI kupitia Shirika ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi