loader
Serikali yarejesha bei ya zamani kuunganisha umeme

Serikali yarejesha bei ya zamani kuunganisha umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kurudisha bei ya zamani ya kuunganishia umeme ambayo kuanzia sasa mteja wa njia moja ndani ya meta 30 kutoka kwenye miundombinu ya umeme katika maeneo ya mjini, atalipa kuanzia Sh 320,960 badala ya Sh 27,000.

Hata hivyo, shirika limesema wateja wote waliokwishalipia gharama za kuunganishiwa umeme kwa bei ya awali ya Sh 27,000 iliyotangazwa mwaka jana, wataendelea kuunganishiwa umeme kama kawaida na hawataguswa na bei mpya iliyotangazwa jana.

Meneja Uhusiano wa Tanesco, Johari Kachwamba alibainisha zaidi kwamba, mteja wa njia moja ndani ya meta 70 kutoka kwenye miundombinu ya umeme atalipa Sh 515,618 na umbali wa njia moja ndani ya meta 120 kutoka kwenye miundombinu ya umeme itakuwa ni Sh 696,670.

Gharama za kuunganisha umeme mjini ndani ya meta 30 kwa mteja wa njia tatu kutoka kwenye miundombinu ya umeme itakuwa ni Sh 912,014, kwa mteja wa njia tatu ndani ya meta 70 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh milioni 1.2 na umbali wa njia tatu ndani ya meta 120 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh milioni 1.6.

Kwa upande wa vijijini, Kachwamba alisema gharama ya kuunganisha umeme vijijini kwa wateja wa njia moja itaendelea kuwa Sh 27,000 kama ilivyoelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Meneja Uhusiano, gharama zote ambazo zimejumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ni kama ilivyotangazwa na Ewura kupitia Gazeti la Serikali taarifa namba 1020 iliyochapishwa Desemba 4, mwaka 2020.

Hatua hiyo ya Tanesco imekuja ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kumuagiza Waziri wa Nishati, January Makamba kusimamia bei ya kuunganishiwa umeme na kuhakikisha kila mwananchi anaunganishiwa umeme kwa bei inayopaswa kulingana na eneo.

Juzi, wakati akipokea Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa, Rais Samia alisema katika mazungumzo yoyote ya maendeleo suala la umeme kwa sasa kwa mwananchi si anasa bali ni lazima.

Alisema kutokana na ukweli huo, serikali imeitengeneza Tanesco iweze kupeleka umeme vijijini na kwamba serikali yake itaendelea kukopa kuhakikisha umeme unawafikia wananchi.

“Tuliharibiwa hapa katikati kwa kusema kila mwananchi atafungiwa umeme kwa shilingi 27,000, si hivyo, gharama za umeme haziko hivyo. Kuna maeneo tutafanya hivyo kuwabeba wananchi wetu lakini kuna maeneo lazima gharama irudi palepale,” alieleza Rais Samia.

Aliongeza: “Waziri umeogopa sana kusema hilo, nakusaidia nenda katekeleze. Kuna maeneo lazima gharama ya umeme ibebe uhalisia. Unapompangia leo Tanesco aende akaunge umeme kwa shilingi 27,000 kwa kila mtu, yeye anatoa wapi hizo fedha? Hana pa kuzitoa.”

Alisema ni lazima shirika hilo liunge umeme kwa gharama inayopaswa kwa kila mahali. “Juzi niliona watu wanalia kwenye televisheni wameshalipa miezi kadhaa umeme hawaungiwi, ukiuliza Tanesco wanasema hatuna nguzo, hatuna vifaa sasa shilingi 27,000 tunafanyaje,” alisema.

Alimtaka Waziri January alisimamie suala hilo ipasavyo huku akimhadharisha gharama hizo zisiende juu bali zilingane na mahitaji ya eneo husika bila kuiacha sera ya kuunganisha umeme vijijini kwa Sh 27,000.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e47abfc565bf83671e412f52435f7949.jpeg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi