loader
Uwekezaji zaidi wanukia Mwanza inaposukwa upya

Uwekezaji zaidi wanukia Mwanza inaposukwa upya

MWANZA mpya itakayoonekana kwa kipindi kirefu kijacho inakuja baada ya kuzinduliwa kwa mpango kabambe wa kuusuka upya mkoa huo ambao ni kitovu cha ukanda wa maziwa makuu.

Hii ni baada ya miongo kadhaa ya kuwepo kwa mipango mikakati ya kutaka kuendeleza eneo hilo la milima lililozungukwa na Ziwa Victoria kwa kuanzishwa kwa mpango wa upimaji shirikishi jamii.

Watu kutoka katika maeneo tofauti waliitikia kwa kutoa ushirikiano uliowezesha kujengwa miundombinu ya usafiri katika maeneo yaliyokuwa hayapitiki kwa usafiri wa magari ama pikipiki.

Eneo hili lenye wingi wa samaki tofauti katika ziwa lina vivutio vingi vya kiutalii kuanzia katikati mwa jiji kwenye kilele cha mlima eneo palipokuwa makazi ya mkuu wa kwanza wa Wilaya ya Mwanza kwa utawala wa Kijerumani zaidi ya miaka 100 iliyopita panapoitwa Gunzert house.

Pia pana mti uliokuwa ukitumiwa na watawala wa Kijerumani kunyongea watu waliokuwa wakipinga utawala wao huku ndani ya ziwa kukiwa na kivutio cha wanyama wapatikanao katika Kisiwa cha Saanane kilichopo kilometa mbili Kusini Magharibi mwa jiji.

Ziwa Victoria ambayo wakazi wake Wasukuma huita Nyanza liliitwa Ziwa Victoria na Waingereza likiwa jina la malkia wa Uingereza aliyekuwa anaitwa Victoria ambaye baba yake ni Edward na mama yake Victoria Saxe. Malkia huyo alikuwa mwenye sifa akimfuatia Malkia Elizabeth.

Mwanza yenye ziwa hilo, ambalo ni maarufu kama fahari ya Afrika ni ziwa kubwa zaidi la kitropiki duniani ambapo lilipachikwa jina la Malkia Victoria wa Uingereza mwaka 1850 na Hanning Speke aliyekuwa miongoni mwa Waingereza wa kwanza kuliona ziwa hilo.

Jiji la Mwanza linaloundwa kwa pamoja na manispaa za Ilemela na Nyamagana limepokea kwa shangwe kubwa kukamilika kwa maandalizi ya kuwa na mpango kabambe wa uendelezaji wa eneo hilo linalokuwa kwa kasi siku hadi siku.

Desemba 22 mwaka jana (2021), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akiwa na Naibu wake, Dk Angelina Mabula ambaye vilevile ni mbunge wa Jimbo la Ilemela walifika jijini humo 

katika ukumbi maarufu kwa vikao vya madiwani katika halmashauri ya jiji hilo.

Madiwani wote wa halmashauri mbili za jiji na Manispaa ya Ilemela walifika kushuhudia tukio hilo la kihistoria la uzinduzi wa mpango huo.

Akitoa taarifa ya mchakato wa kupatikana kwa mpango huo kabambe ulioandaliwa na serikali kwa kushirikiana na kampuni za kikandarasi kutoka nchini Singapore, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi, Deogratias Kalimenze alisema mpango huo unatokana na msukumo wa kutekelezwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa mwaka 1970.

Kalimenze alisema mpango huo ulikusudia kuhakikisha kunakuwa na ukuaji wa miji tisa ambayo ni Dar es Salaam, Arusha, Moshi, Tanga, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Mtwara na Tabora ambapo michakato kadhaa imefanyika kwa ajili ya kutimiza malengo hayo na kwa sasa ikiwa ni mpango wa tatu uliozaa mpango huo kabambe mkoani Mwanza.

Mpango kabambe mkoani Mwanza ni wa miaka 20 kutoka 2015 mpaka 2035 ukiwa na lengo la kusimamia uendelezaji wa jiji unaozingatia uendelevu katika ukuaji wa eneo hilo.

“Baada ya huo mpango uliokuwa umejikita kubadili miji hiyo tisa Mkoa wa Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi uliingizwa katika mchakato huo,” Kalimenze aliwaambia wadau hao wa maendeleo ya Mkoa wa Mwanza.

Alisema mpango huo kabambe wa mchakato wa kupangilia Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela katika mpango endelevu kwa maendeleo ya watu na mazingira ni mpango utakaowezesha eneo hilo kuhimili ukuaji kwa muda mrefu.

Kalimenze alisema kuwa mpango huo kabambe uliopitishwa umezingatia kutazama usalama wa afya ya binadamu, mazingira na ukuaji wa kiuchumi kwa pande zote ndani ya jamii, vilevile mpango huo utawezesha eneo hilo kuwa na mpangilio mzuri wa makazi yake kwa muda mrefu na utawezesha kuwepo kwa uendelevu wa uhifadhi wa mazingira.

Akizindua mpango huo hivi karibuni jijini Mwanza, Waziri Lukuvi alisema lengo la mpango huo ni kukabiliana na changamoto ya ujenzi holela kwa makazi ya watu na utunzaji mazingira.

Lukuvi alisema kuwa kutokana na eneo hilo kukuwa kwa kasi kubwa kwa sasa wakati vile vile ni kitovu cha nchi za ukanda wa maziwa makuu ndio maana uhitaji wa kupanga eneo hilo ni muhimu kwa sasa ili kuepusha madhara ya kimazingira.

“Nataka niwaambie watu wa Mwanza kuwa kuanzia leo thamani ya ardhi yenu imepanda na wananchi wasiwe na wasiwasi kuwa mpango huo utakuwa na athari kwao bali ni neema,” alisema Lukuvi.

Alisema kuanzia sasa mamlaka zote zizuie ujenzi holela usiozingatia utaratibu wa kupata vibali vya ujenzi kutoka katika mamlaka za mipango miji ili kuepusha hasara inayoweza kupatikana kwa kubomolewa majengo hayo yasiyofuata kanuni za ujenzi.

Ofisa Mipango Miji, Jiji la Mwanza, Mosses Seleki alisema kuwa mpango huo umeandaa mazingira ambayo yatafanya eneo hilo kuwa mahiri katika sekta zote za kimaendeleo ambapo itawezesha uwepo wa miundombinu ya usafiri wa dakika 45 kufika kazini kutoka maeneo yote katika eneo hilo kwani mpango wa mabasi ya mwendokasi ama treni umeandaliwa kwa ajili hiyo.

Seleki alisema kuwa kufikia mwaka 2035 miji yote iliyo katika mpango huu itakuwa na umeme kwa asilimia 100, wakazi wake watafikia 2,400,000, ajira zipatazo 1,500,000 zitazalishwa huku pato la watu wake kwa mwaka litakuwa Dola za Marekani 4,240.

Alisema maeneo ya katikati mwa jiji yatapanuka na kufika hadi mitaa ya Mkuyuni, Mabatini, Kona ya Bwiru na Kirumba huku kukihitajika kujengwa nyumba zenye urefu wa ghorofa 20.

Hata hivyo, mpango huo hautamwathiri mmiliki wa eneo ambaye atakuwa hana uwezo wa kujenga majengo ya namna hiyo kwani sheria inamwezesha kupata mwekezaji ambaye anaweza kuingia naye ubia na kuwa sehemu ya umiliki wa majengo hayo na kuendelea kuishi katika eneo lake na huku akinufaika kupitia uwekezaji huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel alisema kupatikana kwa mpango huo unatengeneza fursa za ajira kwa watu na kuhifadhi mazingira na ikolojia.

Gabriel alisema mpango huo ni suluhisho kwa umasikini wa wakazi wa eneo hilo kwani utafungua fursa za watu wake kuwekeza kupitia rasilimali ya ardhi yao kwa wenye mitaji huku ukikata mizizi ya migogoro ya ardhi kwa watu wake.

Naye Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine alisema kuwa kupatikana kwa mpango huo ni fursa kwa watu wa eneo hilo kutumia kwa jili ya kujiletea maendeleo yao kwa haraka akibainisha kuwa vilevile ni hatua nzuri kwa uendelezaji wa ujenzi wa jiji lenye mpangilio bora.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Sekiete Yahaya alisema kuwa wamepokea kwa furaha kubwa azimio hilo la kutengeneza jiji katika mpango ambao ni endelevu katika nyanja zote za kimaisha.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kupokea kwa furaha mpango huo unaotengeneza dira ama mwelekeo wa ujenzi wa eneo hilo katika hadhi yake ya jiji na hivyo kubainisha kuwa eneo hilo litaendelea kuwa nadhifu kwa kiasi kikubwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/493d5d139f3b29a87b2012457cb5ce52.png

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Suleiman Shagata

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi