loader
Kuna maisha hata baada ya sikukuu

Kuna maisha hata baada ya sikukuu

DESEMBA 25 Wakristo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Krismasi.

Wapo walioshereheka wakizingatia kuwa, Krismasi ni hasa tafakari ya kiroho inayotaka mtu azaliwe upya kwa mawazo, maneno na matendo kama yalivyo mapenzi ya Mungu.

Kadhalika, wapo walioitumia sikukuu hii kwa ulevi, uzinzi na uasherati na wengine wakakung’uta ‘vibubu’ vyao kuhakikisha hawabakizi hata senti moja kwa ajili ya kesho wakisahau kuna maisha hata baada ya sikukuu.

Kimsingi, Jumamosi ijayo sikukuu ya kuuaga mwaka 2021 na kuuanza mwaka 2022 (Mwaka Mpya) itakuwa ‘hewani’.

Hii pia ni sikukuu ya kuutafakari upendo wa Mungu, maana kumaliza mwaka ni kazi ngumu na isiyowezekana bila mapenzi ya Mungu mwenyewe.

Kwangu mimi, Waafrika wa EAC wanywe, wale na kucheza huku wakizingatia kuwa, Januari na Februari ni ‘miezi mirefu na migumu’ inayohitaji fedha nyingi, hivyo wawe makini katika matumizi.

Ikumbukwe kuwa, baada ya Sikukuu ya Mwaka Mpya, wazazi na walezi wengi huingia katika jukumu zito la kupeleka watoto shule na hivyo kuhitaji fedha nyingi.

Kwa wengine pia, huu ni msimu mpya wa kulipa pango la nyumba, kodi, tozo au michango mbalimbali ya kijamii na kiserikali na ni kipindi ambacho lazima maisha yaendelee.

Hivyo, ni aibu baada ya sikukuu mtu kuanza kutembeza vitu kuweka rehani ili kupata mkopo ukiwamo wa kufanya marejesho ya mkopo mwingine eti kwa sababu katika sikukuu alitumia kama vile anakaribia kufa.

Itakuwa aibu kwa mwana EAC yeyote kuanza mwaka mpya akiwa rumande au hospitali eti kwa sababu tu ‘alilewa’ mihemko ya sikukuu na ndio maana ninasema, tusherehekee sikukuu ya Mwaka Mpya tukizingatia kuwa, ‘Kuna maisha hata baada ya sikukuu.”

Ni aibu kutumia fedha nyingi kwa ulevi na sherehe kisha ukashindwa gharama za watoto kwenda shule, kupata huduma muhimu kama chakula na matibabu. Safari hii, hili liwe aibu kwa Wana EAC wote.

EAC tusaidiane ili sikukuu zisiteketeze maisha ya watu kwa ulevi unaosababisha ugomvi, ajali, majeruhi na hata vifo, bali kutafakari tunatoka wapi, tupo wapi na tunakwenda wapi kwa maendeleo ya kiroho na kimwili.

Familia, jamii na hata nchi za EAC ziimarishe umakini ili wahalifu wasitumie Mwaka Mpya kufanya uhalifu ukiwamo wizi, ujambazi, ubakaji na hata ugaidi maana, kuna maisha baada ya sikukuu.

Kila mmoja apime na kulinganisha kiwango cha fedha alizotumia kwenye sikukuu na kilichobaki sambamba na uwezo wa kumudu mahitaji mengine muhimu na ya lazima baada ya sikukuu.

Kimsingi, ni udhaifu wa kusukumwa na mihemko ya sikukuu, kisha mtu akaanza ‘kutembeza bakuli’ kuomba misaada na mikopo ukomeshwe maana kuna maisha hata baada ya sikukuu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5c2da96a82af7677494d152a71a6afda.jpeg

SERIKALI kupitia Shirika ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi