loader
SMZ na uamuzi bora kuwarudisha shule watoto 4,800

SMZ na uamuzi bora kuwarudisha shule watoto 4,800

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepongezwa kwa juhudi zake kuhakikisha watoto wote wenye haki ya kupata elimu wanafaidika na fursa hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itafanikisha kufikiwa kwa malengo endelevu ya dunia katika sekta ya elimu kwa watoto na kupambana na adui ujinga.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Shalina Bahuguna anasema hatua hiyo ni muhimu.

Alikuwa shuhuda wa utiaji saini wa mradi wa kuwarudisha watoto shule waliotoroka ambao unatekelezwa na Taasisi inayohusika na elimu kwa wote ya EAC kutoka Qatar.

Bahuguna alisema elimu ni miongoni mwa haki ya msingi ya watoto kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ambapo husaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na ujinga wa kutojuwa kusoma na kuandika.

Anasema idadi wa wanafunzi 4,809 wametambuliwa kuwa wapo nje ya mfumo wa elimu ya lazima na ni wengi hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuwarejesha shule na kupata elimu ya lazima.

“Nimefurahishwa na juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya kuwapatia tena elimu wanafunzi walioacha shule ambayo ni haki ya msingi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ya EAC ya Qatar, Mary Pigozzi alisema utafiti uliofanywa awali katika kutekeleza mradi huo unaonesha wanafunzi wengi wapo nje ya mfumo wa elimu ya lazima huku wakijishughulisha na ajira mbaya.

Anasema taasisi yake inatekeleza mradi wa kuwarudisha shule watoto waliopo nje ya elimu ya lazima ambapo juhudi kama hizo zimefanywa katika nchi mbalimbali duniani.

Pigozzi amesema wamefurahishwa na juhudi hizo ambazo zimelenga kuwarudisha shule watoto 4,809 sawa na asilimia 67.3 ya matarajio katika hatua za awali.

Akizungumza katika utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said anasema sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele 17 vya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021-2022.

Simai anasema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeifanya elimu ya maandalizi na msingi hadi sekondari kuwa ya lazima ambapo kila mwanafunzi anastahili kuipata.

Anasema katika utekelezaji wa agizo la kuwarudisha shule, serikali imewaagiza wakuu wa mikoa na masheha wote kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu sana watoto wote ambao hawaendi shule na kuwarudisha haraka.

Anasema ni aibu katika dunia ya teknolojia ya sayansi na mawasiliano kuona wapo watoto wasiojua kusoma wala kuandika huku elimu hiyo katika sera ya serikali ikitolewa bila ya malipo.

“Tumewaagiza walimu wakuu wote wa shule kujipanga na kuwapokea wanafunzi watakaorudishwa shule kuhakikisha wanajumuishwa na wenzao na kuendelea na masomo bila ya kubaguliwa,” anasema Simai.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Khamis anasema mradi umeanza kwa kufanikiwa kuwarudisha shule wanafunzi 2,609 wakiwemo wanawake 1,978 na wanaume 631 ikiwa ni sehemu ya juhudi zilizofanywa na wizara kwa kushirikiana na watendaji wa serikali za mitaa na wazazi.

Anasema tayari Wizara ya Elimu imetayarisha madarasa ambayo yatawapokea wanafunzi watakaorudishwa shule na kuwapatia huduma

nyingine za msingi ikiwemo madaftari na sare za shule.Khamis anasema kwamba utafiti uliofanywa umebaini kwamba watoto wengi waliotoroka shule ni wale wanaoishi katika mazingira magumu ya maisha kiasi kwamba wengine wanalazimika kujitafutia fedha.

“Tutawasaidia kwa kuwapatia fedha na sare pamoja na madaftari ya shule watoto wote watakaorudishwa shule kwa sababu utafiti wetu umebaini kwamba watoto hao wanaishi katika mazingira magumu,” anasema Khamis.

Mradi wa kuwarudisha shule watoto waliotoroka unafadhiliwa na taasisi hiyo kutoka Qatar ya elimu kwa wote na kugharimu jumla ya Sh bilioni 14, tayari umefanikiwa kuwatambua watoto 4,809 wasio shuleni.

“Tumewatambua wanafunzi 4,809 na wameanza kurudi shule hatua kwa hatua baada ya kufanya mashauriano na wazazi wao wengi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja,” anasema Mkurugenzi wa Elimu na Mipango wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Khalid Masoud Waziri.

Vijiji vya Nungwi, Matemwe na Pwani Mchangani kwa upande wa Unguja na Micheweni kwa Pemba vinatajwa watoto wengi wameacha shule na kujishughulisha na kazi za kutembeza watalii kufuatia maeneo hayo kuwa na hoteli nyingi za kitalii.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud akizungumza na masheha kuhusu utekelezaji wa mradi wa kuwarudisha shule watoto waliotoroka na wengine kujiingiza katika ajira za kutembeza watalii na uvuvi, amewapa jukumu la kupita nyumba hadi nyumba kuona watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu.

Anasema malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha watoto waliofikisha umri wa kwenda shule wanapata elimu kwa mujibu wa sheria na hakuna mtoto aliye nje ya mfumo wa elimu ya lazima.

Mahmoud anasema kuwa kipaumbele cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni sekta ya elimu na ndiyo maana mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 serikali ilitangaza elimu bila malipo kwa watoto wote wa wakulima na wafanyakazi.

Haji Hassan (13) ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Uzini, Wilaya ya Kati Unguja ambaye alitoroka shule akiwa katika darasa la nne na kuamua kurudi tena. Amezitaja sababu zilizowafanya kutoroka shule kuwa ni pamoja na kukosa sare ya shule na viatu.

“Nilikuwa sina vifaa vya shule ikiwemo sare licha ya kuwaambia wazazi wangu huku walimu wakitutaka tuvae sare na hapo ndipo nilipoamua kutoroka ili kukimbia adhabu za walimu,” anasema Hassan.

Aidha, Iddi Juma (16) ni mwanafunzi aliyeamua kurudi shule baada ya kukimbia katika Shule ya Msingi Fukuchani mkoani Kaskazini Unguja akiwa katika darasa la nne.

Ameamua kurudi shule baada ya wazazi wake ikiwemo kaka zake kumbana na kumkamilishia baadhi ya mahitaji yake ikiwemo sare na viatu.

‘’Nilikimbia shule na kwenda kuvua samaki lakini nyumbani kaka zangu wamenitaka haraka nirudi shule kwa kunitafutia mahitaji na ndiyo maana nimeanza kuhudhuria darasani,” anasema Juma.

Baadhi ya wazazi waliohojiwa walikiri watoto wao kutoroka shule huku wengine wakizurura mitaani na wengine kutembea maeneo ya fukwe na kuwafuata watalii.

Mzee Faki Mohamed ambaye watoto wake wawili walitoroka shule kwa zaidi ya miaka miwili hadi ulipokuja mradi wa kuwarudisha shule watoto unaotekelezwa na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na taasisi hiyo ya Qatar, wamerudi shuleni.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/36d0f8e0cc98e60387bd7d6a55ff921e.png

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi