loader
Kadi mbili zawaficha wanaowapa mimba wanafunzi

Kadi mbili zawaficha wanaowapa mimba wanafunzi

WANAFUNZI waliopata ujauzito wilayani Kilwa mkoani Lindi, wanadaiwa kuandikisha majina tofauti ya wanaume kwenye kadi za kliniki kuwalinda wanaume waliowapa ujauzito.

Inawezekana mbinu hii ya kihalifu ikaonekana zaidi wilayani Kilwa kwa kuwa mamlaka zimechukua hatua ya kuchunguza

lakini inawezekana inatumika katika maeneo mengi nchini na kupitia makala haya, hatua zinapaswa kuchukuliwa katika wilaya zote nchini.

Fauz Issa, Ofisa Mtendaji Kata ya Miteja anasema kutokana na changamoto hiyo ya watoto kutaja mwanamume zaidi ya mmoja aliyempa ujauzito hivyo inawawia vigumu hata polisi kumtia hatiani mhusika.

Wasichana hao wanadaiwa kuwa wasiri na wakati mwingine wanafikia kuwa na kadi mbili hadi nne zinazowatambulisha wanaume tofauti.

“Matukio ya ukatili wilayani humu ni mengi hasa ya watoto na wanafunzi kupewa ujauzito. Licha ya kuwa Jeshi la Polisi wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wanawatia hatiani wahusika ili kukomesha matukio hayo, changamoto ni kwa wanafunzi wenyewe kuwakuta na kadi zenye majina tofauti tena majina yenyewe wala hayajulikani hapa eneo letu.

“Wengine huenda mbali na kutaja madereva wa malori, ukimbana utasikia mimba ya dereva wa lori, nani utasikia wala simjui na ni kama mtindo sasa hivi kila binti anayepata mimba kisingizio dereva wa malori,” anasema Issa.

Issa anasema lengo ni kumlinda mwanamume aliyempa mimba asifahamike lakini asichukuliwe hatua kwa sababu shahidi namba moja wa kesi hiyo ni mjamzito.

Pia anasema wamekuwa na tabia ya kuwasingizia walimu wao kuwa ndio waliowapa ujauzito ili kulinda wasiripotiwe polisi au kuchukuliwa hatua za kufukuzwa shule.

“Mwanafunzi akiona amebanwa na mwalimu anataka kumfukuza shule, anasingizia mwalimu ndiye amempa mimba lakini baadaye akijifungua unakuta aliyemtaja si mhusika kabisa.”

Diwani wa Miteja, Ibrahim Msati anasema familia zimekuwa zikipeleka polisi kesi za ujauzito baada ya kushindwana kwenye malipo na mara nyingi wanaingia kwenye makubaliano ya kumalizana kifamilia wakati kesi ikiwa mahakamani.

“Wakati mwingine mtuhumiwa anatoroshwa na ndugu na wasichana huwa wanadanganya kuwa walibakwa na hawakumbuki waliowabaka wakati si kweli wanafanya hivyo kuwalinda watuhumiwa, wakitofautiana kwenye malipo ndio linabumburuka, kumbe mzigo ulikuwa wa kijana wa fulani,” anasema.

Mmoja wa mzazi ambaye mtoto wake aliyetarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana (2021), lakini alikatisha masomo kutokana na ujauzito, Mohamed Said Banji, anasema: “Nilimhoji baada ya kugundua kuwa ni mjamzito lakini hajanipa jibu la msingi.

“Aliniambia mwanaume mwenyewe wala hamfahamu, anataja jina moja tu Salum ambaye yupo Kivinje, sasa Salum si wengi. Kwa sasa yupo Dar es Salaam kwa shangazi yake anajisikilizia ajifungue, akishajifungua basi tutaangalia namna nyingine,” anasema Banji.

Naye Ofisa Elimu Msingi, Wilaya ya Kilwa, Hussein Kitingi anasema wazazi, walezi na watoto wenyewe wanaficha wahusika na kumalizana kifamilia kitendo ambacho kinasababisha matukio hayo kuendelea kuwepo.

“Kipindi cha likizo ya corona wanafunzi 106 waliacha shule kutokana na mimba pamoja na changamoto ya mafuriko yaliyotokea katika baadhi ya kata mwaka 2020.

"Shule ni sehemu ya malezi, Walimu wanaporudiarudia baadhi ya mambo wanawakumbusha watoto pia. Ila mtoto anapokuwa nyumbani malezi ya sasa ni tofauti kidogo,” anasema Kitingi.

Takwimu zasikitisha:

Takwimu za Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia, Kilwa, zinasema ukatili wa kingono ni masuala yale yote yanayohusisha mambo ya kingono. Kwa mfano watoto wengi walibakwa, kulawitiwa, kupewa mimba, mashambulio mengine ya aibu na kufanya watoto wengi kukatisha ndoto zao kipindi cha likizo ya corona.

Takwimu hizo zinaonesha katika kipindi cha Julai 2020 hadi Septemba 2021, jumla ya matukio ya mimba za utotoni 102 yaliripotiwa pamoja na matukio 23 ya ubakaji.

“Kesi za mimba zilizofika mahakamani ni 50 zilizofanikiwa ni 42, zilizoshindwa ni nane na za ubakaji na ulawiti zilizoenda mahakamani ni 20. Matukio ya mimba 52 yapo kwenye ngazi ya polisi sababu watuhumiwa hawakupatikana, mwenye mimba au wazazi wanawaficha waliowapa mimba watoto wao,” inaeleza taarifa hiyo.

Ofisa wa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Kilwa, Charity Ngezi, anasema changamoto kubwa ambayo wameiona katika jamii hasa kipindi watoto wakiwa likizo ni watoto wengi kujilea wenyewe huku wazazi wakibanwa na shughuli za kusaka kipato na kusababisha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto kama ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni.

“Changamoto kubwa wazazi wameacha majukumu yote kwa walimu, kwa jiografia ya huku Kilwa kwetu mazingira si rafiki mtoto anatembea kilometa 10 kwenda na kilometa 10 kurudi hapo katikati lazima atakutana na waendesha malori, bodaboda ni rahisi kudanganyika na lifti.

“Kuna uzembe pia unaofanyika nyumbani unaofanywa na wazazi kwa kuwaachia watoto kuwa huru mitaani. Ndio maana tunaona ukatili wa kijinsia umekuwa ni mkubwa lakini pia maswala ya ndoa za utotoni yanatokea kwa kiasi kikubwa,” anasema Charity.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, katika tamko lake la Aprili 2020 kuhusu virusi vya corona na athari zake kwa wanawake na watoto wa kike, alieleza kuwa watoto walikuwa katika hatari ya kupata mimba za utotoni.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hutokea majumbani na wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu au majirani.

Mwongozo wa Kisera wa Sekta ya Afya wa Kuzuia na Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (2013), utafiti wa kitaifa nchini kuhusu ukatili dhidi ya watoto ni wa kwanza na wa aina yake katika Bara la Afrika.

Matokeo ya utafiti yameonesha kwamba mara nyingi watoto wanakabiliwa na unyanyasaji wa matukio mengi na ya namna mbalimbali yanayojumuisha ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia.

Utafiti huo unapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto unabainisha kuwa watoto wengi wako kwenye hatari kubwa ya kunyanyaswa kwenye mazingira ya nyumbani na shuleni.

“Robo tatu ya watoto wanapofikia umri wa miaka 18 huwa wameathirika na ukatili wa kimwili kwa namna moja ama nyingine kutokana na ukatili wa ndugu, mwalimu au kiongozi. Takribani asilimia 30 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24 na asilimia 14 ya wanaume wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24 nchini waliripotiwa kuathirika na ukatili wa kingono angalau mara moja kabla ya kufikisha umri wa miaka 18,” inaeleza sehemu ya utafiti.

Hata hivyo, sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inawezesha jitihada za kupunguza ukatili dhidi ya watoto. Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (1998) ilitungwa kwa lengo la kulinda heshima ya mwanamke na kuweka vikwazo kwa ukatili wa kijinsia kwa kutoa adhabu kali kwa makosa ya kingono.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b729bde93500291d44e4d1081cba463f.png

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi