loader
Tudumishe ulinzi shirikishi sikukuu za mwisho wa mwaka

Tudumishe ulinzi shirikishi sikukuu za mwisho wa mwaka

WAKATI sikukuu za mwisho wa mwaka zikikaribia, suala la ulinzi na usalama ndani ya familia pamoja na jamii nzima kwa ujumla linahitaji ushirikishwaji wa kila mtu ili kukabiliana na uhalifu ambao aghalabu umekuwa ukijitokeza kila zifikapo Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Ili kufanikisha ulinzi shirikishi kwa jamii, inatakiwa kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake, mlinzi wa mtoto wa mwenzake, awe mlinzi wa nyumba ya mwenzake na pia awe mlinzi wa mali ya mwenzake wakati wote wa sikukuu hizo na hata baada ya kipindi cha sikukuu.

Ulinzi wa watoto unaanzia nyumbani kwa kuhakikisha kuwa muda wote watoto wanapata uangalizi wa karibu wakati wa kucheza na pia kuhakikisha kuwa watoto wanapotoka kwenda kula sikukuu wanaambatana na watu wazima ili kuhakikisha 

usalama wao barabarani na kwa kila watu wanaokutana nao.

Ulinzi wa nyumba unakuwa wa usiku na mchana kuhakikisha kuwa hakuna watu wenye nia mbaya wanaozikaribia nyumba au makazi ya majirani lakini pia kila mtu ahakikishe kuwa milango ya nyumba yake au ya jirani inafungwa pindi familia yote inapotoka nje ya eneo la nyumbani.

Kwa kufanya hivyo ina maana hatari yoyote inayonyemelea nyumba yako au ya jirani inaweza kubainika kupitia kwa majirani na hatimaye kuokoa maisha ya watu na mali zao kupitia nadharia ya ulinzi shirikishi katika jamii.

Ulinzi shirikishi kwa hakika ndio njia pekee yenye kuhakikisha ulinzi na usalama wa familia katika vipindi vyenye changamoto za kiusalama kama vipindi vya kuelekea katika sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo matukio ya kihalifu yanaongezeka kwa sababu wezi wanatafuta fedha kwa ajili ya sikukuu.

Ingawa Jeshi la Polisi lipo na linatimiza majukumu yake ipasavyo, ni ngumu polisi kuweza kufika kila mahali kwa wakati mmoja. Njia pekee ya kuhakikisha ulinzi katika jamii kipindi kama hiki ni kupitia ulinzi shirikishi ambalo ni jukumu la kila mtu ili kurahisisha kazi ya ulinzi na usalama.

Ushirikiano huo unapaswa kwenda mbali zaidi hata nyakati za usiku ikiwa mmoja wa wanajamii amevamiwa au mlango wake umevunjwa na vibaka majirani wengine tunapaswa kujitolea kumsaidia kupambana na majambazi hao ili kuwafundisha kuwa katika jamii kuna umoja na ni ngumu kufanya uhalifu kwa kuwa wananchi wameungana.

Wazazi na walezi wana jukumu la kuhakikisha kuwa watoto wanawahi kurudi nyumbani wakati wa kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ili kudhibiti wimbi la watoto kupotea. Ni jambo la ajabu sana kuona wazazi na walezi wapo kimya wakati mtoto au watoto wao wanachelewa kurudi nyumbani kutoka matembezini.

Kwa kawaida inatakiwa hadi kufika saa kumi na mbili watoto wawe wamerudi nyumbani na kucheza katika maeneo ya karibu na nyumbani. Sio unakuta watoto wanacheza mitaani hadi saa mbili usiku na wazazi wapo kimya nyumbani.

Kama watoto wataenda kucheza mtaani wakachelewa hadi saa mbili usiku ni vema wazazi au walezi wakaandamana nao ili kuhakikisha suala la usalama wao linakuwepo mikononi mwa wazazi wao au walezi wao.

Vilevile wazazi wahakikishe kuwa wanasikiliza na kufuata maelekezo ya Jeshi la Polisi kuhusu mambo ambayo watoto wanatakiwa wafanye wakati wa kusherehekea sikukuu na mambo yasiyotakiwa kufanywa na watoto ili kutoingia katika matatizo.

Kwa kuzingatia hayo, ni imani yangu kuwa kila mwananchi atasherehekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa amani na utulivu na kufanikiwa kuuaga mwaka 2021 na kuanza maisha mapya ya mwaka 2022.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/899e137ee647f722750dbc065c1d954b.jpeg

SERIKALI kupitia Shirika ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi